Laktosi ni aina ya sukari ambayo ni maziwa na bidhaa za maziwa.
Laktasi ni kimeng'enya kwenye utumbo mdogo ambacho kinameng'enya laktosi ili mwili wako uweze kunyonya.
Kutovumilia laktosi ni nini?
Kutovumilia maziwa humaanisha huwezi kuvumilia kula maziwa kwa sababu huwezi kuyameng'enya. Kushindwa kumeng'enya maziwa hutokea wakati utumbo wako mdogo hautengenezi vimeng'enya vya kutosha vya laktasi, ambavyo vinameng'enya maziwa.
Hali ya kutovumilia laktosi ipo kwa watu wengi
Kunywa maziwa au kula bidhaa za maziwa kunaweza kusababisha dalili
Dalili zinajumuisha tumbo kuvimbiwa na kukakamaa, kuharisha, kutoa gesi, na kujihisi kichefuchefu
Matibabu yanajumuisha kuepuka bidhaa za maziwa au kutumia kidonge cha laktasi
Kuwa na mzio wa maziwa ya ngo'ombe si sawa na kutovumilia laktosi. Watu wenye mzio wa maziwa ya ng'ombe wanaweza kumeng'enya maziwa vizuri lakini protini iliyo kwenye maziwa ya ng'ombe inachochea mmenyuko wa mzio.
Nini kinachosababisha kutovumilia laktosi?
Watoto wote wachanga wana laktasi kwenye utumbo wao kwa hivyo wanaweza kumeng'enya maziwa ya mama yao. Karibu kila mtu anatengeneza laktasi kidogo kadiri anavyokua. Mara baada ya kiwango cha laktasi kuwa hakitoshi tena, watu wanaanza kupata dalili za kutovumilia laktasi baada ya kula bidhaa za maziwa. Hata hivyo, watu wenye familia zinazotoka Ulaya ya Kaskazini hawaathiriwi. Watu wengi kutoka katika eneo hili wanaweza kumeng'enya bidhaa za maziwa katika maisha yao yote.
Kutovumilia laktosi kunaweza pia kuanza baada ya kupata jeraha au upasuaji kwenye utumbo wako mdogo au kuwa na tatizo lingine la utumbo.
Dalili za kutovumilia laktosi ni zipi?
Kutovumilia laktosi kunaweza kusababisha:
Tumbo kuvimbiwa na kukakamaa
Kinyesi cha kuhara chenye majimaji
Gesi
Kuhisi mgonjwa tumboni
Sauti za kunguruma au mvurugiko kwenye eneo la tumbo
Hisia ya ghafla ya kutaka kwenda haja kubwa dakika 30 hadi saa 2 baada ya kula chakula pamoja na maziwa
Kwa kawaida utalazimika kunywa aunsi zisizopungua 8 hadi 12 (mililita 250 hadi 375) za maziwa ili upate dalili. Ikiwa utapata dalili baada ya kunywa maziwa kidogo tu, pengine si kwa sababu ya kutovumilia laktosi.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa siwezi kuvumilia laktosi?
Mataktari watakushauri uache kula au kunywa maziwa kwa muda. Ikiwa dalili zako zitakoma kisha kurejea unapokula bidhaa za maziwa tena, pengine una hali ya kutovumilia laktosi.
Vipimo vingine ni nadra sana kuhitajika isipokuwa:
Dalili zako haziondoki unapoacha kutumia maziwa
Madaktari wanaweza kudhani kwamba unaweza kuwa na tatizo jingine pamoja na hali ya kutovumilia laktosi
Wakati mwingine, madaktari watafanya kipimo cha pumzi. Watakupa kinywaji cha laktosi na kupima hewa unayoitoa nje. Mchakato huu unaweza kuonyesha ni vizuri kiasi gani laktosi ilimeng'enywa.
Je, madaktari wanatibu vipi hali ya kutovumilia laktosi?
Unapaswa kucha kula vyakula vinavyosababisha dalili zako. Mtindi na jibini vina laktosi kidogo ndani yake na huenda visisababishe dalili. Unaweza kupata maziwa maalumu ambayo yana laktosi kidogo ndani yake.
Pia unaweza kutumia vidonge vya laktasi ili kuvunja laktosi unapopanga kula au kunywa maziwa au bidhaa za maziwa.
Watu ambao wanaepuka bidhaa za maziwa wanaweza kuhitaji vidonge vya kalsiamu ili kuzuia upungufu wa kalsiamu.