Je, ni yapi malengo ya matibabu ya saratani?
Lengo kuu la matibabu ya saratani ni kuondoa ugonjwa huo wa saratani. Matibabu haya yanaweza kufanywa kwa kutumia mbinu moja ya tiba (kama vile upasuaji) au mseto wa matibabu, kama vile upasuaji na tibakemikali (dawa zinazoharibu seli za saratani) na tiba ya mionzi.
Ikiwa haiwezekani kuondoa kansa yako, madaktari watajaribu kuipunguza, kukufanya upate nafuu zaidi, na kupunguza dalili zako ili upate afueni.
Kutibu saratani ni mchakato changamano, na madaktari na watoa huduma wengine wa afya hufanya kazi pamoja kama timu. Timu yako inaweza kujumusisha madaktari wa huduma za msingi, wataalamu, wapasuaji, wasaidizi wa madaktari, wataalamu wa tiba ya mionzi, wauguzi, wahudumu wa jamii, na wauzaji wa madawa.
Madaktari wako watachagua aina ya matibabu (iitwayo itifaki ya matibabu) inayofaa aina ya saratani unayougua.
Je, madaktari huchagua vipi matibabu yanayofaa kwa saratani yako?
Madaktari huamua matibabu yanayofaa zaidi kwa kansa yako kulingana na:
Uwezekano wa kupona (kansa yako kuisha na kutorudi tena)
Uwezekano wa kupata maisha marefu zaidi yenye afueni
Jinsi matibabu yatakavyopunguza dalili zako
Madhara ya matibabu
Matamanio yako ya matibabu
Zungumza na daktari wako kuhusu manufaa na changamoto za matibabu tofauti.
Itifaki za matibabu ni mbinu za kawaida zilizobainishwa na madaktari za kutibu aina fulani za saratani. Itifaki hizi zimejaribiwa kwa umakini katika tafiti ziitwazo majaribio ya kikliniki. Katika majaribio ya kikliniki, madaktari hulinganisha dawa na matibabu mapya na matibabu ya kawaida ili kusaidia kujua iwapo matibabu mapya yanafanya kazi vizuri zaidi. Watu wengi walio na saratani hupewa fursa ya kushiriki kwenye jaribio la kikliniki. Zungumza na daktari wako kuhusu manufaa na changamoto za kushiriki kwenye jaribio.
Je, madaktari hujuaje iwapo matibabu yanafanya kazi?
Madaktari watakagua ili waone iwapo matibabu unayopewa yanafaulu kupambana na saratani. Wakati wa matibabu yako, madaktari wanaweza:
Kufanya uchunguzi wa picha (kama vile uchanganuzi wa CT [tomografia ya computer]) ili kuona iwapo ukubwa wa uvimbe wako umepungua
Kufanya vipimo vya damu ili kuangalia viwango vyako vya antijeni za uvimbe (ziitwazo alama za uvimbe kwa aina fulani za saratani) kwenye damu yako
Iwapo matibabu ya kansa yako yatafaulu, huenda ukapata yafuatayo:
Kupungua—kansa yako kuisha kabisa
Afueni kidogo—uvimbe wako kupungua hadi chini ya nusu ya ukubwa wake wa awali, hali ambayo inaweza kupunguza dalili zako na kuongeza muda wako wa kuishi
Kurudia—kansa yako kuisha kabisa lakini irudi baadaye