Madaktari huchunguzaje ugonjwa wa saratani?
Madaktari wanaweza kuona kuwa una saratani kulingana na:
Dalili zako
Vipimo vya kimwili
Matokeo kutokana na vipimo vya uchunguzi wa saratani (vipimo vya kuangalia iwapo una saratani kabla hujapata dalili zozote)
Ili kuhakikisha, madaktari watafanya vipimo. Watatambua (kubainisha) saratani yako kwa kutumia matokeo ya vipimo.
Madaktari pia wataona hatua ya saratani yako (hatua ya I, hatua ya II, hatua ya III, au hatua ya IV). Hatua hufafanua ukubwa wa saratani yako na iwapo imeenea kwenye sehemu zingine za mwili wako.
Ni vipimo gani vinaweza kuchunguza iwapo una saratani?
Vipimo vya uchunguzi ni vile ambavyo daktari wako hufanya wakati huna dalili zozote. Daktari wako anaweza kupendekeza vipimo vya uchunguzi ikiwa uko katika hatari kubwa ya kupata saratani kulingana na umri, jinsia, historia ya familia, afya, au hali ya maisha.
Madaktari hutumia vipimo tofauti vya uchunguzi kwa ajili ya aina tofauti za saratani. Baadhi ya vipimo vya uchunguzi vinaweza kusaidia kuokoa maisha, lakini ni baadhi tu ya vipimo vya uchunguzi vinaweza kutegemewa.
Baadhi ya vipimo vya kawaida vya uchunguzi ni:
Kipimo cha Pap ili kubaini saratani ya mlango wa kizazi
Mamogramu (eksirei ya matiti) ili kubaini saratani ya matiti
Kipimo cha PSA (antijeni mahususi kwa tezi dume) ili kubaini saratani ya tezi dume
Vipimo vya kinyesi (haja kubwa) au kolonoskopia ili kubaini saratani ya utumbo mpana
Madaktari wanaweza kufanya vipimo vya uchunguzi:
Kama sehemu ya tathmini zako za kawaida za mwili
Wakati wa ziara ofisini
Kwenye utaratibu ambao ni lazima uratibiwe mapema
Hata kama matokeo ya kipimo ni mazuri, madaktari hawawezi kujua kwa uhakika iwapo una saratani. Madaktari watafanya vipimo mahususi zaidi ili kubaini iwapo una saratani.
Ni vipimo gani vinaweza kutambua ugonjwa wa saratani?
Madaktari wakishuku kuwa una saratani, huwa wanafanya kipimo cha kupiga picha sehemu za ndani ya mwili wako, kama vile eksirei, kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti, au uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au uchanganuzi wa MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku). Ili kuhakikisha kabisa, madaktari watafanya:
Uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi (kuchukua sampuli ya tishu zako) na kukiangalia chini ya hadubini
Vipimo vya kubaini hatua
Madaktari wakitambua kuwa una saratani, watafanya vipimo ili wagundue hatua iliyofikia. Hatua hiyo huwaambia mahali saratani ilipo na ukubwa wake. Pia, hatua hubainisha iwapo kansa imekua na kuenea kwenye sehemu nyingine za mwili. Kujua hatua ya ugonjwa huwasaidia madaktari kuamua matibabu yanayofaa zaidi. Vipimo vya kubaini hatua ni pamoja na:
Vipimo vya picha, kama vile eksirei, uchanganuzi wa CT na MRI, uchanganuzi wa mifupa na PET (tomografia ya kutoa positroni)—daktari wako atatumia baadhi ya vipimo hivi kulingana na aina ya saratani uiyo nayo
Uondoaji wa kipande cha tishu kwenye uvimbe au kwenye tishu zilizo karibu na uvimbe ili kifanyiwe uchunguzi
Vipimo vya damu ili kuona iwapo ini, mifupa na figo zako zinafanya kazi kwa njia ya kawaida