Maambukizi ya Virusi vya Herpesi Simpleksi

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2024

Kuna aina 8 tofauti za kirusi cha herpesi. Japokuwa herpesi simpleksi ndio pekee kati ya aina hizo, watu wengi huita tu "herpesi."

Je, maambukizi ya virusi vya herpesi simpleksi (HSV) ni nini?

Herpesi simpleksi ni maambukizi ya virusi ambayo husababisha upele/ukurutu wa malengelenge madogo, yenye uchungu ambayo hubadilika kuwa vidonda vilivyo wazi. Vidonda hupotea, lakini virusi hubaki mwilini mwako kwa maisha yako yote. Virusi vinaweza kuanza kushugulika tena na kusababisha vidonda zaidi.

  • Kwa kawaida maambukizi ya HSV husababisha vidonda kwenye mdomo au sehemu zako za siri lakini wakati mwingine huambukiza sehemu zingine za mwili, kama vile macho, ncha za vidole, na mara chache ubongo

  • Kirusi husambaa kwa mgusano, Virusi huenezwa kwa kuguswa, ikijumuisha kwa kujamiiana na wakati wa kuzaliwa ikiwa uke wa mama umeambukizwa

  • Maambukizi ya HSV yanaweza kuwa hatari kwa watoto wachanga waliozaliwa hivi karibuni na watu wenye UKIMWI

  • Unapokuwa na mlipuko wa herpesi, dawa za kuzuia virusi zinaweza kupunguza dalili zako na kuzifanya ziondoke haraka

  • Kutumia mipira wakati wa kujamiiana kunaweza kusaidia kuzuia kusambaa kwa herpesi kwa watu wengine

Je, nini husababisha maambukizi ya HSV?

Kuna aina 2 za virusi vya herpesi simpleksi. Zote husambaa kwa kugusana kimwili na mtu mwenye maambukizi.

Virusi vya herpesi simpleksi husambaa kwa urahisi, ikijumuisha kupitia:

  • Kugusa

  • Kubusu

  • Kushiriki ngono

  • Kushirikiana matumizi ya vitu kama vile taulo au nyembe na mtu mwenye maambukizi

Una uwezekano mkubwa zaidi wa kupata herpesi kutoka kwa mtu ikiwa ana vidonda. Hata hivyo, watu wenye maambukizi wakati mwingine wanaweza kusambaza virusi hata wasipokuwa na vidonda.

Ikiwa wewe ni mjamzito na una herpesi kwenye au kuzunguka uke wako, unaweza kumwambukiza mtoto wako wakati wa kujifungua hata kama huna vidonda.

Je, dalili za maambukizi ya HSV ni zipi?

Watu wengi wana kati ya:

  • Herpesi wa mdomo, ambao huathiri midomo yako na sehemu za ndani ya mdomo

au

  • Herpesi wa sehemu za siri, ambao huathiri sehemu za siri, ikijumuisha uume, ngozi ya nje ya uke au sehemu ya ndani ya uke

Herpesi ya mdomo

Dalili za maambukizi ya mwanzo ni pamoja na:

  • Vidonda uchungu vingi kwenye mdomo wako, ambavyo huduma kwa siku 10 hadi 14 na vinaweza kuuma sana kiasi kwamba usipende kula au kunywa

  • Wakati mwingine, homa, na maumivu ya kichwa au mwili

Virusi vinapoanza kushughulika tena:

  • Kwanza, utahisi mwasho, kuungua, au msisimko kwenye mdomo wako

  • Kisha, kidonda kimoja au zaidi hujitokeza kwenye ncha ya mdomo wako, mara nyingi kwenye eneo lile lile kwa kila mlipuko

  • Kidonda kwa haraka kitatengeneza upele wenye gamba ambao utajiondoa baada ya takribani siku 8 hadi 12

Kidonda cha mdomo wakati mwingine huitwa "kidonda cha mafua" au "lengelenge la homa" kwa sababu mara nyingi huchochewa na mafua au homa

Iwapo utaumwa kirahisi au utakuwa na mfumo dhaifu wa kingamwili, unaweza kupata vidonda vinavyoongezeka ukubwa na kuchukua wiki kadhaa kupona. Mwone daktari wako haraka uwezavyo.

