Endokardaitisi ya kuambukiza

Imepitiwa/Imerekebishwa Oct 2024

Endokardaitisi ya kuambukizwa ni nini?

Endokardaitisi ni hali ya kuvimba kwa sehemu ya ndani ya moyo wako. Endokardaitisi ya kuambukizwa ni:

  • Maambukizi ya sehemu ya ndani ya moyo wako

Maambukizi yanaweza kuwa kwenye utando wa chemba ya moyo wako au kwenye vali za moyo wako.

  • Endokardaitisi ya kuambukizwa hutokea pale bakteria wanapoingia kwenye damu yako na kusafiri hadi kwenye moyo wako

  • Endokardaitisi ya kuambukizwa kimsingi hutokea kwenye tishu za moyo zenye kasoro, kwa mfano hutokea pale unapokuwa na kasoro ya kuzaliwa kwenye moyo au vali za moyo zilizoharibika, au ikiwa una vali ya moyo ya bandia

  • Maambukizi yanaweza kuharibu vali za moyo hivyo kushindwa kufanya kazi vizuri na kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi

  • Madaktari hufanya vipimo vya damu na echocardiografia ili kuona kama una endokardaitisi ya kuambukizwa

  • Madaktari hutibu endokardaitisi ya kuambukizwa kwa kutumia dawa za kuua bakteria na wakati mwingine kwa upasuaji wa moyo

  • Ikiwa una vali ya moyo ya bandia au kasoro ya kuzaliwa katika moyo wako, unaweza kutakiwa kutumia dawa za kuua bakteria kabla ya upasuaji au tiba ya meno ili kuzuia endokardaitisi

Je, nini husababisha endokardaitisi ya kuambukizwa?

Endokardaitisi ya kuambukizwa husababishwa na bakteria au kuvu ambao huingia kwenye damu yako na kuasfiri hadi kwenye moyo wako. Bakteria wanaweza kuingia kwenye damu yako unapokuwa na:

Una hatari kubwa ya kupata endokardaitisi ya kuambukizwa kama:

  • Ulizaliwa ukiwa na tatizo la moyo

  • Una vali ya moyo yenye kasoro au iliyoharibika

  • Kujidunga dawa za kulevya

  • Una mfumo wa kingamwili ambao ni dhaifu

  • Una vali ya moyo ya bandia, kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo, au kifaa cha kuamsha moyo uliosimama

  • Umewahi kuwa na endokardaitisi ya kuambukizwa hapo awali

Zipi ni dalili za endokardaitisi ya kuambukizwa?

Kwa kawaida endokardaitisi ya kuambukizwa huanza taratibu. Lakini wakati mwingine hutokea kwa ghafla.

Endokardaitisi ya kuambukizwa ya wastani hutokea pale endokardaitisi inapotokea taratibu, ikichukua wiki hadi miezi. Taratibu unapata dalili kama vile:

  • Uchovu

  • homa ya chini (99° to 101° F or 37.2° to 38.3° C)

  • Kupungua uzani

  • Kutokwa jasho

Endokardaitisi kali ya kuambukizwa huanza ghafla, na unakuwa mgonjwa sana kwa haraka. Mojawapo ya vali za moyo wako inaweza kuharibika vibaya ndani ya siku chache. Dalili zinajumuisha:

  • Homa kali (102° to 104° F or 38.9° to 40° C)

  • Uchovu mwingi

  • Ugumu wa kupumua

Ukiwa na aina yoyote ya endokardaitisi, unaweza pia kuwa na:

  • Baridi

  • Maumivu ya viungo

  • Ngozi ya yenye rangi iliyofifia

  • Viuvimbe uchungu chini ya ngozi yako

Wakati mwingine vitu vyenye maambukizi kutoka kwa moyo wako husambaa kupitia damu yako hadi sehemu zingine za mwili wako. Unaweza kupata maambukizi kwenye mapafu, ubongo, figo au ogani zako nyingine.

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina endokardaitisi ya kuambukizwa?

Madaktari hushuku uwepo wa endokardaitisi ya kuambukizwa kutokana na dalili zako. Ili kuthibitisha, daktari atafanya:

  • Ekokadiografia (kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti kwa moyo wako)

  • Vipimo vya damu ili kutafuta bakteria

Je, madaktari wanatibu vipi endokardaitisi ya kuambukizwa?

Madaktari hutibu endokardaitisi ya kuambukizwa kwa kutumia:

  • Dawa za kuua bakteria, zinazoingizwa kupitia vena (IV), kwa angalau wiki 2 na hadi wiki 8

  • Wakati mwingine, upasuaji wa moyo ili kurekebisha au kurudishia vali ya moyo iliyoharibika

Ninawezaje kuzuia endokardaitisi ya kuambukizwa?

Ili kuzuia endokardaitisi ya kuambukizwa:

  • Usijidunge dawa za kulevya

  • Tibu maambukizi kwa haraka

  • Tunza vizuri meno na fizi zako

Ikiwa uko katika hatari kubwa ya kupata endokardaitisi ya kuambukizwa, unapaswa kuwa makini sana na vitu hivi. Zaidi ya hayo, watu waliyo katika hatari kubwa wanaweza pia kutakiwa:

  • Kumeza dawa za kuua bakteria kabla ya tiba fulani za meno au tiba kwa njia ya upasuaji ambazo zinaweza kuruhusu bakteria waingie kwenye mwili

Muulize daktari wako kama uko katika hatari kubwa.