Ugonjwa wa Carpal Tunnel

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Ugonjwa wa carpal tunnel ni nini?

Ugonjwa wa carpal tunnel ni maumivu, kufa ganzi, na kuwashwa kwenye vidole na mkono. Hisia hizo husababishwa na shinikizo kwenye neva ya mkono wako.

  • Kijia cha kiganja ni nafasi (kijia) kwenye upande wa kiganja cha mkono wako

  • Neva za mediani inapita kwenye kijia cha kiganja

  • Shinikizo kwenye neva inaweza kusababisha ugonjwa wa carpal tunnel

  • Matibabu kwa kawaida huhusisha dawa za kutuliza maumivu za kumeza, kifaa cha kushikilia kiungo, dozi ya dawa inayoitwa kotikosteroidi, na wakati mwingine upasuaji.

Ni nini husababisha ugonjwa wa carpal tunnel?

Ugonjwa wa carpal tunnel hutokea wakati neva ya kati kwenye kifundo cha mkono wako inapobanwa kutokana na uvimbe au mikanda ya tishu ngumu ndani ya kijia cha kiganja. Kwa kawaida sababu haijulikani. Lakini baadhi ya vitendo vya kurudiarudia vinaweza kusababisha ugonjwa wa carpal tunnel, ikijumuisha:

  • Kazi inayokuhitaji kunyoosha mkono wako zaidi kwanamna ya kurudiarudia, kwa nguvu, kama vile kutumia nyundo.

  • Kutumia kibodi katika namna isiyo sahihi

  • Kutumia zana zinazotetemeka kwa muda mrefu (kwa mfano, zana fulani zinazotumia umeme)

Una uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa carpal tunnel ikiwa una hali fulani za kiafya, kama vile kisukari au ugonjwa wa baridi yabisi ya rumatoidi.

Dalili za ugonjwa wa carpal tunnel ni zipi?

Dalili zinaweza kutokea kwa mkono mmoja au yote miwili:

  • Ganzi, uchungu, kuwasha, na maumivu kwenye kidole gumba, kidole cha shahada, cha kati na sehemu ya vidole vyako vya pete.

  • Uchungu au maumivu makali na kufa ganzi na kuwashwa ambako mara nyingi hukuamsha usiku

  • Udhaifu na matatizo katika kushikilia vitu mkononi mwako

  • Baada ya muda mfupi, misuli ya kidole inaweza kudhoofika na kunywea

Madaktari wanawezaje kujua kama nina ugonjwa wa carpal tunnel?

  • Daktari atakagua dalili zako na kuchunguza mkono na kiganja chako

  • Daktari anaweza kufanya kipimo ambacho cha kupitisha kiwango kidogo cha umeme kwenye kiganjaa cha mkono wako ili kupima kasi na nguvu ya neva hutuma ishara kupitia neva (kipimo cha upitishaji wa neva)

Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa carpal tunnel?

Matibabu yanaweza kujumuisha:

  • Kuepuka kukunja mkono wako sana au kuweka shinikizo kwenye kiganja chako, kama vile kutumia kibodi vibaya.

  • Kuvaa vifaa vya kushikilia mkono ili kuweka mikono yako sawa, haswa unapolala au unapotumia kibodi au zana za mikono.

  • Kumeza dawa za kupunguza maumivu kama vile ibuprofeni au acetaminopheni

  • Kudungiwa dozi kwenye mkono (kijia cha kiganja) ya dawa inayoitwa kotikosteroidi, iwapo maumivu ni makali.

  • Kufanyiwa upasuaji, ikiwa maumivu yako ni makali sana au ikiwa misuli yako yananywea au kudhoofika

Ninawezaje kuzuia ugonjwa wa carpal tunnel?

Unapaswa kuepuka kukunja mkono wako sana au kuweka shinikizo zaidi kwenye neva.

Tumia kibodi kwa namna sahihi:

  • Weka mkono, kifundo cha mkono na kiganja chako kwenye mstari ulionyooka

  • Tumia pedi ya mkono ili kushikilia kifundo cha mkono wako, ikiwa inahitajika

Kuweka Kibodi kwa namna Sahihi

Kutumia kibodi ya kompyuta ambayo imewekwa vibaya inaweza kusababisha au kuchangia ugonjwa wa carpal tunnel. Ili kuzuia kuumia, mtumiaji anapaswa kuweka mkono ikiwa imetulia wakati wote. Yaani, mstari kutoka kwa mkono hadi kwenye kiganja unapaswa kunyooka. Mkono unaweza kuwa chini kidogo kuliko kiganja. Lakini mkono haupaswi kamwe kuwa juu zaidi, na kifundo cha mkono hakipaswi kukunjwa. Kibodi inapaswa kuwekwa chini, na mkono uwe chini kidogo kuliko kiwiko. Pedi ya mkono inaweza kutumika kushikilia kifundo cha mkono.