Granuloma Annulare

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2023

Granyuloma anulea ni nini?

Granyuloma anulea ni athari za ngozi zisizo hatarishi ambazo husababisha uvimbe mdogo, imara ulioinuliwa kwenye ngozi. Uvimbe huunda kizingo chenye ngozi iliyodidimia kawaida au kidogo katikati ya kizingo.

  • Granyuloma anulea huwapata zaidi wanawake

  • Unaweza kuwa na kizingo kimoja au vizingo vingi

  • Granyuloma anulea mara nyingi hupona pasipo matibabu

Je, nini husababisha granyuloma anulea?

Madaktari hawajui chanzo cha granyuloma anulea. Inaweza kuwa ni athari ya mfumo wako wa kingamwili.

Zipi ni dalili za granyuloma anulea?

Dalili hujumuisha uvimbe mdogo, imara ulioinuliwa ambao hutokea kwenye nyayo, miguu, mikono, au kidole chako katika umbo la kizingo. Uvimbe unaweza kuwa wa bluu, njano, au wenye rangi ya ngozi. Vinaweza kuwa laini.

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina granyuloma anulea?

Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una granyuloma anulea kwa kutazama ngozi yako. Ili kufahamu kwa hakika, madaktari wanaweza kuondoa kipande cha tishu kwa uchunguzi (kuchukua kipande kidogo cha ngozi ili kukichunguza kwenye hadubini).

Je, madaktari wanatibu vipi granyuloma anulea?

Granyuloma anulea mara nyingi hupona pasipo matibabu. Ikiwa inakupa wasiwasi, madaktari wataitibu kwa kutumia:

  • Malai ya kotikosteroidi au kuchoma sindano

  • Malai ya ngozi kwa ajili ya kutibu athari za kingamaradhi

  • Tiba ya mwanga na dawa za kufanya ngozi yako iathiriwe zaidi kwa mwanga

  • Dawa nyingine au tiba ya leza