Herpesi ya sehemu za siri

Dalili za maambukizi ya mwanzo ni pamoja na:

  • Vidonda uchungu vingi ndani na kuzunguka uke wako, uume na tundu la haja kubwa

  • Kwa wanawake, vidonda hivi wakati mwingine viko ndani ya uke—kwa kawaida hivi haviumi sana ukilinganisha na vile vilivyo nje ya uke

  • Homa au kuumwa

  • Hisia ya kuungua unapokojoa

  • Tatizo la kukojoa au kupitisha kinyesi

Virusi vinapoanza kushughulika tena, huenda:

  • Kusisimka, mwasho, au kuwashwa kwenye eneo linalozunguka uke au uume

  • Ndani ya siku chache, malengelenge yenye uchungu hutokea katika maeneo haya

kwa kawaida malengelenge hupotea baada ya wiki moja. Iwapo utaumwa kirahisi au utakuwa na mfumo dhaifu wa kingamwili, utapata vidonda vinavyoongezeka ukubwa na kuchukua wiki kadhaa kupona. Mwone daktari wako haraka uwezavyo.

Herpesi katika maeneo mengine

  • Kidole: Ncha ya kidole yenye uchungu, iliyovimba na nyekundu (mdudu wa herpesi)

  • Jicho: Kidonda chenye uchungu katika sehemu ya wazi ya mbele ya jicho (konea), yenye kuchanika, kuathiriwa na mwanga, na uoni hafifu (keratitisi ya herpesi simpleksi)

  • Ubongo: Kuchanganyikiwa, homa, mishtuko kutokana maambukizi makali ya ubongo (herpesi inayosababisha kuvimba kwa ubongo)

Watoto waliozaliwa hivi karibuni ambao walipata maambukizi ya herpesi wakati wa kuzaliwa (herpesi simpleksi ya wakati wa kuzaliwa) mara nyingi huwa wanaumwa kabla ya kufikisha umri wa wiki 4. Wanaweza kuwa na vidonda mwili mzima. Wakati mwingine virusi huambukiza ubongo wao, na kusababisha kifafa, kupoteza fahamu na kifo Herpesi katika watoto waliozaliwa hivi karibuni ni atari na yenye kutishia maisha. Hata kwa matibabu, watoto wengi hufariki.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina maambukizi ya HSV?

Kwa kawaida madaktari wanaweza kufahamu ikiwa una maambukizi ya HSV, ikiwa ni pamoja na herpesi ya mdomo au herpesi ya sehemu za siri, kwa kutegemea dalili zako. Ili kuthibitisha, huenda daktari akafanya yafuatayo:

  • Kutuma majimaji yaliyotoka kwenye kidonda kwenye maabara kwa ajili ya kupimwa

  • Fanya vipimo vya damu

Je, madaktari hutibu vipi maambukizi ya HSV?

Madaktari hawawezi kuponya maambukizi ya HSV, lakini dawa za kuzuia maambukizi ya virusi zinaweza kusaidia kuondoa dalili zako kwa haraka.

  • Dawa za kuzuia maambukizi ya virusi hufanya kazi vizuri kabisa unapozitumia mara baada ya kuona dalili ya kwanza ya kusisimka au kutojihisi vizuri, kabla ya malengelenge kutokea

  • Ikiwa utapata vidonda vyenye uchungu mara kwa mara, madaktari wanaweza kukufanya utumie dawa za kuzuia maambukizi ya virusi kila siku (tiba ya kukandamiza)

  • Ikiwa jicho lako limeambukizwa, daktari wa macho (mtaalamu wa macho) atakupatia matone ya kuzuia maambukizi ya virusi kwenye macho

Ili kukusaidia uweze kupata nafuu, madaktari wanaweza kupendekeza:

  • Utumie malai au mafuta ya ganzi ili kufanya vidonda vyako vipate ahueni

  • Utumie dawa za kutuliza maumivu (kwa mfano, acetaminophen or ibuprofeni) iwapo vidonda vyako vinauma sana

  • Kuosha sehemu hiyo taratibu kwa sabuni na maji

  • Kuweka barafu kwenye vidonda vyako

Je, ninawezaje kuepusha kusambaza herpesi ya mdomo na sehemu za siri?

Ili kuzuia kusambaza herpesi ya mdomo, ikiwa una mwasho au vidonda vya mafua:

  • Usichangie bilauri ya kinywaji

  • Usiwabusu watu au kujamiiana kwa njia ya mdomo

  • Usiruhusu mtu aguse kidonda chako

Ili kuepuka kupata au kusambaza herpesi ya sehemu za siri:

  • Vaa mpira kila wakati unaposhiriki ngono

Hata hivyo, kwa sababu herpesi inaweza kuambukiza maeneo ya sehemu za siri ambayo hayakufunikwa kwa mpira, mipira haikulindi kikamilifu.

Kumbuka kwamba, bado unaweza kusambaza herpesi kwa watu wengine, hata kama huna dalili.