Limfedema ni nini?
Limfu ni majimaji yanayotoka kwenye mishipa yako midogo zaidi ya damu. Majimaji huingia katikati ya seli zako na huleta virutubishi na kubeba seli zilizoharibiwa, seli za saratani, na viini vilivyoangamizwa. Kisha limfu husafiri kupitia bomba ndogo zinazoitwa mishipa ya limfa. Mishipa hubeba limfu kutoka kwenye tishu zako hadi kwenye sehemu za mkusanyiko zinazoitwa tezi/vinundu vya limfu.
Limfedema ni kuvimba kwa mkono au mguu kwa sababu mtiririko wa limfu umezuiwa.
Kwa kawaida limfedema hutokea kutokana na kuwa na mishipa ya limfu au tezi za limfu zilizoondolewa au kuharibiwa (kama vile wakati wa upasuaji au mionzi ya saratani)
Ni nadra sana kuwa ni kasoro ya kuzaliwa nayo
Limfedema haina tiba, lakini aina maalum ya ukandaji pamoja na soksi na bandeji za shinikizo zinaweza kukusaidia kupunguza uvimbe
madaktari na wauguzi hujiepusha kutoa damu, kupima shinikizo la damu, au kupitisha vitu kwenye mshipa wa mkono au mguu wenye limfedema
Je, nini husababisha limfedema?
Limfedema hutokea pale sehemu ya mfumo wako wa limfu unapoziba Kisha, limfu hujikusanya kwenye tishu, na kusababisha kuvimba.
Ni nadra, kwa watoto kuzaliwa bila mishipa ya limfu ya kutosha.
Mara nyingi, mishipa ya limfu huwa ina hali ya kawaida, lakini kitu hutokea ambacho huziziba, kama vile:
Upasuaji, kama vile madaktari wanapotoa tezi za limfu kutoka kwenye makwapa ya wanawake wanaofanyiwa upasuaji wa saratani ya matiti
Majeraha makubwa kwenye mkono au mguu
Katika nchi zinazoendelea, aina fulani ya maambukizi ya minyoo yanayoitwa matende husababisha lymphedema. Nadra, saratani ikaziba mishipa yako ya limfu.
Dalili za limfedema ni zipi?
Mkono mmoja au mguu huvimba na kuonekana umevimbavimba lakini huwa na rangi ya kawaida. Huenda ukahisi inabana, lakini haiumi. Baada ya kupata limfedema kwa muda fulani, sehemu ya ngozi yenye limfedema inaweza kuwa na rangi ya hudhurungi nyeusi kuliko rangi ya kawaida ya ngozi yako.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina limfedema?
Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una limfedema kwa kufanya uchunguzi wa mwili. Kwa kawaida, chanzo kinakuwa bayana, kama vile upasuaji uliofanyiwa. Ikiwa madaktari hawana uhakika wa kwanini una limfedema, wanaweza kufanya vipimo vya kupiga picha, kama vile uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku), ili kutambua mahali penye kizuizi kweye mfumo wako wa limfu.
Je, madaktari hutibu vipi limfedema?
Limfedema haina tiba. Yafuatayo yanaweza kusaidia kupunguza uvimbe wako:
Kunyanyua mguu au mkono ambao umevimba ili kusaidia majimaji kutoka (kwa mfano, kuweka mguu wako juu ya stuli)
Aina maalumu ya ukandaji inayosaidia kutoa majimaji
Kusogeza mkono au mguu kama ulivyoshauriwa na daktari ili kusaidia kusogeza majimaji
Bandeji au soksi za shinikizo za kuvaa kwenye mkono au mguu uliovimba
Mara chache, upasuaji wa kuondoa tishu zilizovimba chini ya ngozi na ili kusaidia kuondoa limfu
Ni muhimu kuepuka kujeruhi mkono au mguu wenye limfedema. Pia, ikiwa una mkono wenye limfedema, usiruhusu utumike kupima shinikizo la damu au kutoa damu kwenye mkono huo. Hii inaweza kufanya hali ya limfedema kuwa mbaya zaidi.