Keratosis pilaris ni nini?
Keratosis pilaris ni tatizo ambalo seli za ngozi zilizokufa kutoka kwenye tabaka la juu la ngozi yako huziba vinyweleo vya nywele katika ngozi yako, hivyo kusababisha viuvimbe vidogo vidogo.
Keratosis pilaris imezoeleka na haina madhara
Mara nyingi hutokea kwenye hali ya hewa ya baridi na hupungua makali wakati wa majira ya joto
Ngozi yako inaweza kuonekana yenye kuparuza kwa sababu ya viuvimbe
Madaktari wanaweza kutibu kuwasha/mwasho au wekundu utokanao na keratosis pilaris kwa kutumia losheni za ngozi au matibabu ya leza
Je, nini husababisha keratosis pilaris?
Madaktari hawana uhakika wa ni nini husababisha keratosis pilaris, lakini kurithi kunaweza kuchangia hili. Haionekani kuwa ni tatizo la mzio au mfumo wa kingamwili.
Watu wenye ukurutu wana nafasi kubwa ya kupata keratosis pilaris.
Zipi ni dalili za keratosis pilaris?
Dalili za keratosis pilaris hujumuisha:
Viuvimbe vidogo vidogo vyenye rangi ya ngozi au vyekundu, hasa kwenye sehemu ya juu ya mikono, mapaja, na makalio, na wakati mwingine usoni
Wakati mwingine, kuziba kwa sehemu ya kati ya viuvimbe vyenye kufanana chunusi
Ngozi yako kuwa nyekundu na yenye kuwasha
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina keratosis pilaris?
Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una keratosis pilaris kwa kuchunguza ngozi yako.
Je, madaktari wanatibu vipi keratosis pilaris?
Mara nyingi, keratosis pilaris haihitaji matibabu. Ikiwa kuwasha/mwasho au wekundu unakupa wasiwasi, madaktari wanaweza kuitibu kwa kutumia:
Vilainisha ngozi vyenye asidi ya glaikoliki na ya laktiki
Wakati mwingine, matibabu ya leza ili kupunguza wekundu