Udhaifu ni nini?
Udhaifu ni hali ya kupoteza nguvu za misuli. Ukiwa na udhaifu, huwezi kusogeza musuli kwa njia ya kawaida, hata kama unajitahidi kwa kiasi gani. Udhaifu ni tofauti na uchovu (kuchoka), kuwa na misuli iliyokakamaa, au kutoweza kusogeza sehemu ya mwili wako kwa sababu ina maumivu mengi sana.
Udhaifu wa misuli unaweza kutokea ghafla au polepole kadiri muda unavyosonga
Unaweza kupata udhaifu kwenye mwili mzima au katika misuli fulani tu
Udhaifu unaweza kuwa hatari ikiwa unahusisha misuli inayodhibiti kupumua
Tiba ya mazoezi ya mwilil na ya kikazi inaweza kusaidia misuli yako kuwa thabiti zaidi kwa kutegemea kinachosababisha udhaifu
Je, napaswa kumwona daktari lini?
Nenda kwenye kitengo cha dharura mara moja ikiwa una udhaifu wa misuli na mojawapo ya ishara hizi za tahadhari:
Udhaifu unaoanza kwa kipindi cha siku chache au haraka zaidi
Kupumua kwa shida
Kushindwa kuinua kichwa chako ukiwa umelala
Matatizo ya kutafuna, kuzungumza au kumeza
Kushindwa kutembea
Mpigie simu daktari wako ikiwa una udhaifu wa misuli bila ishara za tahadhari ili daktari wako aamue wakati atakapokuona.
Ni nini husababisha udhaifu?
Udhaifu kwenye mwili mzima kwa kawaida una sababu tofauti na za udhaifu katika misuli fulani.
Ikiwa una udhaifu katika mwili mzima, sababu za kawaida ni:
Kudhoofika kwa siha ya mwili, hususan ikiwa una zaidi ya miaka 55
Kupoteza nguvu za misuli baada ya mapumziko ya kitandani
Matatizo ya neva kwenye mwili mzima zinazodhibiti misuli yako
Matatizo ya misuli yanayoweza kutokea kutokana na upungufu wa potasiamu, kutumia kotikosteroidi, au kunywa pombe kupita kiasi
Dawa fulani, kama vile dawa zinazotumiwa na madaktari wakati wa upasuaji ili kukuzuia kusogeza viungo
Ikiwa una udhaifu katika misuli fulani tu, sababu za kawaida ni:
Kiharusi (hususan iwapo udhaifu wako uko upande mmoja wa mwili)
Uharibifu wa neva kutokana na majeraha
Neva iliyobanwa, kama vile kutokana na ugonjwa wa carpal tunnel
Diski iliyopasuka kwenye uti wa mgongo
Shinikizo kwenye uti wa mgongo kutokana na ugonjwa mkali wa baridi yabisi, maambukizi, au saratani iliyoenea kwenye uti wako wa mgongo
Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?
Madaktari watakuuliza maswali kuhusu tatizo lako la udhaifu. Watafanya uchunguzi wa mwili ili kuangalia iwapo kuna matatizo ya ubongo, uti wa mgongo, neva, na misuli, na kuhakikisha kuwa unapumua vizuri.
Kwa kutegemea kile ambacho madaktari wanafikiria kuwa kinasababisha udhaifu wako, wanaweza kufanya vipimo (angalia Utambuzi wa ugonjwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo, na Matatizo ya Neva). Vipimo hivi vinaweza kujumuisha:
Uchunguzi wa MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) au uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) ili kuona picha za sehemu za ndani za mwili wako
Uchunguzi wa elektromayografia na uendesaji wa ishara za umeme wa neva ili kupima shughuli za kielektriki za neva na misuli yako
Wakati mwingine, kipimo cha kufyonza majimaji ya uti wa mgongo ili kutoa majimaji ya uti wa mgongo ya kufanyia vipimo
Uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi wa musuli au neva
Upimaji wa jenetiki ili kuona kama una tatizo linalotokea sana katika familia yako
Vipimo vya damu na mkojo
Madaktari hutibu vipi udhaifu?
Madaktari watatibu kisababishaji cha udhaifu wako wa misuli
Ikiwa unashindwa kupumua kutokana na udhaifu wa misuli inayohitajika kupumua, wanaweza kukuwekea mashine ya kupumua
Wanaweza kukushauri upate tiba ya mazoezi ya mwili ili kusaidia kuimarisha uthabiti wa misuli yako na tiba ya mazoezi ya kikazi ili kukusaidia kujifunza njia mpya za kufanya shughuli za kila siku