Ugonjwa wa saratani huanza vipi?
Saratani huanza seli nzuri inapobadilika. Hali hii inaweza kutokea:
Bila sababu yoyote inayofahamika
Kwa sababu uliathiriwa na kasinojeni
Kasinojeni ni kitu kinachoweza kusababisha kansa.
Baadhi ya kasinojeni ni pamoja na:
Miale ya jua (nje na ndani ya nyumba kwenye kitanda cha kubadilisha rangi ya ngozi)
Tumbaku
Kemikali fulani
Virusi fulani
Mionzi
Kwa kawaida, ni lazima uwe umeathiriwa na kasinojeni kwa muda mrefu kabla ya kupata kansa. Watu wengi wanaoathiriwa hawapati kansa.
Baadhi ya seli zina uwezekano mkubwa wa kupata saratani kuliko zingine. Seli hizi zinaweza kuwa na tatizo kwenye jeni zake. Jeni ni seti ya maagizo yaliyo ndani ya seli yanayozielekeza jinsi ya kufanya. Seli zilizo na hitilafu kwenye jeni zake zinapoathiriwa na kasinojeni, kuna uwezekano mkubwa kuwa zitageuka kuwa saratani. Hii ndiyo sababu kunaweza kuwa na aina fulani ya saratani inayotokea kwenye familia yenu.
Je, saratani huenea vipi?
Seli za saratani zinaweza kuenea:
Kwa kusambaa moja kwa moja kwenye tishu na ogani zilizopo karibu
Kwa kusafirishwa hadi ogani zingine kupitia mfumo wa limfu au mishipa ya damu
Mfumo wa limfu ni sehemu ya kinga za mwili wako. Ni mtandao wa tezi limfu na mishipa ya limfu inayobeba majimaji ya limfu mwilini. Majimaji ya limfu hubeba na kuondoa seli na vitu vilivyosalia wakati mwili wako unapambana na ugonjwa. Kinga za mwili wako hupigana na kuua seli za saratani pia, lakini wakati mwingine seli hai za saratani zinaweza kuingia kwenye majimaji ya limfu. Seli za saratani zinaweza kusafirishwa kwenye majimaji ya limfu au kwenye damu na kufikia ogani zingine. Wakati mwingine seli za kansa hufikia ogani zilizo mbali sana na sehemu halisi zilikoanza. Mahali kansa ilipoanza huitwa sehemu msingi ya saratani. Saratani iliyoenea kwenye ogani zingine huitwa kansa enezi.