Muhtasari wa Damu

Imepitiwa/Imerekebishwa Mar 2024

Damu ni majimaji mekundu yaliyopo kwenye ateri na mishipa yako. Hutoa oksijeni, maji, na virutubisho ambavyo tishu na ogani zako zinavihitaji ili kuishi. Una takribani lita 5 (zaidi kidogo ya galoni 1) za damu katika mwili wako. Wakati wote moyo wako husukuma damu katika sehemu zote za mwili wako.

Je, damu hufanya shughuli gani?

Damu ni huduma ya uwasilishaji ya mwili wako. Damu yako:

  • Hubeba oksijeni, maji, na virutubishi hadi kwa tishu zote katika mwili wako

  • Hukusanya taka kutoka kwenye tishu zako na kuzibeba ili ziondolewe

  • Hubeba seli na protini ambazo husaidia kulinda mwili wako dhidi ya dutu za kigeni

Seli zote mwilini mwako zinahitaji oksijeni na maji ili kuweza kuishi. Seli zako zinahitaji virutubishi kama vile sukari, protini, na mafuta. Damu yako huchukua oksijeni kwenye mapafu, na maji na virutibishi kwenye tumbo na utumbo.

Seli zako huzalisha taka mwili pale zinapochakata virutubishi. Oksijeni na virutubishi hugeuka kuwa kaboni dioksidi na taka mwili za kemikali ambazo huwa sehemu ya mkojo. Damu yako husafirisha kaboni dioksidi hadi kwenye mapafu, ambapo hutolewa nje kwa njia ya kupumua. Taka mwili husafirishwa hadi kwenye figo zako, ambapo huchujwa kutoka kwenye damu na kuingia kwenye mkojo. Damu yako pia husafriisha taka mwili zingine hadi kwenye ini kwa ajili ya kuchakatwa zaidi na kuondolewa.

Mfumo wa kingamwili wako ni mfumo wa ulinzi wa mwili wako dhidi ya vivamizi kama vile viini vya maradhi na seli za saratani. Damu yako husafirisha seli na protini maalumu za mfumo wa kingamwili hadi pale zinapohitajika.

Je, kuna nini katika damu?

Damu imeundwa kwa:

  • Kimiminiko (plasma)

  • Seli nyekundu za damu

  • Seli nyeupe za damu

  • Chembe sahani

Seli nyeupe na nyekundu za damu na chembe sahani hutengezwa wakati wote katika uboho wa mifupa yako, ndani ya mifupa yako.

Plasma

Sehemu kubwa ya plasma ni maji. Plasma pia hubeba madini muhimu na chumvi (elektroliti) na protini mbalimbali zenye manufaa. Baadhi ya protini husaidia kugandisha damu. Protini zingine huvamia vivamizi kama vile viini vya maradhi.

Seli nyekundu za damu

Seli nyekundu za damu hujumuisha kiini chekundu kinachoitwa hemoglobini. Wakati damu inapotiririka kwenye mapafu yako, hemoglobini huchukua oksijeni ili kuipeleka kwa tishu zako. Pia hemoglobini hubeba kaboni dioksidi na kuirejesha kwenye mapafu ili itolewe nje.

Seli nyeupe za damu

Seli nyeupe za damu ni sehemu ya mfumo wako wa kingamwili Seli nyeupe za damu husafiri kupitia damu yako ili kutafuta na kupambana na vitu vigeni kama vile viini vya maradhi na seli za saratani. Mara zinapopambana na kitu fulani, kwa kawaida seli nyeupe za damu hukikumbuka ili ziweze kupambana nacho kwa haraka zaidi wakati mwingine kitakapojitokeza.

Chembe sahani

Chembe sahani ni vipande vidogo sana kuliko seli nyekundu au nyeupe za damu. Hufanya kazi kwa kushirikiana na protini kwenye damu yako ili kuisadia damu yako kuganda ili uweze kuacha kuvuja damu.

Je, ni matatizo gani yanaweza kutokea katika damu yako?

Mara nyingi matatizo ya kawaida hujumuisha:

  • Kuwa na kiasi kikubwa sana au kidogo sana cha seli nyekundu za damu

  • Kuwa na kiasi kikubwa sana au kidogo sana cha seli nyeupe za damu

  • Kuwa na kiasi kikubwa sana au kidogo sana cha chembe sahani

Kuwa na kiasi kidogo sana cha seli nyekundu za damu (anemia) husababisha udhaifu na uchovu kwa sababu tishu za mwili wako haziwezi kupata oksijeni ya kutosha. Kuwa na kiasi kikubwa sana cha seli nyekundu za damu kunaweza kusababishwa na tatizo la kiafya linaloitwa polisithemia vera.

Kuwa na kiasi kidogo sana cha seli nyeupe za damu hukufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi. Kuwa na kiasi kikubwa sana cha seli nyeupe za damu inaweza kuwa ni dalili ya aina ya saratani ya damu inayoitwa lukemia.

Kiasi kidogo sana cha chembe sahani huongeza hatari yako ya kuvuja damu baada ya kupata majeraha, kufanyiwa upasuaji, au hata bila sababu yoyote. Kuwa na kiasi kikubwa sana cha chembe sahani hufanya iwe vigumu kwa damu yako kuganda kawaida. Hali hii inaweza kusababisha damu kuganda kupita kiasi au upungufu wa kuganda kwa damu.