Maambukizi ya Virusi vya Ebola na Marburg

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2024

Maambukizi ya virusi vya Ebola na Marburg ni nini?

Ebola na Marburg ni maambukizi ya nadra ya virusi ambayo yanasababisha homa na kuvuja damu. Virusi hivi kwa kawaida huambukiza wanyama, si watu. Zinapoathiri watu zinaweza kuwa hatari.

  • Virusi huathiri watu kwa sana katika Afrika Magharibi na Kati

  • Wasafiri wachache (ikijumuisha wafanyakazi wa huduma ya afy) kutoka sehemu zingine za dunia wamerudi nyumbani kutoka Afrika wakiwa na maambukizi ya virusi vya Ebola

  • Virusi vya Marburg na Ebola huenea kwa urahisi zaidi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine—unaweza kupata virusi kutoka kwa mtu mgonjwa au mtu aliyefariki

  • Unaweza kupata virusi hivyo kwa kugusa ngozi au viowevu vya mwili vya mtu aliyeambukizwa

  • Dalili zinajumuisha homa, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa na baadaye kuhara sana na kuvuja damu chini ya ngozi yako

  • Kupona huchukua muda mrefu kwa sababu virusi hivyo vinaweza kusalia kwenye mwili kwa wiki

Ni nini husababisha maambukizi ya virusi vya Ebola na Marburg?

Virusi vya Marburg na Ebola kwa kawaida huathiri wanyama wanaoishi Afrika Magharibi na Kati. Lakini pindi zinapoambukiza watu, vinaweza kuenea haraka zaidi. Watu wanaweza kuambukizwa kwa:

  • Kugusa au kula wanyama walioambukizwa

  • Kugusa watu walioambukizwa

  • Kugusa miili ya watu waliofariki kutokana na maambukizi

Virusi vipo kwa karibu viowevu vyote vya mwili kutoka kwa watu na wanyama walioambukizwa. Hivi vinajumuisha damu, mate, kuhara, mkojo, kinyesi, jasho, maziwa ya matiti na shahawa. Unaweza pia kupata virusi kwa kugusa vitu ambavyo viligusa yoyote ya viowevu hivi, kama vile mavazi au vifaa vya kulalia vilivyopata viowevu. Hio inamaanisha kuwa uko kwenye hatari kubwa ikiwa wewe ni:

  • Mfanyakazi wa huduma ya afya

  • Mwanafamilia wa mtu aliyeambukizwa

  • Mtu ambaye anagusa miili ya waliofariki wakati wa matayarisho na hafla za mazishi

Je, dalili za virusi vya Ebola na Marburg ni zipi?

Kwanza, una dalili zinazojumuisha:

  • Homa, maumivu ya misuli na kuumwa na kichwa

  • Maumivu kooni

Ndani ya siku chache, unakuwa mgonjwa zaidi na unaweza kuwa na:

  • Maumivu ya tumbo, kutapika kupita kiasi na kuhara, wakati mwingine ikiwa na damu—hii inaweza kusababisha kukosa maji mwilini (kuwa na maji kidogo kwenye mwili wako)

  • Kuvuja damu chini ya ngozi yako (madoa au viraka vienye rangi ya zambarau), kutoka kwenye mdomo au mapua yako au kutoka kwenye viungo ndani ya mwili wako

  • Upele kwenye kifua au tumbo yako

  • Kuchanganyikiwa

  • Kupoteza fahamu (kukosa fahamu na kutoweza kuamka)

Katika wiki ya pili ya ugonjwa, aidha watu huanza kuhisi vizuri au kufariki mapema kwa sababu viungo vyao vinaacha kufanya kazi. Watu wana uwezekano mkubwa zaidi wa kufariki kutokana na virusi Ebola kuliko Marburg.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina virusi Ebola au Marburg?

Madaktari wanashuku virusi vya Ebola au Marbug ikiwa wewe ni mgonjwa na uko kwenye au hivi karibuni umetembea kwenye eneo ambapo watu wameambukizwa. Unachopaswa kutarajia:

  • Vipimo vya damu

Madaktari hutibu vipi virusi vya Ebola na Marburg?

Madaktari hawana dawa ya virusi ambayo inatibu virusi vya Ebola au Marburg. Dawa za kufanyiwa majaribio zinaendelezwa na watafiti. Madaktari hutibu maambukizi kwa:

  • Kupatiana viowevu vya IV (kwenye mshipa wako) ili kusaidia kuzuia kukosa maji mwilini

  • Kusaidia kupunguza kasi au kusitisha kuvuja damu

  • Kutibu dalili kama maumivu

Madaktari watavalia mavazi ya kujikinga na kwa umakini kukutenga ili kuzuia kueneza maambukizi kwa wengine.

Ni nini huzuia maambukizi ya virusi vya Ebola na Marburg?

Chanjo kadhaa na dawa za kuua virusi zinaendelezwa. Chanjo ya Ebola iliidhinishwa na Usimamizi wa Dawa na Vyakula wa Marekani wa 2019.

Katika sehemu za dunia ambazo zina virusi vya Ebola na Marburg, unapaswa:

  • Kuepuka kugusana na wanyama wa mwituni, haswa popo na tumbili

  • Kutokula nyama ya wanyama hawa (isipokuwa wakipikwa vizuri kabisa)

Ikiwa uko kwenye eneo ambalo kuna mlipuko wa virusi vya Ebola au Marburg:

  • Osha mikono yako mara nyingi kwa sabuni na maji au kisafishaji cha mkono ambacho kina pombe ndani yake

  • Usiguse watu wagonjwa isipokuwa kama unavalia vifaa vya kujikinga, vikijumuisha glovu, gauni na barakoa

  • Usiguse mwili wa mtu aliyefariki

Ikiwa hivi karibuni ulisafiri kwa mojawapo ya maeneo haya, tilia makini afya yako kwa siku 21 na uone daktari mara moja ikiwa dalili zozote zinatokea.