Mfumo wa Uzazi wa Mwanamke

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Je, mfumo wa uzazi wa mwanamke ni nini?

Mfumo wa uzazi wa mwanamke ni mfumo kwenye mwili wa mwanamke wenye lengo la kuumba watoto. Mfumo wa uzazi wa mwanamke hujumuisha ogani za uzazi za nje (zilizo nje ya mwili) na ogani za uzazi za ndani (zilizo ndani ya mwili).

Ogani za uzazi za nje zinajumuisha:

  • Labia: Seti ya mikunjo miwili ya ngozi ambayo hufunika uwazi wa uke

  • Kisimi: Ogani ambapo labia hukutana ambapo hutoa hisia ya starehe wakati wa ngono

  • Uwazi kwenye uke

Sio viungo vyote vya uzazi vilivyo nje ni "uke" wako. Uke hasa ni njia ya uzazi tu.

Viungo vya uzazi vya ndani ni pamoja na:

  • Uke: Njia ya uzazi

  • uterasi (mfuko wa uzazi): Ogani ya ndani ambapo kijusi huota na kukua kabla ya kuzaliwa

  • Mlango wa kizazi: Upande wa mwisho wa uterasi, ambao ni mnene na wa mviringo, ambao una uwazi kwa ajili ya kupitisha damu ya hedhi na kwa ajili ya kujifungua mtoto

  • Ovari: Jozi ya ogani ambazo huunda mayai na homoni za kike kama vile estrojeni

  • Mirija ya uzazi: Miriji ambapo mayai hupita kutoka kwenye ovari kwenda kwenye uterasi

Anatomia ya Uzazi wa Mwanamke wa Nje

Anatomia ya Ndani ya Uzazi ya Mwanamke

Je, mfumo wa uzazi wa mwanamke hufanyeje kazi?

Kazi kuu ya mfumo wa uzazi wa mwanamke ni pamoja na:

  • Kubalehe: Kuandaa mwili wako kwa ajili ya kupata watoto

  • Mzunguko wa hedhi: Mzunguko wa mwezi wa uzalishaji wa mayai na kuvuja damu

  • Ujauzito: Kushika mimba na kukuza mtoto

Ovari za mtoto wa kike aliyezaliwa hivi karibuni huwa tayari zina mayai yote ambayo atakuwa nayo maishani. Lakini mayai haya hayawezi kugeuka kuwa watoto hadi pale mfumo wa uzazi wa mtoto wa kike upitie hatua za mabadiliko zinazoitwa Kubalehe. Wakati wa kubalehe:

  • Homoni (wajumbe wa kemikali) zinazoachiwa na ubongo husababisha ovari kukua

  • Ovari zinazokua huachia homoni ya ngono ya mwanamke estrojeni

  • Estrojeni husababisha mfumo wa uzazi wote kukua

Katika mzunguko wa hedhi wa kila mwezi:

  • Yai hukomaa na kutolewa (mchakato unaoitwa udondoshaji)

  • Utando wa uterasi huvimba na mishipa ya damu hivyo huwa tayari kupokea yai iwapo litarutubishwa kwa shahawa za mwanaume

  • Yai lililotungishwa hujipachika kwenye utando wa uterasi na kuanza kukua AU

  • Yai lisipotungishwa, halijipachiki, nao utando wa uterasi hubambuka na kutolewa kama damu ya hedhi.

Iwapo mwanamke hatapata mimba, mzunguko wa hedhi hujirudia karibu mara moja kwa mwezi. Wanawake hupata mzunguko wa hedhi hadi wakiwa na umri wa kati. Ukomo wa hedhi ni wakati mzunguko unapoacha.

Utungaji mimba ni pale ambapo shahawa ya mwanaume inapoungana (rutubisha) yai la mwanamke. Mara nyingi urutubishaji hufanyika kwenye mirija ya uzazi.

  • Yai lililorutubishwa husafiri hadi chini ya mrija wa uzazi na kuingia kwenye uterasi

  • Yai lililorutubishwa hujipachika kwenye ukuta wa uterasi na kuanza kukua

  • Hukua na kuwa kijusi na kondo la nyuma—kondo la nyuma ndilo huunganisha kijusi kwenye uterasi

Mfumo wa uzazi hudhibitiwa na homoni. Homoni ni visafirishaji vya kemikali ambavyo hutengenezwa katika sehemu fulani za mwili na husafiri kupitia damu kuelekeza sehemu nyingine za mwili kuhusu cha kufanya.

Baadhi ya homoni hutoka kwenye tezi ya pituitari kwenye ubongo. Homoni za uzazi kutoka kwenye tezi ya pituitari hupanda na kushuka kila mwezi na kuchochea mzunguko wa hedhi. Ikiwa utapata mimba, ogani zako za uzazi huzalisha homoni zingine ambazo huzima mzunguko wako wa hedhi na kutoa ishara kwa uterasi kukua na kumwezesha mtoto. Baada ya kujifungua, homoni nyingine hutoa ishara kwa matiti kutengeneza maziwa ya kumlisha mtoto wako.

Je, matatizo gani yanaweza kuukumba mfumo wa uzazi wa mwanamke?

Matatizo ya kawaida ya mfumo wa uzazi huhusisha homoni. Mfumo wa uzazi wa mwanamke hujumuisha homoni mbalimbali ambazo hufanya kazi kwa pamoja katika njia ambazo ni tata. Matatizo mengi mbalimbali yanaweza kuingilia homoni, ambapo inaweza kusababisha:

  • Kuchelewa kubalehe

  • Kubalehe mapema

  • Vipindi vya hedhi vinavyobadilika badilika

  • Kukosa hedhi

  • Kushindwa kupata ujauzito

  • Tatizo la kukaa na mimba

Magonjwa mengi, kama vile maambukizi na saratani, yanaweza kuathiri ogani za uzazi.