Dalili za saratani

Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023

Kansa hukua kwenye mwili wako, inaweza kukuathiri kwa njia kadhaa. Kansa hiyo inaweza:

  • Kubana tishu iliyo karibu na kusababisha maumivu au kuzuia utendakazi muhimu wa sehemu ya mwili

  • Kutoa madutu yanayoweza kuhitilafiana na ogani zingine (hali iitwayo matatizo ya paraneoplastiki)

Kwa mfano, kupata uvimbe karibu na kibofu chako cha mkojo (ogani inayobeba mkojo) kunaweza kuzuia mkojo wako kutoka. Saratani iliyo ndani ya mifupa yako husababisha maumivu ya mifupa.

  • Mwanzoni, saratani haitasababisha dalili zozote kwa sababu ni kikundi kidogo tu cha seli

  • Kadiri kansa inavyokua, dalili zako zitategemea mahali ilipo

  • Baadhi ya kansa zinaweza kusababisha dalili kwenye sehemu za mwili wako ambazo haziko karibu na sehemu yako ya kansa

Dalili za saratani ni zipi?

Dalili hutofautiana kulingana na aina ya saratani. Baadhi ya kansa hazitaonyesha dalili hadi zitakapokuwa kubwa kabisa. Zingine huonyesha dalili katika hatua ya awali. Dalili za saratani zinaweza kujumuisha:

Maumivu

  • Kansa nyingi hazisababishi maumivu mwanzoni

  • Kadiri kansa yako inavyokua, unaweza kupata maumivu madogo

  • Kisha, maumivu huongezeka kadiri kansa inavyokuwa kubwa

  • Si aina zote za kansa husababisha maumivu makali

Kuvuja damu na damu iliyoganda

Saratani inaweza kusababisha kuvuja damu ndani ya mwili wako, kwa kutegemea mahali ilipo:

  • Saratani iliyo kwenye njia ya mmeng'enyo wa chakula inaweza kusababisha damu kuwepo kwenye kinyesi chako (haja kubwa)

  • Saratani iliyo kwenye njia ya mkojo inaweza kusababisha damu kuwepo kwenye kmkojo wako

  • Saratani iliyo kwenye mapafu yako inaweza kukufanya ukohoe damu

  • Saratani iliyo karibu na ateri kuu inaweza kusababisha shimo kwenye ateri ambalo litavuja damu nyingi mno

  • Saratani iliyo kwenye uboho (uwazi ulio ndani ya mifupa yako, ambapo seli za damu hutengenezewa) inaweza kuzuia mwili wako kuzalisha seli zinazofanya damu igande:

Kwenye saratani iliyoenea sana, kuvuja damu nyingi kunaweza kusababisha kifo

Aina nyingi za saratani huongeza hatari ya kuwa na damu iliyoganda kwenye mishipa ya miguu yako. Damu iliyoganda kwenye mishipa ya miguu wakati mwingine husafirishwa hadi kwenye mapafu na kuzuia mtiririko wa damu. Hali hii inaweza kusababisha ugumu wa kupumua na wakati mwingine kifo.

Kupoteza uzani na kuhisi udhaifu

  • Unaweza kupoteza uzani na kuwa mwembamba sana

  • Chakula kinaweza kukufanya uhisi kichefuchefu tumboni au unaweza kutatizika kumeza

  • Ikiwa una anemia, unaweza kuwa na uchovu na udhaifu sana kadiri saratani inavyokua

Dalili kwenye misuli na ubongo

Iwapo kansa imekua au imebana neva au uti wa mgongo wako, huenda ukapata:

  • Maumivu

  • Udhaifu

  • Mabadiliko katika hali yako ya kuhisi, kama vile kuwashwawashwa

Kansa ikianza au ikienea kwenye ubongo wako, huenda ukapata:

  • Kuchanganyikiwa

  • Kizunguzungu

  • Maumivu ya kichwa

  • Hisia ya kichefuchefu tumboni

  • Mabadiliko katika hali ya kuona

  • Vifafa

Dalili kwenye mapafu

Kansa ikibana au kuzuia njia za kupitisha hewa kwenye mapafu yako, unaweza kupata:

  • Kupumua kwa shida

  • Kikohozi

  • Nimonia (maambukizi ya mapafu)