Je, tetekuwanga ni nini?
Tetekuwanga ni maambukizi ya virusi ambayo huwapata zaidi watoto kuliko watu wazima.
Tetekuwanga husababisha homa na mwasho wa vipele vidogo, malengelenge yaliyovimba au alama za magamba
Tetekuwanga husambaa kirahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine
Kwa kawaida tetekuwanga huwa si kali sana kwa watoto wenye afya—na mara nyingi hupata ahueni pasipo shida yoyote
Kwa watu wenye mfumo dhaifu wa kingamwili, tetekuwanga inaweza kuwa kali na yenye kutishia maisha
Hata baada ya kupata ahueni, virusi vya tetekuwanga hubaki mwilini mwako
Miaka mingi baada ya kupona tetekuwanga, virusi hao hao wanaweza kusababisha mkanda wa jeshi, vipele uchungu vya malengelenge yaliyojaa majimaji
Chanjo ya tetekuwanga inaweza kuzuia tetekuwanga
Je, nini husababisha tetekuwanga?
Tetekuwanga husababishwa na virusi vya varisela-zosta.
Virusi huenea:
Kupitia hewa, kutoka kwenye matone anayokohoa au kupiga chafya mtu mwenye maambukizi
Kupitia kugusa malengelenge ya tetekuwanga
Baada ya kupona tetekuwanga, virusi hubaki mwilini mwako. Hubaki kwenye mizizi ya neva, karibu na uti wako. Wakati mwingine virusi huanza kushughulika tena na kusababisha upele (mkanda wa jeshi) kwenye sehemu ya ngozi yako iliyoungana na mzizi wa neva wenye maambukizi.
Je, zipi ni dalili za tetekuwanga?
Dalili za kwanza ni:
Homa
Maumivu ya kichwa
Kuhisi uchovu, kuumwa, na kutokuhisi njaa
Takribani siku 1 hadi 2 tangu kuanza kwa dalili, upele hutokea. Mambo yafuatayo hutokea:
Kwanza, upele hujumuisha madoa madogo, bapa yenye rangi nyekundu
Ndani ya saa 6 hadi 8, kila doa huvimba na malengelenge yanayowasha, ya duara na yaliyojaa majimaji hutokea
Kwa kawaida, upele huanzia usoni na kifuani kwako, kisha husambaa hadi kwenye mikono na miguu
Unaweza kupata madoa machache au unaweza kuwa nayo kwenye mwili wako wote, ikijumuisha ndani ya mdomo, uke na rektamu
kwa kawaida, unaacha kupata malengelenge baada ya takribani siku 5
Melengelenge mengi hugeuka kuwa magamba ndani ya siku 6 na mara nyingi hupotea ndani ya siku zisizozidi 20
Watu wenye tetekuwanga wana uwezo mkubwa wa kuambukiza (uwezekano wa kuambukiza ugonjwa kwa watu wengine) mwanzoni mwa ugonjwa huo, lakini wanaweza kuendelea kuambukiza hadi pale malengelenge yao yanapogeuka kuwa magamba.
Wakati mwingine, watu hupata maambukizi ya ubongo, mapafu au moyo kutoka kwenye tetekuwanga. Wanawake wajawazito au watu wenye mfumo dhaifu wa kingamwili wako hatarini kupata matatizo makubwa kutokana na tetekuwanga.
Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina tetekuwanga?
Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una tetekuwanga kutokana na dalili zako na upele.
Je, madaktari hutibu vipi tetekuwanga?
Kwa kawaida tetekuwanga hupungua makali bila matibabu. Ili kujihisi vizuri zaidi:
Weka vitambaa vya kuosha vilivyopoa na vyenye unyevunyevu kwenye upele ili kutuliza mwasho
Oga mara kwa mara kwa sabuni na maji ili kuzuia bakteria kuambukiza malengelenge
Kata kucha ili kuzuia kukwaruza, kwa sababu kukwaruza kunaweza kusababisha makovu na kufungua malengelenge ili kuruhusu bakteria kuingia
Tumia dawa ya antihistamini ili kupunguza mwasho
Iwapo malengelenge yatapata maambukizi ya bakteria, unaweza kuhitaji kutumia dawa ya kuua bakteria.
Madaktari wanaweza kuwapatia watoto na watu wazima ambao wako hatarini kupata maambukizi makali ya tetekuwanga dawa za kuzuia maambukizi ya virusi. Dawa hizi hupunguza makali ya dalili za tetekuwanga na kuzifanya ziondoke haraka. Dawa za kuzuia maambukizi ya virusi hufanya kazi pale tu utakapozitumia ndani ya saa 24 tangu dalili zilipoanza.
Je, ninawezaje kuzuia tetekuwanga?
Unaweza kuzuia tetekuwanga isisambae kwa watu wengine kwa:
Kupata chanjo ya tetekuwanga
Kukaa mbali na mtu ambaye ana tetekuwanga (ikiwa hujawahi kupata tetekuwanga)
Waache watoto wabaki nyumbani pasipo kwenda shule hadi pale malengelenge yatakapobadilika kuwa magamba
Kwa watu wazima, kukaa nyumbani pasipo kwenda kazini hadi pale malengelenge yatakapobadilika kuwa magamba
Chanjo ni sindano ambazo watoto na watu wazima wenye afya wanazihitaji ili kuwakinga dhidi ya maambukizi fulani. Nchini Marekani, watoto hupata chanjo yao ya kwanza ya tetekuwanga wanapokuwa na umri wa miezi 12 hadi 15 na chanjo pili ya tetekuwanga wanapokuwa na umri wa miaka 4 hadi 6. Watu wengi ambao hupata chanjo ya tetekuwanga kamwe hawatapata tetekuwanga. Ikiwa mtu ambaye alichoma chanjo ikatokea akapata tetekuwanga, kwa kawaida huwa si kali kabisa.