Je, mafua ya kawaida ni nini?
Mafua ya kawaida ni maambukizi ya virusi. Ni ugonjwa wa kawaida zaidi ambao huwapata watu wengi.
Mafua husambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, hasa ndani ya siku 2 za mwanzo za dalili
Dalili hujumuisha pua zilizoziba au zinazotoa kamasi, vidonda kwenye koo, uchovu, na wakati mwingine homa kiasi na dalili hizi huondoka zenyewe ndani ya siku 4 hadi 10
Kukaa kwenye baridi au kulowa maji hakusababishi mafua au kukufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kuumwa
Kuwa na kamasi za kijani au njano ni hali ya kawaida katika hatua za baadaye za mafua—haimaanishi kuwa unahitaji dawa za kuua bakteria au una maambukizi makali zaidi
Dawa za kufungua pua na antihistamini zinaweza kusaidia kuleta nafuu ya dalili za mafua, lakini usiwape watoto wenye umri chini ya miaka 4 dawa hizi
Kwa sababu mafua husababishwa na virusi, dawa za kuua bakteria haziwezi kuponya mafua au kuyafanya yapotee kwa haraka
Je, nini husababisha mafua?
Mafua husababishwa na virusi vingi tofauti. Kikundi cha virusi vinavyoitwa virusi vya pua ndio chanzo kikuu. Virusi vya pua huwa na tabia ya kusababisha mafua katika majira ya kuchipua na majira ya majani kupukutika.
Unaweza kupata mafua kwa:
Kugusa mkono wa mtu mwenye maambukizi baada ya mtu huyo kujifuta au kupenga pua zake
Kugusa kitu ambacho mtu mwenye maambukizi alikigusa
Kupangusa pua za mtoto mwenye maambukizi
Kuvuta hewa yenye virusi baada ya mtu mwenye maambukizi kukohoa au kupiga chafya
Je, dalili za mafua ni zipi?
Mwanzo, unakuwa na:
Koo lililochubuka au lenye vidonda
Pua zinazotoa makamasi mepesi, meupe (majimaji)
Wakati mwingine, homa kiasi
Baadaye, unapata:
Pua zilizoziba au pua zinazotoa makamasi mazito yenye rangi ya njano au kijani
Kuhisi uchovu na kuumwa
Kikohozi, ambacho kinaweza kudumu hadi wiki 2
Nenda kwa daktari mara moja ikiwa una homa kali, maumivu makali ya kichwa, upele, shida ya kupumua, au maumivu ya kifua. Una uwezekano wa kuwa na maambukizi makali zaidi ya mafua.
Mafua yanaweza kusababisha shambulizi la pumu kwa watu wenye pumu. Pia mafua yanaweza kusababisha maambukizi ya sikio au sanasi.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina mafua?
Kwa kawaida madaktari wanaweza kufahamu kuwa una mafua kutegemea na dalili zako.
Je, mafua huwa yanatibiwaje?
Huenda daktari akakueleza:
Pumzika nyumbani
Kunywa vinywaji kwa wingi
Tumia kifaa cha kuongeza unyevunyevu au kivukisho usiku ili uweze kulala vizuri zaidi
Pia madaktari wanaweza kukushauri utumie dawa za kununua kwenye duka la dawa ili zikusaidie kupata nafuu wakati ukisubiri mafua yako yapone:
Acetaminophen au ibuprofeni inaweza kupunguza maumivu yanayotokana na koo lenye vidonda au misuli inayouma na pia kushusha homa
Dawa za kufungua pua zinaweza kufungua pua zilizoziba
Antihistamini zinaweza kukausha pua zinazotoa makamasi au kuzuia kupiga chafya
Dawa fulani za kikohozi zinaweza kulainisha makamasi ili kufanya iwe rahisi kukohoa au kukuepusha na kukohoa
Kusukutua kwa maji ya chumvi kunaweza kusaidia kupunguza maumivu ya koo lenye vidonda
Unaweza kupata hizi dawa 2 au zaidi katika bidhaa moja, kama vile dawa ya kikohozi na mafua. Zungumza na daktari au famasia wako iwapo una maswali kuhusu dawa za mafua.
Dawa za kufungua pua au antihistamini zinaweza kusababisha athari za kando kwa watoto wadogo. Hazipaswi kutumika kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 4. Watoto wadogo wanaweza kupatiwa matone ya maji ya chumvi kwenye pua na yananaweza kusaidia kufungua pua zilizoziba.
Dawa zilizopo za kuua bakteria na kuzuia maambukizi ya virusi hazifanyi kazi dhidi ya mafua.
Je, ninawezaje kuzuia mafua?
Kunawa mikono yako mara kwa mara kwa sabuni na maji ndio njia bora ya kujiepusha na mafua.
Ikiwa una mafua, fuata hatua za kuwaepusha wengine wasipate mafua:
Piga chafya au kohoa kwenye karatasi ya shashi na weka karatasi ya shashi iliyotumika kwenye taka
Nawa mikono yako au tumia kitakasa mikono baada ya kugusa karatasi ya shashi iliyotumika hata kama ni yako mwenyewe.
Safisha vitu vya ndani ya nyumba, kama vile vifaa vya kuchezea na vitasa vya milango, kwa kutumia kipukusi (kiowevu ambacho huua viini vya maradhi)
Baki nyumbani pasipo kwenda kazini au shule hadi dalili zako zitakapoanza kupotea—unaweza kutakiwa kulala katika chumba tofauti na wanafamilia wenye afya