Mafua (Homa ya mafua)

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Je, homa ya mafua ni nini?

Homa ya mafua, mara nyingi huitwa mafua, ni maambukizi ya virusi ambayo huathiri mapafu na njia za hewa. Dalili za homa ya mafua zinafanana kwa kiasi fulani na zile za mafua ya kawaida lakini huwa kali zaidi.

  • Homa ya mafua husambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine hivyo kusababisha ugonjwa wa mlipuko (pale ambapo watu wengi huumwa kwa kipindi kifupi)

  • Homa ya mafua husababisha mzizimo, maumivu ya kichwa, vidonda kwenye koo, na kokohozi

  • Watu wengi hupona, lakini homa ya mafua huwafanya baadhi ya watu waumwe sana na watu wengine hufa kutokana na nimonia, maambukizi makali ya mapafu.

  • Madaktari watakufanya upumzike, unywe kiasi kikubwa cha majimaji, na utumie dawa kwa ajili ya kutuliza dalili zako iwapo itahitajika—wakati mwingine watakufanya utumie dawa za kuzuia virusi

  • Watu wenye umri wa miezi 6 au zaidi wanapaswa kupata chanjo ya homa ya mafua kila mwaka ili kusaidia kuzuia homa ya mafua.

  • Chanjo ya homa ya mafua ni njia bora kabisa ya kuzuia homa ya mafua, lakini unahitaji kupata chanjo kila mwaka—kirusi cha homa ya mafua hubadilika kila mwaka, hivyo sindano ya chanjo ya mwaka jana bila shaka haiwezi kuzuia homa ya mafua ya mwaka huu

Je, nini husababisha homa ya mafua?

Virusi huenea:

  • Kupitia hewa, matone ambayo mtu mwenye maambukizi husambaza kupitia kukohoa au kupiga chafya

  • Kupitia kugusa vitu ambavyo mtu mwenye maambukizi amevigusa baada ya kufuta au kupenga pua zake

Majira ya homa ya mafua nchini Marekani hudumu kuanzia Novemba hadi Machi. Kila mwaka, mamilioni ya watu hupata mafua na maelfu hufa.

Kirusi cha homa ya mafua hubadilika kwa kiasi kidogo kila mwaka. Mabadiliko haya husababisha matatizo:

  • Baadhi ya mabadiliko hufanya kirusi kiwe hatari zaidi

  • Chanjo mpya zinapaswa kutengenezwa kila mwaka

Wakati mwingine mabadiliko ya kirusi cha homa ya mafua hukifanya kiwe na uwezekano zaidi wa kusambaa na kuwa hatari zaidi. Hili hutokea mara chache katika kipindi cha miaka mia moja na kusababisha mlipuko wa homa ya mafua duniani kote. Mlipuko huu huua mamilioni ya watu duniani kote. Kwa bahati nzuri, kwa sababu virusi huendelea kubadilika, homa hii hatari zaidi hatimaye hubadilika na kuwa hatari kiasi.

Je, dalili za homa ya mafua ni zipi?

Dalili za mapema za homa ya mafua ni pamoja na:

  • Baridi

  • Homa, hadi takribani 103° F (39.4° C)

  • Kuumwa, udhaifu, na kuhisi uchovu

  • Maumivu ya misuli, hasa kwenye mgongo na miguu yako.

  • Maumivu makali ya kichwa

  • Pua zinazotoa kamasi

  • Koo lenye michubuko na vindoda

Dalili za baadaye zinajumuisha:

  • Kihozi kikali ambacho husababisha makohozi (makamasi)

  • Kuhisi mgonjwa tumboni na kutapika

Dalili nyingi hutoweka ndani ya wiki moja, lakini kikohozi kinaweza kudumu kwa wiki kadhaa.

Watoto, wanawake wajawazito, wazee, watu wenye magonjwa mengine kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo na ugonjwa wa mapafu, na watu ambao wana mfumo dhaifu wa kingamwili wanaweza kuwa na dalili kali zaidi. Pia wanaweza kupata nimonia.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina homa ya mafua?

Kwa kawaida madaktari wanaweza kufahamu kuwa una homa ya mafua kutokana na dalili ulizonazo, hasa ikiwa watu wengi katika eneo lako wana ugonjwa wa homa ya mafua. Ili kuthibitisha, daktari anaweza kukupima damu au majimaji puani au kwenye koo kubaini ikiwa una virusi vya mafua.

Iwapo madaktari wanadhani kuwa una nimonia, watafanya:

  • Eksirei ya kifua

  • Kipimo cha kiwango cha oksijeni, kipimo kinachotumia kitambuzi kilichowekwa kwenye ncha ya kidole chako ili kujua kiwango cha oksijeni kilichopo kwenye damu yako

Je, madaktari hutibu vipi homa ya mafua?

Madaktari watafanya:

  • Watakwambia upumzike sana na unywe kiasi kikubwa cha majimaji, hasa mpaka pale homa itakapopona.

  • Watakwambia utumie dawa fulani ili zikusaidie kupata ahueni, kama vile acetaminopheni au ibuprofeni kwa ajili ya maumivu ya misuli na homa, au dawa za kufungua pua kwa ajili ya pua zilizoziba

  • Wakati mwingine, watakupatia dawa za kuzuia virusi, iwapo umepata dalili kwa siku 1 au 2 tu

Je, ninawezaje kuzuia homa ya mafua?

Chukua hatua hizi:

  • Choma chanjo ya homa ya mafua

  • Nawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji au kitakatisha mikono

  • Jiepushe na mikusanyiko ya watu wakati wa msimu wa homa ya mafua

  • Funika pua na mdomo wako wakati unapokohoa au kupiga chafya (iwapo una homa ya mafua)

Karibu kila mtu mwenye umri wa miezi 6 au zaidi anapaswa kuchoma sindano ya homa ya mafua (chanjo) kila mwaka ili kusaidia kuzuia homa ya mafua. Zungumza na daktari wako kuhusu kuchoma sindano ya kuzuia homa ya mafua.

  • Huchukua wiki 2 kwa chanjo ya homa ya mafua kufanya kazi, hivyo madaktari nchini Marekani wanashauri kupata chanjo Oktoba, kabla ya kuanza kwa msimu wa homa ya mafua

  • Ikiwa chanjo ya homa ya mafua si salama kwako, madaktari wanaweza kukupatia dawa za kuzuia maambukizi ya homa ya mafua ikiwa kuna mlipuko mwingine wa homa ya mafua katika eneo lako

Wakati mwingine bado utapata homa ya mafua hata baada ya kuchoma chanjo ya homa ya mafua. Hata hivyo, chanjo hupunguza uwezekano wako wa kupata homa ya mafua. Pia, watu wengi ambao wanafikiri kuwa walipata homa ya mafua baada ya kuchonda chanjo huwa walipata mafua makali na sio homa ya mafua.