kandidiasisi ni nini?
Kandidiasi ni maambukizi yanayosababishwa na Chachu ya Kandida. Kwa sababu chachu ni aina ya kuvu, kandidiasi ni maambukizi ya kuvu, lakini mara nyingi huitwa maambukizi ya chachu. Chachu ya Kandida mara nyingi huishi kwenye mwili wako kwa kiasi kidogo pasipo kuonyesha dalili zozote. Lakini wakati mwingine zinaweza kukua kupita kiasi au maambukizi yanaweza kutokea.
Maambukizi ya chachu mara nyingi hutokea kwenye sehemu ya juu ya mwili wako, ikiwemo ngozi, mdomo, au uke wako
Wakati mwingine watu wenye mfumo wa kingamwili ambao ni dhaifu hupata maambukizi ya chachu kwenye ogani zao za ndani (kandidiasi inayoenea kwa hatua), hali ambayo inaweza kutishia maisha
Maambukizi ya chachu yanaweza kusababisha wekundu, upele, kuwasha/mwasho, kuvimba, au madoa meupe yenye rangi ya malai
Baadhi ya upele utokanao na nepi husababishwa na maambukizi ya chachu
Madaktari hutibu maambukizi ya chachu kwa kutumia malai au dawa za kumeza
Je, nini husababisha maambukizi ya chachu?
Maambukizi ya chachu husababishwa na chachu ya Kandida, kuvu ambayo kwa kawaida huishi mwilini mwako kwa kiasi kidogo. Ikiwa katika kiasi kidogo, huwezi kuitambua. Ikiwa chachu itaongezeka kwa kiasi kikubwa, unapata kipele.
Baadhi ya sababu za chachu kuongezeka kwa kiasi kikubwa hujumuisha:
Kuvaa nguo za ndani zenye kubana, sidiria, au nguo nyingine ambazo huweka jasho karibu na mwili wako
Kuwaacha watoto wachanga wakiwa na nepi zilizolowa au chafu kwa muda mrefu
Kuwa na kisukari
Kuwa na mfumo wa kingamwili ambao ni dhaifu kwa sababu ya matatizo kama vile maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi au saratani
Kutumia dawa za kuua bakteria
Chachu hupenda kuishi gizani, kwenye maeneo yenye unyevunyevu mwilini mwako Hivyo, maambukizi ya chachu hutokea sana katika maeneo haya:
Chini ya mikunjo ya ngozi kwa watu ambao ni wanene sana
Mdomoni
Chini ya matiti ya wanawake
Kwenye eneo la kinena au uke
Zipi ni dalili za maambukizi ya chachu?
Dalili hutegemea eneo lenye maambukizi ya chachu:
Kwenye ngozi yako: Upele mbichi, wenye wekundu wa kung'aa
Ndani ya uke wako: Madoa meupe na vitu vyeupe mfano wa jibini kutoka ukeni
Mdomoni mwako: Madoa meupe (kuvimba ndani kwa ndani)
Kwenye pembe ya mdomo wako: Mpasuko kwenye ngozi
Madoa meupe yenye rangi ya malai huonekana mdomoni na yanaweza kuvuja damu iwapo yatakwanguliwa. Ugunduzi huu ni uvimbaji wa kawaida wa ndani kwa ndani, ambao husababishwa na maambukizi ya Kandida.
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Picha hii inaonyesha kuvimba na kupasuka kwa pembe za midomo (wakati mwignine huitwa perlèche) kunakosababishwa na maambukizi ya Kandida katika pembe za mdomo.
© Springer Science+Business Media
Maambukizi ya kucha yanayosababishwa na Kandida yanaweza kuathiri pleti za kucha (onychomycosis—inayoonekana chini ya kucha), ncha za kucha (paronychia), au vyote.
Picha kwa heshima ya CDC/Sherry Brinkman kupitia Maktaba ya Picha za Afya kwa Umma ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Picha hii inaonyesha upele uliosababishwa na chachu ya Kandida.
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Picha hii inaonyesha kuvimba na wekundu wa uke na vitu vyeupe vinavyotoka kwenye uke kwa sababu ya maambukizi ya chachu.
WASHIRIKA WA BIOPHOTO/MAKTABA YA PICHA ZA KISAYANSI
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina maambukizi ya chachu?
Madaktari kwa kawaida wanaweza kujua ikiwa una maambukizi ya kuvu kwa kuiangalia tu. Ili kufahamu kwa hakika, daktari anaweza kubandua sehemu ndogo sana ili kuitazama kwenye hadubini.
Je, maambukizi ya kuvu hutibiwa vipi?
Matibabu hutegemea mahali yalipo maambukizi ya chachu.
Kwa maambukizi ya kwenye ngozi yako, madaktari watakufanya:
Upake malai, poda, au bidhaa nyingine zenye dawa ya kuua kuvu kwenye eneo lenye maambukizi
Uweka ngozi yako katika hali ya ukavu (kwa mfano, kwa kubadilisha nepi za mtoto mchanga kila mara)
Utumie dawa za kumeza, ikiwa maambukizi ni makali
Kwa maambukizi ya chachu kwenye uke wako, madaktari watakufanya:
Upake malai ya dawa ya kuvu ndani na nje ya uke wako
Wakati mwingine, umeze dawa
Kwa uvimbe wa ndani kwa ndani kwa watu wazima, madaktari watakufanya:
Utumie dawa ya kuvu
Wakati mwingine, usukutue kwa dawa ya kuvu ya kiowevu (nystatin)
Kwa uvimbe wa ndani kwa ndani kwa watoto wachanga, madaktari watakufanya upake dawa ya kuvu ya kiowevu mdomoni mwa mtoto wako mchanga.