Maumivu ya Sehemu ya Chini ya Mgongo

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2024

Mshipa wa sehemu ya chini mgongo (lumbar) huwezesha mwili wako kugeuka, kujipinda, na kuinama. Pia inakuwezesha kusimama, kutembea, na kuinua vitu. Sehemu ya chini ya mgongo inahusika katika takriban harakati zote za mwendo. Maumivu katika sehemu ya chini ya mgongo ni ya kawaida sana.

  • Maumivu ya sehmu ya chini ya mgongo kawaida husababishwa na kuinua kitu, kufanya mazoezi, kuanguka, au kuhusika katika ajali ya gari

  • Sababu ya kawaida ya maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo ni mkazo wa misuli

  • Kuimarisha tumbo lako, nyonga, na misuli ya mgongo kunaweza kusaidia kuzuia maumivu ya chini ya mgongo

  • Unaweza kutibu maumivu ya mgongo kwa kuepuka shughuli zinazosababisha mkazo kwenye mgongo wako, kunywa dawa za kupunguza maumivu, na kutumia barafu au joto kwenye mgongo wako, lakini mara nyingi maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo kawaida hupona yenyewe

  • Watu wazee wenye maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo bila sababu dhahiri au "ishara za tahadhari" zilizo hapa chini wanaweza kuhitaji kumwona daktari

Je, napaswa kumwona daktari lini?

Muone daktari wako mara moja ikiwa una maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na mojawapo ya ishara hizi za tahadhari:

  • Kufa Ganzi

  • Udhaifu katika mguu mmoja au yote miwili

  • Matatizo ya kukojoa au kwenda haja kubwa (kinyesi)

  • Homa

  • Wepesi wa kichwa au kuzirai

  • Maumivu makali popote kwenye tumbo lako

Muone daktari wako ndani ya siku moja ikiwa una maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na mojawapo ya ishara hizi za onyo:

  • Historia ya saratani

  • Kupungua uzani

  • Maumivu makali usiku

  • Una umri wa miaka 55 au zaidi na hakuna sababu dhahiri, kama vile jeraha linalosababisha maumivu yako

  • Uko kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi kwa sababu ya dawa unazotumia, upasuaji au jeraha la hivi majuzi, matumizi ya dawa za kulevya au kwa sababu una HIV au UKIMWI

Ikiwa maumivu yako si makali na huna dalili za tahadhari, unaweza kusubiri siku kadhaa kabla ya kuona daktari.

Je, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo husababishwa na nini?

Madaktari huenda wasiweze kujua kila mara kile kinachosababisha maumivu yako ya sehemu ya chini ya mgongo. Chanzo cha kawaida cha maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo ni:

  • Mkazo wa misuli au kano (kano ni vifundo vya tishu ngumu vifupi ambavyo vinashikilia mifupa yako pamoja kwenye kiungo)

Hii inaweza kutokea kwa upande mmoja au pande zote mbili za mgongo wako. Maumivu yako yanazidi kuwa makali unapotembea na ahueni unapopumzika.

Sababu nyingine za kawaida ni pamoja na:

Diski ni tishu zenye sponji kati ya mifupa ya mgongo (vertebrae) ambazo huruhusu mgongo wako kuinama. Diski inapochanwa au kubanwa, nyenzo zinazofanana na jeli zinaweza kuvimba (kuumuka) na zinaweza kuweka shinikizo kwenye neva. Kukohoa au kupiga chafya kunaweza kufanya maumivu ya mkazo wa neva kuwa mabaya zaidi.

Kupungua kwa mfereji wa uti wa mgongo katika sehemu ya chini ya mgongo wako ni sababu ya kawaida ya maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo.

Maumivu yako yanaweza kuwa mabaya zaidi ikiwa:

  • Utainua kitu kizito kwa njia isiyofaa

  • Una unene kupita kiasi

  • Umechoka sana

  • Una mkao mbaya (husimami wima)

  • Huna nguvu nzuri ya misuli kwenye mgongo wako, tumbo, na misuli ya nyonga (misuli kuu)

Je, maumivi makali ya siatika ni nini?

Maumivu ya siatika ni maumivu yanayosababishwa na shinikizo kwenye neva ya siatiki. Neva ya siatiki ndiyo neva kubwa zaidi ya mgongo. Inatoka kwenye sehemu ya chini ya mgongo wako hadi nyuma ya mguu wako. Sababu yoyote ya maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo inaweza kusababisha maumivu makali ya siatika.

Kawaida maumivu makali ya siatika huathiri upande mmoja tu. Unaweza kuhisi hisia ya kudungwa kwa pini na sindano kwenye mikono na miguu, kuwashwa, au kufa ganzi katika sehemu ya mguu wako. Unaweza kuwa na maumivu makali au ya kushtua chini ya sehemu ya nyuma ya mguu wako hadi kwenye goti au mguu wako. Mkazo unaoendelea kwenye neva ni jambo hatari na linaweza kusababisha udhaifu na kufa ganzi wa muda mrefu kwenye mguu wako.

Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?

Daktari wako atakuuliza maswali kuhusu dalili zako na historia ya afya yako na kufanya uchunguzi wa kimwili.

Katika hali fulani, daktari wako anaweza kukufanyia vipimo kama vile eksirei, MRI, (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta), au elektromaiografia na uchunguzi wa uwezo wa neva kupitisha umeme.

Hauhitaji eksirei au uchanganuzi wa MRI kila wakati unapokuwa na maumivu ya mgongo.

Je, daktari wangu atatibu vipi maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo?

