Erythema nodosum ni nini?
Erythema nodosum ni athari ya kuvimba kwa tabaka la mafuta chini ya ngozi. Husababisha uvimbe mwekundu au wa zambarau chini ya ngozi, hasa kwenye miundi yako.
Erythema nodosum huwapata sana watu wenye umri wa miaka 20 na 30 hasa wanawake
Mara nyingi husababishwa na athari za dawa au maambukizi
Mbali na uvimbe kwenye ngozi yako, unaweza kupata homa na maumivu ya viungo
Kwa kawaida huwa yanapona yenyewe ndani ya wiki 3 hadi 6
Je, nini husababisha erythema nodosum?
Sababu za kawaida ni pamoja na:
Maambukizi, ikijumuisha maambukizi ya streptococcal
Sakoidosisi (ugonjwa ambao husababisha mabonge madogo madogo ya seli za kingamaradhi kuota katika ogani zako nyingi)
Sababu zisizo za kawaida:
Baadhi ya dawa, ikijumuisha dawa za kuua bakteria na dawa ya kuzuia mimba
Ujauzito
Ugonjwa wa Behçet—ni kuvimba kwa muda mrefu (uvimbe) kwa mishipa ya damu kunakoweza kusababisha vidonda vya uchungu kwenye mdomo na viungo vya uzazi, malengelenge kwenye ngozi, na mara nyingine matatizo kwenye macho, viungo, au ogani zako
Saratani fulani
Zipi ni dalili za erythema nodosum?
Dalili zinajumuisha:
Uvimbe mwekundu au wa zambarau wenye uchungu, mara nyingi kwenye miundi yako
Homa
Maumivu ya viungo
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina erythema nodosum?
Mara nyingi madaktari wanaweza kufahamu kuwa una erythema nodosum kwa kutazama uvimbe ulio kwenye ngozi yako. Mara nyingine ili kuwa na uhakika wataondoa kipande cha tishu kwa uchunguzi (kuondoa kipande kidogo cha tishu ili kukichunguza kwenye hadubini).
Ili kufahamu chanzo cha erythema nodosum yako, wanaweza kufanya vipimo vingine, kama vile:
Eksirei ya kifua
Vipimo vya damu
Kipimo cha ngozi kwa ajili ya kifua kikuu
Je, madaktari wanatibu vipi erythema nodosum?
Erythema nodosum hupungua makali yenyewe baada ya wiki 3 hadi 6 Ikiwa hali yako ya erythema nodosum inasababishwa na maambukizi, madaktari watatibu maambukizi. Yafuatayo yanaweza kukusaidia kupunguza maumivu:
Kupumzika kitandani
Kujiwekea kitu cha baridi
Kuacha mguu wako ukiwa umenyanyuliwa
Kutumia dawa ya kupunguza uvimbe isiyo na asteroidi (NSAID—kama vile aspirini au ibuprofeni)
Wakati mwingine, daktari wako anaweza kukupatia potasiamu iodidi ili kupunguza dalili
Waka mwingine, kotikosteroidi (dawa ya kupunguza kuvimba)