Homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na virusi

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2024

Homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na virusi ni nini?

Homa ya uti wa mgongo ni maambukizi ya tishu nyembamba inayofunika ubongo na uti wa mgongo wako. Safu hii ya tishu inajulikana kama utando. Katika ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo unaotokana na virusi, maambukizi husababishwa na virusi. Homa ya uti wa mgongo inayotokana na virusi si hatari kama homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na bakteria (homa ya uti wa mgongo iliyotokana na bakteria).

  • Homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na virusi huanza kwa homa, kujihisi mgonjwa, maumivu ya kichwa, na maumivu ya misuli

  • Baadaye, maumivu ya kichwa huzidi, na unaweza kupata shingo iliyokaza

  • Madaktari hushuku kuwa una homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na virusi kulingana na dalili ulizo nazo na matokeo ya kipimo cha kufyonza majimaji ya uti wa mgongo

  • Ikiwa una homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na VVU au virusi vya herpesi, utatibiwa kwa dawa za virusi hivyo, lakini hakuna dawa zinazoweza kutibu aina nyingi za homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na virusi

  • Watu wengi walio na homa ya uti wa mgongo iliyotokana na virusi hupata nafuu baada ya wiki chache

Nini husababisha homa ya uti wa mgongo inayotokana na virusi?

Aina nyingi za virusi zinaweza kusababisha homa ya uti wa mgongo, ikiwa ni pamoja na:

Unaweza kupata virusi vinavyosababisha homa ya uti wa mgongo kwa njia kadhaa, kwa kutegemea aina ya virusi vilivyosababisha:

  • Kugusa kinyesi (haja kubwa) kilichoathirika ambako kunaweza kufanyika watu wanapoogelea kwenye bwawa la kuogelea la umma au wanapokosa kunawa mikono baada ya kutoka msalani

  • Kujamiiana au kugusana sehemu za siri kwa njia nyingine na mtu aliyeambukizwa

  • Kuumwa na mdudu, kama vile mbu

  • Kupumua virusi vilivyo hewani

  • Kugusa vumbi au chakula kilicho na mkojo au kinyesi kutoka kwa panya au buku wa kufugwa walioambukizwa

  • Kutumia sindano kwa pamoja

Ni zipi dalili za homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na virusi?

Dalili zinaweza kufanana na zile za homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na bakteria lakini huwa kidogo na makali yake huongezeka polepole. Mwanzoni, huenda usiwe na dalili zozote au uwe na dalili zinazofanana na za mafua au virusi vya tumboni, kama vile:

  • Homa

  • Kikohozi

  • Maumivu ya misuli

  • Kutapika

  • Kutohisi njaa

Baadaye, utapata:

  • Homa

  • Maumivu ya kichwa

  • Shingo iliyokaza inayokuzuia kugusa kifua chako kwa kidevu au kusababisha maumivu unapojaribu kufanya hivyo—kusogeza kichwa chako kuelekea pande zingine huenda kusisababishe maumivu sana

Watu wengi, ila si wote, walio na homa ya uti wa mgongo iliyotokana na herpesi hupata pia vidonda vya herpesi kwenye sehemu zao za siri.

Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na virusi?

Madaktari hufanya vipimo vya kutafuta virusi kwenye majimaji yanayozunguka ubongo na uti wako wa mgongo (majimaji ya uti wa mgongo). Ili kupata umajimaji wa uti wa mgongo, madaktari:

Wakati wa kukinga majimaji ya uti wa mgongo, madaktari hudunga sindano ndefu, nyembamba kwenye sehemu ya chini ya mgongo wako. Wanavuta majimaji kidogo ya uti wa mgongo kwa ajili ya vipimo. Kabla ya kufyonza majimaji ya uti wa mgongo, madaktari wakati mwingine hufanya MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) au uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta).

Madaktari pia:

  • Watafanya vipimo vya damu ili kuangalia dalili za maambukizi ya virusi

Jinsi ya Kufanya Kinga Majimaji ya Uti wa Mgongo

Majimaji ya uti wa mgongo hutiririka kupitia mkondo katikati ya safu ya kati na ya ndani ya tishu (tando) zinazofunika ubongo na uti wa mgongo. Ili kutoa sampuli ya majimaji haya, daktari huingiza sindano ndogo, yenye mrija katikati ya mifupa miwili (vifupa vya uti wa mgongo) kwenye sehemu ya chini ya uti wa mgongo, chini ya mahali ambapo uti wa mgongo huishia. Kwa kawaida, anayefanyiwa vipimo hulalia upande na kukunja magoti kukaribia kifua. Mkao huu huongeza nafasi kati ya vifupa vya uti wa mgongo, ili daktari asiguse mifupa anapoingiza sindano.

Madaktari hukusanya majimaji ya uti wa mgongo kwenye mirija ya vipimo na kuyapeleka kwenye maabara kwa vipimo.

Madaktari hutibu vipi homa ya uti wa mgongo iliyosababishwa na virusi?

Madaktari hukupatia dawa za kupigana na virusi ikiwa ugonjwa wako wa homa ya uti wa mgongo umesababishwa na VVU au herpesi. Pia, watakupatia dawa za kutibu dalili zako, kama vile acetaminophen ya kutibu homa na maumivu ya kichwa.

Watu wengi wanaougua homa ya uti wa mgongo iliyotokana na virusi hawahitaji dawa za kupigana na virusi, kwa sababu watapata nafuu baada ya wiki chache iwe wamepata matibabu au la. Wakati mwingine, mchakato wa kupona hufanyika polepole, na inaweza kuchukua miezi kadhaa kupona.