Muhtasari wa Mifupa Iliyovunjika

(Kuvunjika)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2023

Mifupa yote iliyovunjika inachukuliwa kuwa iliyoharibika. Haijalishi kama ni upenyu mdogo tu au mvunjiko mkubwa wenye vipande vingi

  • Mifupa iliyovunjika huleta maumivu makali sana na husababisha kuvimba

  • Mfupa wako unaweza kuonekana kana kwamba umeinama au umeondoka mahali pake

  • Wakati mwingine mifupa iliyovunjika huharibu neva au mishipa ya damu karibu na sehemu iliyovunjika

  • Madaktari hutambua mifupa iliyovunjika kwa kutumia eksirei, lakini wakati mwingine uchanganuzi wa CT au MRI unaweza kufaa

  • Madaktari hurejesha mifupa mahali panapofaa na kuishikilia hapo kwa gango, plasta, au wakati mwingine pini, skrubu na vipande vya chuma.

Nenda kwenye kitengo cha dharura kilicho karibu nawe ikiwa ulijeruhiwa na una maumivu makali au kuvimba au iwapo huwezi kusogeza au kutumia sehemu ya mwili iliyojeruhiwa.

Ni zipi aina tofauti za kuvunjika?

Madaktari hutumia istilahi nyingi kurejelea aina tofauti za mifupa iliyovunjika. Istilahi hizo zinahusiana na vitu kama vile:

  • Vipande vya mfupa uliovunjika vimepangiliwa vipi?

  • Je, kuna shimo kwenye ngozi yako na mfupa unatokeza nje?

  • Je, mvunjiko huo unakwenda kwenye mojawapo ya viungo vyako?

Vipande vya mfupa uliovunjikwa wakati mwingine hupangiliwa katika mstari ulionyooka. Lakini wakati mwingine huwa vimeinama, kukunjwa, kutenganishwa au kubanwa pamoja. Wakati mwingine mfupa wako huwa umevunjwa katika vipande kadhaa vidogo.

Mvunjiko wazi ni wakati ncha kali ya mfupa uliovunjika imedunga ngozi yako. Mara nyingi, mfupa huo hurudi ndani na kuacha sehemu ndogo iliyokatwa. Lakini wakati mwingine mfupa hubaki ukiwa umetokeza nje. Mvunjiko wazi unaweza kuruhusu vidudu vya maradhi na uchafu uingie kwenye mfupa uliovunjika na kusababisha maambukizi ya mfupa. Maambukizi ya mfupa huzuia sehemu iliyovunjika isipone.

Mvunjiko ulioingia kwenye kiungo unaweza kupona ukiwa na ncha inayoparuza ambayo inaweza kusababisha kukakamaa na maumivu ya kiungo ya kudumu.

Some Types of Fractures

Ni nini husababisha mivunjiko ya mifupa?

Mfupa wako unaweza kuvunjika iwapo:

  • Mfupa wako ukiinama au kupindwa kupita kiasi, kama vile kutokana na kuanguka au majeraha ya spoti

  • Mfupa wako ukigongwa kwa nguvu sana, kama vile na kitu kizito au dharuba kutoka kwa mgongano wa gari

  • Dharuba ya mara kwa mara kwenye mfupa, kama vile kukimbia—hii inaitwa mvunjiko unaosababishwa na mkazo

Dalili za mfupa uliovunjika ni zipi?

Dalili za mivunjiko ni kama vile:

  • Maumivu kwenye sehemu ya mwili iliyojeruhiwa inapoguswa, kuwekewa uzito, au kutumika

  • Kuvimba

  • Tatizo la kutumia sehemu ya mwili iliyojeruhiwa kwa kawaida (kwa mfano, ikiwa una mvunjiko wa kifundo cha mguu, huenda usiweze kusimama kwa mguu wako)

  • Kufa ganzi au kuwashwa wakati mwingine ikiwa neva imejeruhiwa

Mfupa uliovunjika hutoka damu. Huku kunaweza kusababisha michubuko baada ya siku moja au zaidi.

Madaktari wanawezaje kujua kama mfupa umevunjika?

Madaktari hufanya:

Wakati mwingine, daktari atafanya pia uchanganuzi wa CT au MRI.

Madaktari hutibu vipi mifupa iliyovunjika?

Mifupa iliyovunjika hupona vyema pale ambapo ncha mbili zinagusana na kulingana. Iwapo hazigusani na kulingana, madaktari wanaweza kuzisogeza ili zilingane. Huku kunaitwa "kupunguza mvunjiko," au "kusogeza mfupa."

Iwapo mvunjiko wako unasukuma mshipa wa damu au neva, au iwapo ni mvunjiko ulio wazi, madaktari watausogeza mara moja. Vinginevyo, madaktari mara nyingi husubiri siku chache ili kuruhusu uvimbe upungue. Kabla ya wakati huo, watakufunga kwa banzi na kukupa dawa ya maumivu.

Baada ya kusogeza mfupa, madaktari watashikilia vipande vilivyovunjika ili visisonge hadi vitakapopona. Ili kuzishikilia pamoja, madaktari wanaweza kutumia

  • Mabanzi

  • Plasta

  • Upasuaji

Banzi na plasta zimetengenezwa kwa nyenzo ngumu kama vile plasta au kioo-nyuzi. Madaktari huweka pedi laini kwanza ili plasta au kioo-nyuzi kisikwaruze ngozi yako. Katika plasta, nyenzo hiyo ngumu hufunika sehemu yote ya mkono au mguu wako. Katika banzi, nyenzo hiyo ngumu hufunika sehemu kidogo tu.

Wakati wa upasuaji wa mfupa uliovunjika, madaktari wanaweza kutumia:

  • Chuma ndefu inayowekwa kwenye shimo iliyopo ndani ya mifupa yako

  • Skurubu na vipande vya chuma vilivyounganishwa moja kwa moja kwenye mifupa iliyovunjika

  • Kiegemezi cha chuma nje ya mguu au mkono wako ambacho kimefungwa kwenye mifupa yako iliyovunjika (kirekebishaji cha pembeni)

Ikiwa una mvunjiko wazi, unaweza pia kuhitaji upasuaji ili kuondoa uchafu na vijidudu kwenye ncha za mifupa iliyovunjika.

External Fixator

Nitatunza plasta vipi?

Iwapo una plasta, unapaswa kufanya yafuatayo:

  • Hakikisha plasta yako ni kavu unapooga—ilinde kwa kuifunika kwa kitu kisichopitisha maji au mfuko wa plastiki (tumia pete ya elastiki kuziba mwanya)

  • Plasta likipata unyevunyevu, ikaushe kwa kikaushio cha nywele—ikiwa linalowa sana huenda daktari wako akalibadilisha.

  • Ikiwezekana, inua plasta ili kupunguza uvimbe

  • Ili kulinda ngozi yako, weka mkanda kwenye kingo zozote zinazokwaruza

  • Safisha eneo karibu na plasta yako kila siku

  • Kamwe usiingize vitu ndani ya plasta yako

Mpigie simu daktari wako ikiwa unapata homa au ikiwa plasta wako:

  • Inakubana sana

  • Inasababisha maumivu, kufa ganzi, au udhaifu kwenye sehemu ya mwili iliyojeruhi

  • Inasababisha uwekundu au uchungu

  • Ina harufu mbaya