Matatizo ya Kujifunza

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Je, matatizo ya kujifunza ni nini?

Matatizo ya kujifunza ni matatizo katika uwezo wa ubongo kupata, kukumbuka, au kutumia maelezo. Matatizo haya hufanya iwe vigumu kuwa makini na kufanya vyema shuleni.

  • Watoto wenye matatizo ya kujifunza mara nyingi huwa na akili ya kawaida au ya juu lakini wanakabiliwa na matatizo katika stadi maalum ya kiakili, kama vile kusoma au kufanya hisabati

  • Matatizo ya kujifunza ni tofauti na ulemavu wa akili (watoto wanapozaliwa na akili ya chini kuliko kawaida jambo ambalo husababisha matatizo katika stadi zote za kiakili)

  • Madaktari watamtuma mtoto wako kwa msururu wa vipimo ili kuhakikisha ikiwa mtoto wako ana tatizo la kujifunza

  • Mipango fulani ya shule inaweza kusaidia katika masomo ambayo mtoto wako ana changamoto nayo

Watoto hawapati matatizo ya kujifunza kwa sababu wao ni wavivu au wasio na nidhamu. Kuna kitu kwenye ubongo wao ambacho hakikukua ipasavyo. Madaktari hawajui kwa uhakika kwa nini hali hutokea, lakini matatizo ya kujifunza yanaweza kutokea zaidi ikiwa:

  • Mama alikuwa mgonjwa au alitumia dawa fulani haramu wakati wa ujauzito

  • Mama au mtoto alipata matatizo ya kiafya wakati wa ujauzito

  • Mtoto alikuwa na ugonjwa mbaya (kama vile saratani) katika umri mdogo

Matatizo ya kawaida ya kujifunza ni:

  • Matatizo ya kusoma, kama vile disleksia

  • Matatizo ya kuandika

  • Matatizo ya hisabati

Watoto ambao hawajifunzi katika kiwango kinacholingana na umri na uwezo wao wanapaswa kutathminiwa ili kubaini ikiwa wana matatizo ya kujifunza.

Je, dalili za matatizo ya kujifunza ni zipi?

Watoto wachanga walio na matatizo ya kujifunza wanaweza kuchukua muda mrefu kuliko kawaida kujifunza:

  • Majina ya rangi, herufi, au vitu

  • Jinsi ya kuhesabu

  • Jinsi ya kusoma na kuandika

Watoto wanaweza pia kuwa na:

  • Muda mfupi wa umakini

  • Kutoweza kumakinika

  • Matatizo ya lugha au kuzungumza

  • Matatizo ya kuelewa maelekezo

  • Matatizo ya kukumbuka mambo yaliyotokea hivi karibuni

  • Matatizo ya kutumia mikono na vidole, kama vile kuandika na kunakili

Baadhi ya watoto wenye matatizo ya kujifunza huonyesha kuchanganyikiwa shuleni. Kuchanganyikiwa kunaweza kusababisha matatizo ya kitabia, kama vile kufanya shughuli nyingi kupita kiasi, kuwa na haya, au kuwa mkali.

Watoto wenye disleksia, aina moja ya tatizo la kusoma, ambalo huwa na dalili kama vile:

  • Kuchelewa kuanza kuzungumza na kutaja herufi na picha

  • Matatizo ya kutamka sauti za maneno au kuweka sauti kwa mpangilio sahihi

  • Tatizo la kuona neno moja katika kikundi au sehemu za neno moja

  • Kuchelewa kuanza kusoma kwa sauti

  • Makosa mengi ya tahajia na kuandika kuliko kawaida, kama vile kugeuza herufi katika maneno

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana tatizo la kujifunza?

Madaktari watatathmini uwezo wa kusikia na wa kuona wa mtoto wako ili kuhakikisha kuwa hizo sio sababu za matatizo ya kujifunza ya mtoto wako (matatizo ya kusikia na kuona sio matatizo ya kujifunza).

Ili kuthibitisha kwa uhakika, watampeleka mtoto wako kwa mtaalamu wa kujifunza (mara nyingi katika shule ya mtoto). Mtaalamu huyo atafanya msururu wa tathmini za akili na kumuuliza mtoto wako maswali ya kusoma, kuandika na ya hisabati.

Je, matatizo ya kujifunza yanatibiwaje?

Matatizo ya kujifunza hutibiwa kupitia mipango ya elimu ambayo husaidia watoto wenye matatizo ya kujifunza. Kwa mfano, disleksia hutibiwa kwa mipango ambayo hufundisha watoto kutambua maneno kwa kuzingatia sauti. Mipango hii pia hutumia vitabu vya sauti, visoma skrini za kompyuta na zana zingine.

Baadhi ya watoto wenye matatizo ya kujifunza pia wana ADHD (tatizo la kukosa umakini kwa muda mrefu /tatizo la kukosa utulivu). Dawa ambazo madaktari wanaagiza kwa ajili ya ADHD huwasaidia watoto kuwa makini, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kujifunza vizuri zaidi.

Nchini Marekani, Sheria ya Elimu ya Watu Wenye Ulemavu (IDEA) inazitaka shule za umma kuwatathmini watoto kwa matatizo ya kujifunza. Pia inazitaka shule kutoa elimu bila malipo na inayofaa kwa watoto wenye matatizo ya kujifunza.