Ugonjwa wa Sturge-Weber

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Je, ugonjwa wa Sturge-Weber ni nini?

Ugonjwa wa Sturge-Weber ni kasoro ya kuzaliwa ya mishipa midogo ya damu.

  • Ugonjwa wa Sturge-Weber husababisha alama ya kuzaliwa kwenye uso wa mtoto aliyezaliwa karibuni

  • Pia watoto wengi hupata uvimbe kwenye mshipa wa damu (angioma) kwenye tishu inayofunika ubongo

  • Baada ya muda kupita, kwa kawaida watoto hupata matatizo ya macho na ubongo yanayozidi kuwa mbaya

  • Matibabu yanaweza kuboresha mwonekano wa alama ya kuzaliwa, na dawa zinaweza kusaidia matatizo ya macho na ubongo

Je, nini husababisha ugonjwa wa Sturge-Weber?

Ugonjwa wa Sturge-Weber husababishwa na jeni isiyo ya kawaida. Jeni hii iliharibiwa kwa bahati mbaya wakati bado mtoto akiwa kwenye mfuko wa uzazi. Jeni yenye kasoro hairithiwi kutoka kwa wazazi.

Mishipa ya damu yenye kasoro inayoota usoni husababisha alama yenye rangi ya zambarau au nyekundu. Mishipa ya damu yenye kasoro ambayo hukua kuzunguka ubongo inaweza kusababisha uharibifu kwenye ubongo au kiharusi.

Je, dalili za ugonjwa wa Sturge-Weber ni zipi?

Watoto huwa na alama ya kuzaliwa usoni. Kwa kawaida, alama ya kuzaliwa iko upande mmoja wa paji la uso na kope ya juu lakini inaweza kutokea kwenye sehemu yoyote usoni. Wakati mwingine huitwa doa la mvinyo kwa sababu rangi yake huanzia kwenye waridi isiyo kolea hadi kuwa zambarau iliyokolea.

Mbali na alama ya kuzaliwa, tatizo linaweza kusababisha:

  • Vifafa

  • Udhaifu kwenye upande mmoja wa mwili

  • Ugumu wa kuona

  • Ugumu wa kujifunza na kufikiri

  • Ongezeko la shinikizo kwenye jicho (glaukoma) na wakati mwingine jicho kuvimba kwa nje

  • Kuongezeka kwa uwezekano wa kupata kiharusi utotoni

Port-Wine Stain on the Face
Ficha Maelezo
This photo shows an infant with a port-wine stain on the face.
© Springer Science+Business Media

Je, madaktari watajuaje ikiwa mtoto wangu ana ugonjwa wa Sturge-Weber?

Madaktari hushuku uwepo wa ugonjwa wa Sturge-Weber kwa watoto wenye alama ya kuzaliwa ya kawaida.

Madaktari wanaweza kuagiza kipimo cha MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) ya ubongo (uchanganuzi unaonyesha picha zenye kuonyesha kila kitu) ili kukagua uwepo wa uvimbe kwenye mishipa ya damu kwenye tishu zinazofunika ubongo.

Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa Sturge-Weber?

Hakuna tiba ya ugonjwa wa Sturge-Weber. Madaktari hutibu dalili kwa:

  • Dawa au upasuaji wa kudhibiti mishtuko

  • Dawa au upasuaji wa glaukoma

  • Dozi ndogo za aspirini ili kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi

  • Matibabu ya leza ili kupunguza au kuondoa alama ya kuzaliwa iwapo itatakiwa kufanya hivyo