Je, ugonjwa wa ganglioni ni nini?
DKT P. MARAZZI/MAKTABA YA PICHA ZA KISAYANSI
Ganglioni (ama uvimbe wa ganglioni) ni uvimbe unaotokea kwenye mikono na vifundo vya mikono. Kwa kawaida ganglia hupatikana juu ya kiungo. Huwa yamejaa majimaji kama vile jeli na si zenye saratani.
Nini husababisha ugonjwa wa ganglioni?
Mara nyingi, madaktari hawajui sababu ya kutokea kwa ugonjwa wa ganglia. Unaweza kuhusishwa na jeraha la hapo awali. Wakati mwingine, ganglia nyuma ya kidole inahusiana na ugonjwa wa baridi yabisi katika kiungo cha kidole.
Dalili za ganglioni ni zipi?
Dalili iliyopo ya ganglia ni uvimbe kwenye kifundo cha mkono au kwenye mkono. Uvimbe huwa:
Mgumu, laini ukiguswa, na mviringo
Umejaa majimaji safi, yanayofanana na jeli
Kwa kawaida hauna maumivu, lakini baadhi ya watu hupata usumbufu mdogo
Ganglioni inaweza:
Kubadilika ukubwa
Kutokea polepole kwa muda au kujitokeza ghafla
Kutoweka bila matibabu na kurudi wakati mwingine
Madaktari wanawezaje kujua kama nina ugonjwa wa ganglioni?
Madaktari wanaweza kutambua ganglioni kwa kuchunguza mkono wako.
Madaktari hutibu ganglioni vipi?
Ganglioni mara nyingi hutoweka yenyewe bila matibabu.
Ikiwa ganglioni ina maumivu makali au inaendelea kukua, madaktari wanaweza kuondoa majimaji ndani yake kwa sindano (mpumuo). Wakati mwingine, madaktari hudunga dawa (inayoitwa kioevu cha kotikosteroidi) kwenye ganglioni ili kusaidia kupunguza maumivu.
Wakati mwingine, madaktari wanahitaji kuondoa ganglioni kwa upasuaji. Katika hali fulani, ganglioni hurudi baada ya kuondolewa.
Baadhi ya watu wanaamini kwamba ganglioni inaweza kuondolewa kwa kuipiga kwa kitu kigumu, kama vile kitabu. Haupaswi kufanya hivi, kwa sababu unaweza kuumiza mkono wako.