Ukurutu (eksema) ni nini?
Ugonjwa wa ngozi ni istilahi ya jumla inayorejelea mwasho na uvimbaji wa kawaida wa ngozi.
Ukurutu, pia unaitwa eksema, ni aina ya muda mrefu ya ugonjwa wa ngozi ambao kwa kawaida upo kwenye familia. Usababisha upele wa mabaka ambao unafanya ngozi yako iwashe, iwe nyekundu, yenye ukurutu na kavu.
Eksema imeenea sana, hasa kwa watoto, watu wengi wanaipata kabla ya umri wa miaka 5
Inapatikana sana kwa watu wenye mzio wa chakula, homa, au asthma na kwa kawaida inarithishwa kwenye familia
Inatibiwa kwa dawa inayowekwa kwenye ngozi na kwa kuepuka vitu vinavyofanya hali iwe mbaya zaidi
Kwa kawaida eksema inaondoka au inakuwa nafuu kadiri unavyokua
Nini kinachosababisha eksema?
Madaktari hawajui kinachosababisha eksema, lakini inarithishwa kwenye familia.
Watu wenye asthma, homa, au mzio wa chakula wana uwezekano mkubwa wa kupata eksema. Eksema haiwezi kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mambo mengi yanaweza kuchochea eksema yako au kufanya hali iwe mbaya zaidi:
Msongo wa mawazo
Mabadiliko katika hali joto au hali ya hewa
Maambukizi ya ngozi kutokana na bakteria
Wadudu wa kwenye vumbi, kuvu na mba
Aina fulani za vipodozi
Nguo zinazosugua ngozi yako, hasa sufu
Kwa watoto wachanga, wakati mwingine mzio wa chakula
Dalili za eksema ni zipi?
Dalili za eksema ni tofauti kwa watoto wachanga ikilinganishwa na watoto na watu wazima.
Kwa watoto wachanga wenye eksema, upele:
Ni mwekundu, una majimaji, wenye magamba na kuwasha
Unaanza usoni na kuenea shingoni, kwenye ngozi ya kichwa, viganjani, mikononi, kwenye miguu na makanyagio
Unaweza kuenea kwenye eneo kubwa sana la mwili
Unaweza kudumu kwa miezi kadhaa kabla hali haijawa nzuri
Kwa watoto na watu wazima wenye eksema, upele:
Unawasha sana
Kwa kawaida unaonekana kwenye sehemu moja tu au sehemu kadhaa, hasa kwenye mikono yako, mikono ya juu, mbele ya viwiko vyako, nyumba ya magoti yako au kuzunguka macho yako
Unaweza kuibuka tena na tena, kwa kawaida katika maeneo yaleyale
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Ikiwa una eksema, ngozi yako inaweza kuwa nene pale unapoikuna sana. Kukuna ngozi yako iliyo wazi kunaweza kusababisha maambukizi.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina eksema?
Madaktari wanaweza kugundua eksema kwa kuangalia upele na kukuuliza kuhusu historia yako binafsi na ya familia.
Madaktari wanatibu vipi eksema?
Madaktari hawawezi kutibu eksema, lakini ili wakusaidie dalili zako, wanaweza kupendekeza kwamba:
Upake dawa, kama vile kotikosteroidi na krimu nyinginezo, ili kupunguza mwasho na kutibu ngozi yako
Iweke ngozi yako iwe na unyevu kwa kukanda kwa maji baridi, losheni, mafuta ya mgando au mafuta ya mbogamboga baada ya kuoga.
Oga mara moja tu kwa siku ili ngozi yako isiwe kavu
Oga maji yenye kiasi kidogo cha dawa ya kuondoa madoa, mchanganyiko wa maji na unga wa shayiri (bidhaa iliyotengenezwa kwa unga laini wa shayiri) au dawa ya lami
Futa ngozi yako iwe kavu baada ya kuoga badala ya kuisugua iwe kavu
Ikiwa eksema yako ni mbaya sana, daktari wako anaweza kukuandikia vidonge vya kotikosteroidi au dawa nyinginezo ambazo zinapunguza kasi ya mfumo wa kingamaradhi.
Ikiwa wewe ni mtu mzima, daktari wako anaweza kujaribu tiba ya nuru. Kwa kutumia tiba ya nuru ngozi yako inawekwa katika mwanga mkali zaidi (sawa na mwanga unaotumiwa kuweka ngozi juani). Madaktari kwa kawaida hawatumii tiba ya nuru kwa watoto au vijana wadogo wenye eksema.
Ninawezaje kuzuia aksema isiwe katika hali mbaya zaidi?
Ili kusaidia kuzuia aksema isiwe katika hali mbaya zaidi:
Usijikune
Tumia vilainisha ngozi ili ngozi yako isiwe kavu
Epuka vitu vinavyowasha ngozi yako
Epuka vyakula vinavyokupa mzio
Epuka kutokwa jasho na hali joto za joto la juu zaidi au za baridi zaidi
Vaa nguo laini za pamba na epuka sufu na mavazi mengine magumu
Tumia vilainisha hewa kwenye nyumba ili kufanya hewa iwe na unyevu
Jaribu kupunguza msongo wa kihisia