Ulemavu wa Akili

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Ulemavu wa akili ni nini?

Ulemavu wa akili ni tatizo la ubongo linalosababisha kuwa na akili kidogo kuliko kawaida. Unaweza kutokea wakati mtoto wako anaendelea kukua katika mfuko wa uzazi. Ulemavu huu unaweza kuwa mdogo au mkali zaidi, lakini watu wenye ulemavu wa akili kwa kawaida wanahitaji usaidizi kiasi ili kutekeleza shughuli zao za kila siku na kujihudumia.

  • Watoto wenye ulemavu wa akili wanaweza kuwa na tofauti za kimwili, kama vile sura isiyo ya kawaida

  • Watoto wengi wanaanza kuonyesha dalili wakiwa shule ya awali, kwa kawaida wanakuwa wazito kuzungumza na kutumia sentensi

  • Matibabu yanajumuisha aina tofuati za matibabu na elimu maalumu

Ili kupunguza uwezekano wa mtoto wako kuwa na ulemavu wa akili:

  • Tumia foliti (asidi ya foliki) kabla ya kupata ujauzito na wakati ujauzito ukiwa mdogo

  • Epuka pombe wakati wa ujauzito

  • Pata huduma bora ya afya wakati wa ujauzito

  • Pata chanjo zote muhimu, hasa dhidi ya rubela

Je, ulemavu wa akili husababishwa na nini?

Ulemavu wa akili una visababishi vingi. Mara nyingi, kitu hutokea ambacho huathiri ubongo wa mtoto wako unaokua kabla ya kuzaliwa. Hii inaweza kujumuisha:

  • Matatizo ya kromosomu kama vile ugonjwa wa Down syndrome

  • Magonjwa ya kurithi kama vile ugonjwa wa Tay-Sachs

  • Aina fulani za maambukizi wakati wa ujauzito

  • Lishe duni sana wakati wa ujauzito

  • Matumizi ya pombe, dawa fulani haramu, au dawa fulani wakati wa ujauzito

Wakati mwingine, ulemavu wa akili hutokana na matatizo wakati wa kuzaliwa, kama vile:

  • Kukosa kiasi cha kutosha cha oksijeni wakati wa kuzaliwa

  • Kuzaliwa mapema sana kabla ya wakati unaofaa

Wakati mwingine, ulemavu wa akili hutokea baada ya kuzaliwa. Husababishwa na:

Je, dalili za ulemavu wa akili ni zipi?

Watoto wengine huonyesha tofauti wakati wa kuzaliwa au muda mfupi baada ya kuzaliwa, kama vile:

  • Uso usio wa kawaida au kichwa ambacho ni kikubwa au kidogo kuliko kawaida

  • Mikono au miguu yenye umbo lisilo la kawaida

Wakati mwingine watoto wanaweza kuwa na dalili za tatizo la afya, kama vile:

  • Matukio ya kifafa, udhaifu, na uchovu, au kutapika

  • Mkojo wenye harufu isiyo ya kawaida au unaonuka

  • Kukosa kula na kukua kama kawaida

  • Kuchelewa kujifunza kugeuka, kuketi, na kusimama

Huenda usione dalili hadi mtoto wako aanze kwenda shuleni na umlinganishe na watoto wengine wa umri sawa. Mtoto wako anaweza kuwa na:

  • Matatizo ya lugha, kama vile kuchelewa kuanza kutumia maneno au kuzungumza kwa sentensi kamili

  • Matatizo ya kupata marafiki na stadi zingine za kijamii

  • Matatizo ya kujivisha nguo na kufanya kazi zingine za kujitunza

  • Wakati mwingine, matatizo ya kitabia kama vile tabia ya kuhamaki au vitendo vya ukali, hasa pale mtoto anapohisi kutoridhika

  • Kwa watoto wenye umri mkubwa, kuwa mwenye kudanganywa kwa urahisi na kuruhusu watoto wengine kuwadhuru

  • Wakati mwingine, tatizo la afya ya akili kama vile wasiwasi au unyogovu, hasa ikiwa mtoto anadhulumiwa au anajitambua kuwa tofauti

Je, mdaktari wanawezaje kutambua ikiwa mtoto wangu ana ulemavu wa akili?

Kama sehemu ya uchunguzi wa kawaida wa mtoto wako, madaktari watauliza maswali ili kuhakikisha kuwa mtoto wako anakua kama ilivyotarajiwa. Ikiwa madaktari wanashuku kuwa mtoto ana ulemavu wa akili, watamtuma mtoto wako kwa:

  • Vipimo vya uwezo wa akili

  • Tathmini za uwezo wa kuzungumza, stadi za kijamii na za matumizi ya misuli

Ikiwa mtoto wako ana ulemavu wa akili, madaktari watajaribu kubaini kile kinachosababisha hali hiyo. Huenda madaktari wakafanya:

  • Upimaji wa jenetiki

  • Vipimo vya mkojo na damu

  • Eksirei za mifupa

  • Vipimo vya picha vya ubongo, kama vile MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) na EEG (umeme wa ubongo)

Je, madaktari hutibu ulemavu wa akili vipi?

Matibabu yanategemea mahitaji na uwezo wa mtoto wako. Watoto wanaweza kupokea huduma kutoka kwa timu ya wataalamu wa afya na shule, ikiwa ni pamoja na:

  • Daktari wa huduma ya msingi (kama vile daktari wa watoto)

  • Wafanyakazi wa jamii na wanasaikolojia ili kumpa ushauri nasaha

  • Mtaalamu wa matamshi, wa utendaji kazi na wa mwili ili kuwasaidia kujifunza kufanya shughuli za kila siku

  • Madaktari wataalamu wa matatizo ya ubongo na neva

  • Wataalamu wa lishe ili kusaidia na lishe bora

  • Walimu wa elimu maalum

Nchini Marekani, Sheria ya Elimu ya Watu Wenye Ulemavu (IDEA) inahitaji shule za umma kuwatathmini watoto kwa ulemavu wa akili. Pia inazitaka shule kutoa elimu ya bila malipo na ifaayo kwa watoto wenye ulemavu wa akili.