Madaktari hukita matibabu kulingana na sababu ya maumivu yako ya sehemu ya chini ya mgongo na muda ambao maumivu yamedumu. Lakini kwa ujumla, maumivu mengi ya sehemu ya chini ya mgongo huisha baada ya utunzaji mzuri wa nyumbani.

  • Ikiwa maumivu yako ni makali, unaweza kuhitaji kupumzika kwa siku moja au mbili

  • Kupumzika sana sio kuzuri kwa sababu kunadhoofisha misuli yako ya mgongo, jambo ambalo linaweza kufanya maumivu yako kuwa mabaya zaidi

  • Shughuli nyepesi husaidia kwa hakika—muulize daktari wako kile unapaswa kufanya na kile hupaswi kufanya

  • Weka joto au baridi kwenye eneo lenye maumivu—baridi inafaa kwa siku 2 za kwanza baada ya jeraha, kisha tumia joto

  • Kunywa dawa ya maumivu kama vile asetaminofeni, ibuprofeni, au naprokseni

  • Unapolala chini, unaweza kuhisi vizuri zaidi ukilala kwa upande huku magoti yakiwa yamekunja

Haraka iwezekanavyo, daktari wako atahakikisha umeanza kufanya mazoezi mepesi ili kuimarisha mgongo wako. Misuli yenye nguvu hufanya mgongo uwe thabiti hivyo hautaskia maumivu mengi. Unaweza kutumwa kwa tibamaungo. Wataalamu wa tibamaungo wanaweza kukufundisha mazoezi ya mgongo ili uweze kuyafanya mwenyewe. Wanaweza pia kukufundisha jinsi ya kuinua vitu na kutembea vizuri ili uweze kufanya kazi kwa usalama.

Ikiwa madaktari wana uhakika kuwa maumivu hayatokani na mkazo wa neva au ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo, unaweza kujaribu:

  • Kukandwa

  • Matibabu kutoka kwa mtaalamu wa afya anayehusika katika kutambua na kutibu matatizo ya mifupa na misuli kupitia marekebisho ya uti wa mgongo

Kwa maumivu ya muda mrefu, madaktari wanaweza kupendekeza:

  • Kupunguza uzani

  • Kuchochea neva ya umeme inayopita kwenye ngozi (TENS), tiba ya umeme nyumbani ambayo hukupa hisia ya kutekerenywa na inaweza kutumika mara kadhaa kwa siku—daktari wako atakutuma kwa mtaalamu tibamaungo ili kukusaidia kujifunza jinsi ya kutumia kifaa hiki

  • Kudunga kotikosteroidi (kama vile dexamethasone au methylprednisolone) pamoja na dawa ya kufisha ganzi kwenye nafasi ya mgongo (nafasi kati ya uti wa mgongo na safu ya nje ya tishu inayofunika uti wa mgongo wako)

  • Upasuaji

Kuna aina nyingi tofauti za upasuaji wa mgongo. Kwa kawaida, madaktari hupendekeza upasuaji tu wakati una dalili za mkazo mkali wa neva au ikiwa maumivu yako ni makali sana na hayapunguki kwa matibabu mengine yote.

Je, ninawezaje kuzuia maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo?

  • Fanya mazoezi ya kunyoosha na kuimarisha misuli ya tumbo, nyonga na mgongo

  • Hakikisha mgongo wako uko wima wakati umesimama na kuketi (kukaa kwa mkao mbaya huleta mkazo kwa mgongo wako)

  • Keti huku miguu yako ikiwa kwenye sakafu, sio ikiwa miguu imepishana

  • Usisimame wala kuketi kwa muda mrefu

  • Unapoinua vitu, inua kwa miguu yako, sio mgongo wako

Mazoezi ya Kuzuia Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo

Kuinua na Kushusha Sehemu ya Nyonga

Lala kwa mgongo huku magoti yakiwa yamekunjwa, visigino vikiwa sakafuni, na uzani ukiwa kwenye visigino. Kaza sehemu ya chini ya mgongo dhidi ya sakafu, kaza makalio (ukiyainua kama nusu inchi kutoka sakafuni), na ukaze misuli ya tumbo. Shikilia nafasi na uhesabu hadi 10. Rudia mara 20.

Kuinua Sehemu ya Juu ya Mwili

Lala kwa mgongo huku magoti yakiwa yamekunjwa na miguu ikiwa sakafuni. Weka mikono yapishane kwenye kifua. Kaza misuli ya tumbo, huku ukiinua mabega taratibu kama inchi 10 kutoka sakafuni huku ukiwa umeinamisha kichwa nyuma (kidevu kisiguse kifua). Kisha wachilia misuli ya tumbo, huku ukiyaachilia mabega polepole. Fanya seti 3 za miinuko 10.

Kunyoosha Magoti Hadi Kifuani

Lala kwa mgongo sakafuni. Weka mikono yote nyuma ya goti moja na uilete kifuani. Shikilia na uhesabu hadi 10. Shusha mguu huo polepole na urudie na mguu huo mwingine. Fanya zoezi hili mara 10.

Mazoezi ya Kunyoosha Ukiwa Umeketi Huku Mguu Umenyooshwa

Keti sakafuni huku magoti yakiwa yameinama kidogo (sio kufungwa) na miguu ikiwa imetengana kadri inavyowezekana. Weka mikono yote miwili kwenye goti moja. Telezesha mikono yote miwili polepole kuelekea kwenye kifundo cha mguu. Acha ikiwa utahisi maumivu, na usiende mbali zaidi ya nafasi ambayo unaweza kushikilia kwa urahisi kwa sekunde 10. Rejelea nafasi ya kukaa taratibu. Rudia kwa mguu huo mwingine. Fanya zoezi hili mara 10 kwa kila mguu.