Angina Isiyo Thabiti

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2023

Angina isiyo thabiti ni nini?

Angina ni maumivu, hisia ya usumbufu, au shinikizo kwenye kifua chako linalotokea wakati moyo wako haupati oksijeni ya kutosha. Ukosefu wa oksijeni husababishwa na ateri za moyo kubanwa au kuzibika (ugonjwa wa ateri za moyo). Angina kawaida huja unapofanya mazoezi mazito, kwa mfano, kwa kupanda ngazi au kupanda kilima. Hupotea baada ya dakika chache ukipumzika. Kawaida, unapata angina kila wakati unapofanya kiasi kile kile cha juhudi.

Angina isiyo thabiti ni wakati angina yako inatokea:

  • Bila wewe kutumia nguvu sana

  • Wakati hautumii nguvu kamwe

Kwenye angina isiyo thabiti:

  • Unapata maumivu au shinikizo kifuani

  • Madaktari hufanya vipimo vya damu na ECG/EKG (elektrokadiografia)

  • Daktari atakupa dawa na kukutibu ili kujaribu kuelekeza damu zaidi kwenye sehemu ya moyo wako iliyoathirika

Je, nini husababisha angina isiyo thabiti?

Moyo ni msuli unaosukuma damu. Kama ilivyo kwa misuli yote, moyo unahitaji damu ya kutosha ili kufanya kazi. Damu inayosukumwa moyoni haifikii msuli wa moyo. Badala yake, msuli wa moyo hulishwa na ateri zake zenyewe. Ateri hizi zinaitwa ateri za moyo.

Angina isiyo thabiti hutokea pale ambapo mojawapo ya ateri zako za moyo imezibwa kwa muda na damu iliyoganda.

Damu hiyo ikiacha kuganda, dalili zako hutoweka. Damu iliyoganda isipotoweka haraka, utapata shambulio la moyo. Wakati wa shambulio la moyo, musuli wa moyo ulioathiriwa hufa kwa sababu haupati damu ya kutosha. Katika angina isiyo thabiti, musuli ulioathiriwa haufi. Hata hivyo, angina isiyo thabiti ni ishara ya tahadhari ya shambulio la moyo.

Kwa kawaida, damu huganda kwenye ateri za moyo ukiwa na tatizo la atherosklerosisi:

  • Usanisi wa mishipa ya damu unajulikana kama kugandamana kwa ateri

  • Usanisi wa miship ya damu ni pale kolesteroli na utando wa mafuta mengine unarundika polepole kwenye ateri zako

  • Mrundiko huu unaitwa atheroma au utando

  • Utando unaweza kupasuka ghafla, na kusababisha donge la damu ambalo linaziba ateri

Kwenye angina isiyo thabiti, midundo ya moyo wako inaweza pia kuathiriwa, na kuufanya upige kwa haraka sana au polepole sana. Kwa nadra, moyo wako huacha kupiga kabisa (mshtuko wa moyo) na unafariki.

Je, dalili za angina isiyo thabiti ni zipi?

Dalili za angina isiyo thabiti ni sawa na za angina, lakini maumivu huwa mengi zaidi, yanadumu kwa muda mrefu, na hayapungui unapopumzika.

  • Huenda ukahisi maumivu katikati ya kifua

  • Maumivu yanaweza kusambaa mgongoni, kwenye taya, au mkono wa kushoto

  • Japo ni nadra, wakati mwinigne maumivu husambaa kwenye mkono wa kulia

  • Maumivu yanaweza kutokea kwenye sehemu moja au zaidi kati ya hizi na wala si kwenye kifua chako

  • Huenda ukahisi woga au kutokwa jasho

  • Midomo, mikono, au miguu yako huenda ikabadilika na kuwa bluu kidogo

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina angina isiyo thabiti?

Madaktari huhusisha utambuzi wa ugonjwa na dalili zako na kufanya vipimo, kama vile:

  • ECG/EKG—kipimo cha kuchunguza jins moyo wako unavyofanya kazi

  • Kufanya vipimo vya damu kuchunguza elementi fulani zinazoonyesha matatizo ya moyo

Je, madaktari hutibu vipi tatizo la angina isiyo thabiti?

Utalazwa hospitalini. Madaktari watafanya:

  • Kudhibiti mapigo ya moyo wako na shinikizo la damu

  • Kukupatia nitrogliserini ya kuweka chini ya ulimi wako na kwa njia ya mshipa ili kupunguza maumivu ya kifua

  • Kukupa dawa za kuzuia damu kuganda

  • Kukupa dawa za kufanya moyo upige kawaida

  • Wakati mwingine kufanya upasuaji (wa kufungua mshipa) ili kufungua ateri iliyozibwa

Wakati wa upasuaji wa kufungua mshipa:

  • Daktari hutia mrija mwembamba, unaoweza kupinda (katheta) kwenye mshipa wa sehemu ya juu ya mguu wako (kinena) au kwenye kifundo cha mkono

  • Katheta inasukumwa ndani kwenye ateri hadi kwenye moyo wako kisha kwenye moja ya ateri za moyo

  • Puto ndogo kwenye ncha ya katheta inatiwa hewa

  • Puto husukuma na kuzibua mshipa

  • Kisha daktari anatia mrija wenye wavu (kipanuzi) mwisho wa katheta na kuisogeza sehemu iliyozibwa.

  • Mrija wenye wavu husaidia kupanua sehemu iliyozibwa

Wakati mwingine madaktari hawawezi kufanya upasuaji wa kufungua mshipa. Wanaweza kupendekeza upasuaji wa kufungua mshipa (ambao pia unaitwa upandikizaji wa kukwepa wa ateri ya moyo au upasuaji wa kukwepa wa ateri ya moyo).

Wakati wa upasuaji wa kupandikiza mshipa:

  • Daktari huchukua kipande cha ateri au mshipa usio na tatizo kutoka sehemu nyingine ya mwili wako

  • Anapandikiza ncha moja ya kipande hicho cha ateri au mshipa kwenye aota yako (mshipa mkuu unaobeba damu kutoka kwenye moyo hadi sehemu nyingine zote za mwili)

  • Anapachika upande wa pili wa ateri yako iliyoziba bila kupitia sehemu hiyo

  • Kisha damu yako inatiririka kupitia mkondo huu mpya, bila kizuizi

Kutibu kisababishi cha angina yako isiyo thabiti

Ili kutibu tatizo lililosababisha angina yako isiyo thabiti, madaktari watakupatia:

Watakuelekeza pia ubadili tabia zozote zinazoumiza moyo wako, kama vile kuvuta sigara, kutofanya mazoezi, na kutokula lishe bora.

Ninawezaje kuzuia angina isiyo thabiti?

Epuka tabia zinazoweza kuudhuru moyo wako

  • Kula vyakula bora kwa afya, kama vile matunda na mboga na vyakula vingine vyenye nyuzinyuzi kwa wingi

  • Kula mafuta kidogo kutoka kwenye nyama, maziwa, na vyakula vilivyotengenezwa viwandani (kama vile piza iliyogandishwa au chakula kinachopashwa moto kwa maikrowevu)—zungumza na daktari wako kuhusu kiasi na aina za mafuta unazopaswa kula

  • Kupunguza uzani ikiwa unahitaji

  • Kufanya mazoezi kwa kutumia uzani au kutembea

  • Kuacha kuvuta sigara au kutumia dawa haramu—inaweza kuwa vigumu kuacha kutumia dawa hizi, kwa hivyo zungumza na daktari au mshauri wako wa kisaikolojia kuhusu jinsi ya kupata usaidizi

Kumeza dawa zako inavyofaa