Nyurofibromatosisi

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Je, nyurofibromatosisi ni nini?

Katika nyurofibromatosisi, vinyama vidogo vingi vya tishu za neva (zinazoitwa nyurofibroma) hutokea juu au chini ya ngozi kwa maneno mengine kwenye sehemu zingine za mwili. Kuna aina kadhaa za nyurofibromatosisi. Baadhi ya aina hugundulika kwa watoto wachanga na aina zingine huwapata sana watu wazima.

  • Nyurofibroma kwenye ngozi zinaweza kuathiri mwonekano wako

  • Wakati mwingine Nyurofibroma husababisha dalili kwa kukandamiza neva

  • Nyurofibroma nyingi hazina saratani lakini baadhi ni zenye saratani

  • Madaktari wanaweza kuona na kuhisi nyurofibroma kwenye ngozi

  • Madaktari hufanya CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) kwenye ubongo na mwili ili kutafuta nyurofibroma zingine

  • Hakuna tiba, lakini wakati mwingine madaktari hufanya upasuaji au kutumia leza kuondoa baadhi ya nyurofibroma

  • Madaktari hutumia tibakemikali kwa nyurofibroma ambazo ni zenye saratani.

Je, nini husababisha nyurofibromatosisi?

Nyurofibromatosisi husababishwa na jeni zisizo za kawaida. Aina mbalimbali za nyurofibromatosisi husababishwa na aina mbalimbali za jeni zisizo za kawaida. Wakati mwingine mtoto hurithi jeni isiyo ya kawaida kutoka kwa mzazi. Wakati mwingine, mtoto ndiye mtu wa kwanza katika familia kuwa na jeni isiyo ya kawaida.

Je, dalili za nyurofibromatosisi ni zipi?

Dalili hutegemea na sehemu zilipo nyurofibroma.

Dalili za ngozi:

  • Madoa kwenye ngozi yanayofanana na mabakabaka makubwa yenye rangi ya kahawa ya maziwa (madoa ya "cafe-au-lait")

  • Viuvimbe au mabonge madogo kwenye ngozi (baadhi ya watu wanayo machache, lakini baadhi wanayo maelfu)

Dalili za neva au uti wa mgongo:

  • Kuwashwa

  • Maumivu

  • Udhaifu wa misuli

Dalili za neva zinaweza kutokea pale vinyama vinapokandamiza neva kwenye mikono au miguu.

Dalili za ubongo:

  • Upofu

  • Kizunguzungu

  • Udhaifu

  • Kusogea kwa kushtuka na pasipo uthabiti

  • Kupoteza uwezo wa kusikia

  • Mlio katika masikio

  • Maumivu ya kichwa

Mara chache, vinyama vinaweza kusababisha matatizo katika muundo wa fuvu na mgongo na mifupa ya ubavu, mkono na mguu. Iwapo mfupa unaozunguka mboni ya macho utaathiriwa, macho yanaweza kuchomoza nje.

Je, madaktari watajuaje ikiwa mtoto wangu ana nyurofibromatosisi?

Watu wengi huwa hawaoni tatizo lolote kwa watoto wao. Badala yake, daktari huwa anaona mabakabaka makubwa yenye rangi ya kahawa ya maziwa au viuvimbe chini ya ngozi ya mtoto wako wakati wa uchunguzi wa kawaida. Wanaaweza kukuuliza ikiwa wanafamilia wengine wana dalili sawa na hizo.

Daktari wa mtoto wako atachunguza vinyama na madoa. Madaktari wanaweza kufanya uchanganuzi wa CT au MRI (vipimo vinavyoonyesha picha zenye kila kitu mwilini mwako) ili kutafuta uwepo wa vinyama ndani na eneo linalozunguka ubongo na uti wa mgongo wa mtoto wako.

Je, madaktari hutibu vipi nyurofibromatosisi?

Hakuna tiba ya nyurofibromatosisi.

Vinyama vinaweza kuondolewa kwa upasuaji au matibabu ya leza, lakini vinaweza kuota tena. Madaktari hutumia tibakemikali kwa vinyama vyenye saratani.

Je, ninawezaje kuzuia nyurofibromatosisi?

Ikiwa kuna wanafamilia wenye nyurofibromatosisi na unapanga kupata watoto, unaweza kufanya vipimo vya jeni. Vipimo hivi vitakueleza kama unaweza kubeba jeni hiyo. Ikiwa hivyo, ushauri nasaha kuhusu jeni unaweza kukusaidia kuona uwezekano ulionao wa kurithisha (au kutorithisha) jeni hiyo kwa watoto wako.