Kupoteza Kumbukumbu

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Kupoteza kumbukumbu ni nini?

Kupoteza kumbukumbu ni kukosa uwezo wa kukumbuka vitu vizuri kama ilivyokuwa awali.

Hali isiyokithiri ya kupoteza kumbukumbu inaweza kuwa sehemu ya kawaida ya kuzeeka. Kwa mfano, unaweza kusahau mahali ulipoweka funguo zako za gari. Tatizo la kupoteza kumbukumbu ambalo ni mbaya linaweza kuwa ishara ya tahadhari ya tatizo la utendaji wa ubongo, kama vile ugonjwa wa Alzheimer au ulegevu wa akili.

  • Wanafamilia wenzako wanaweza kugundua tatizo lako la kupoteza kumbukumbu kabla hujaligundua wewe mwenyewe

  • Ishara za tatizo mbaya la kupoteza kumbukumbu ni pamjoa na kusahau vitu vilivyofanyika hivi punde au matatizo ya kufanya shughuli ulizofanya mara nyingi hapo awali

  • Kutumia orodha, kalenda, na visaidizi vya kukumbuka kunaweza kukusaidia kukabiliana na tatizo la kupoteza kumbukumbu

Je, napaswa kumwona daktari lini kuhusiana na kupoteza kumbukumbu?

Mwone daktari wako ikiwa una tatizo la kupoteza kumbukumbu na dalili yoyote kati ya ishara hizi za tahadhari:

  • Matatizo ya kufanya shughuli za kila siku kama vile kudhibiti pesa au dawa zako

  • Matatizo ya kumakinika

  • Kuhisi mfadhaiko kutokana na kupoteza kumbukumbu

Mwone daktari mara moja ikiwa umepoteza kumbukumbu na:

  • Unashindwa kumakinika na unahisi kama umechanganyikiwa sana

  • Unahisi mfadhaiko na unafikiria kujidhuru

  • Una dalili za tatizo la mfumo wa neva kama vile maumivu ya kichwa, tatizo la kutumia au kuelewa lugha, kupungukiwa na motisha, matatizo ya macho, au kizunguzungu

Nini husababisha hali ya kupoteza kumbukumbu?

Sababu kuu za kupoteza kumbukumbu ni:

  • Kuzeeka—mabadiliko madogo ya kumbukumbu yanaweza kuwa tukio la kawaida unapozeeka

Sababu nyingine za kawaida:

  • Matatizo madogo ya kufikiria (kudhoofika kidogo kwa uwezo wa utambuzi)—takribani nusu ya watu walio na tatizo hili watapata dementia miaka kadhaa baadaye

  • Ulegevu wa akili (kama vile ugonjwa wa Alzheimer)

  • Mfadhaiko—ikiwa una mfadhaiko, inawezekana kuwa una dalili zingine pia, kama vile huzuni nyingi na matatizo ya kulala

  • Baadhi ya dawa

  • Kutumia dawa haramu au pombe kupita kiasi

Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?

Madaktari watafanya uchunguzi wa mwili na wakuulize maswali kuhusu hali yako ya kupoteza kumbukumbu, kama vile:

  • Aina ya mambo unayoyasahau

  • Wakati tatizo lako la kukumbuka lilianza

  • Iwapo unaona kama tatizo lako la kupoteza kumbukumbu linazidi

  • Ikiwa inazidi kuwa vigumu kufanya kazi yako au shughuli za kila siku

  • Ikiwa tatizo la kupoteza kumbukumbu linatokea sana katika familia yako

Madaktari wanaweza kupendekeza umlete mwanafamilia au rafiki kwenye miadi yako ambaye anaweza kufafanua dalili ambazo huenda hujazitambua au ambazo unatatizika kuzikumbuka.

Daktari anaweza kufanya vipimo kama vile:

  • Jaribio la hali ya kiakili—madaktari watakuuliza maswali na wakuelekeze kufanya majukumu mahususi ili kupima uwezo wako wa kufikiria, kama vile umakini, kumbukumbu na lugha

  • MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) au uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) iwapo madaktari watashuku kuwa una ulegevu wa akili au matatizo mengine kama vile uvimbe au kiharusi

  • Vipimo vya damu

  • Kipimo cha kufyonza majimaji ya uti wa mgongo (kutumia sindano ndefu kupata sampuli ya majimaji ya uti wa mgongo kutoka kwenye sehemu ya chini ya mgongo wako) ikiwa madaktari watashuku kuwa una maambukizi ya ubongo au uti wa mgongo

Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu?

Madaktari watafanya:

  • Kutibu tatizo lolote la afya linalosababisha kupoteza kumbukumbu

  • Wakati mwingine kukupatia dawa, iwapo una ulegevu w akili

  • Kukupima ili kuona iwapo unapaswa kuacha kufanya shughuli fulani, kama vile kuendesha gari

  • Kukupa mbinu na vidokezo, kama vile matumizi ya orodha na vikumbusho

Ninaweza kufanya nini ili kukabiliana na hali ya kupoteza kumbukumbu?

Ishi maisha bora kiafya:

  • Kula vyakula bora kwa afya, kama vile matunda na mboga

  • Fanya shughuli za mazoezi kila siku

  • Muone daktari wako kwa ukaguzi wa mara kwa mara

  • Shiriki katika shughuli za kimasomo, kijamii na kimwili

  • Pata usingizi wa kutosha kila usiku

  • Acha kuvuta sigara na kunywa pombe

  • Kuepuka mawazo

Tumia mikakati ya kukabiliana na hali ya kupoteza kumbukumbu:

  • Tengeneza orodha

  • Kuwa na kalenda yenye maelezo ya kina

  • Fuata ratiba maalum, kama vile kuingia kitandani wakati sawa kila usiku na kujiandaa kwa njia sawa kila asubuhi

  • Rudia taarifa mpya mara kadhaa

  • Angazia tu jambo moja kwa wakati mmoja

  • Jipange, kama vile kuweka funguo zako za gari mahali pamoja

  • Jiunge na shughuli za kijamii ili ujishirikishe na wengine na uendelee kufanyiza akili kazi