Kuvuja Damu Ndani ya Ubongo

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Ni nini maana ya kuvuja damu ndani ya ubongo?

Kuvuja damu ndani ya ubongo ni kutokwa na damu kwenye ubongo. Ni dharura ya matibabu ambayo mara nyingi husababisha uharibifu wa ubongo wa kudumu au kifo.

  • Hali ya kuvuja damu kwenye ubongo hufanyika wakati mshipa wa damu umepasuka

  • Kisababishi cha kawaida ni Shinikizo la damu kuwa juu

  • Kunaweza kusababishwa na jeraha

  • Dalili ya kwanza kwa kawaida ni maumivu ya kichwa

  • Huenda ukachanganyikiwa au ukapoteza fahamu

  • Madaktari watatibu matatizo yaliyosababisha kuvuja damu, kama vile shinikizo la juu la damu

Watu walio na dalili yoyote ya kuvuja damu ndani ya ubongo wanapaswa kwenda kwenye kitengo cha dharura mara moja.

Milipuko na Mipasuko: Yanayosababisha Kiharusi cha Kuvuja Damu kwenye Ubongo

Mishipa ya damu kwenye ubongo ikiwa dhaifu, isiyo ya kawaida, au iwe na shinikizo la chini, kiharusi cha kuvuja damu kwenye ubongo kinaweza kutokea. Katika viharusi vya kuvuja damu kwenye ubongo, mtu hutokwa damu ndani ya ubongo, sawa na tishu ya ubongo kuvuja damu. Au kutokwa na damu kunaweza kutokea kati ya safu ya ndani na ya katikati ya tishu inayofunika ubongo (kwenye nafasi ya subaraknoidi), kama kuvuja damu kwenye subaraknoidi.

Ni nini husababisha kuvuja damu ndani ya ubongo?

Kuvuja damu ndani ya ubongo husababishwa na mshipa wa damu kupasuka ndani ya ubongo wako.

Kisababishi cha kawaida zaidi cha mshipa wa damu kupasuka ni shinikizo la damu kuwa juu, hali ambayo hufanya mishipa yako ya damu iwe dhaifu.

Sababu zisizo za kawaida sana ni:

  • Kutumia kokeni au amfetamini (vichangamsho)

  • Kuzaliwa ukiwa na mishipa ya damu isiyo ya kawaida kwenye ubongo wako

  • Jeraha baya la kichwa

  • Uvimbe wa ubongo

  • Kutumia dawa za kuyeyusha damu kupita kiasi

Ni zipi dalili za kuvuja damu ndani ya ubongo?

Dalili za kuvuja damu ndani ya ubongo huanza mara moja. Huwa unapata maumivu makali sana ya kichwa, mara nyingi ukiwa unashughulika. Watu wazee huenda wasipate maumivu ya kichwa au huenda yakawa madogo tu. Dalili nyingine za kawaida ni:

  • Udhaifu au kufa ganzi upande mmoja wa mwili

  • Shida ya kuzungumza

  • Kuchanganyikiwa

  • Kuhisi mgonjwa kwenye tumbo lako au kutapika

  • Vifafa

  • Kuzirai

Kuvuja damu ndani ya ubongo ni tatizo kubwa sana hivi kwamba takribani nusu ya watu wanalolipata hufariki ndani ya siku chache za kwanza. Watu wengi wanaonusurika kifo hupata uharibifu wa kudumu kwenye ubongo.

Daktari wangu atajuaje iwapo ninavuja damu ndani ya ubongo?

Madaktari hushuku kuwa unavuja damu ndani ya ubongo kulingana na dalili zako. Ili kuhakikisha kuwa hawajakosea, watapiga picha zenye maelezo ya kina za sehemu ya ndani ya ubongo wako kwa kutumia upimaji wa picha, kama vile uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku).

Madaktari hutibu vipi tatizo la kuvuja damu kwenye ubongo?

Madaktari watakulaza hospitalini na kutibu matatizo yaliyosababisha kuvuja damu. Watakulazimisha ukae kitandani na uache kutumia dawa zozote ambazo zinaweza kuzidisha hali yako ya kuvuja damu. Huenda pia ukapata:

  • Dawa za kupunguza maumivu ya kichwa na mishtuko yoyote ambayo huenda unapata

  • Dawa na vinywaji vya kudumisha shinikizo la damu kiwango kinachostahili

  • Ikiwa ulikuwa unameza dawa za kuyeyusha damu, huenda ukapata dawa za kusaidia damu yako kugada na kusitisha uvujaji wa damu

  • Wakati mwingine, unaweza kufanyiwa upasuaji wa kuondoa damu ya ziada na kupunguza shinikizo ndani ya fuvu