Chunjua ni nini?

Chunjua ni viota vidogo vya ngozi vinavyosababishwa na virusi viitwavyo virusi vya papiloma vya binadamu (HPV). Kuna aina nyingi tofauti za HPV. Chunjua zinaweza kukua kwenye sehemu yoyote ya ngozi yako, na zinaweza pia kuenea kwa watu wengine.

  • Chunjua zinaweza kuwa viota vinavyoinuka au bapa

  • Zinaweza kuonekana kwenye ngozi ya kawaida au kwenye sehemu zako za siri

  • Chunjua hutokea kwa watu wa umri wote, lakini mara nyingi hutokea sana kwa watoto

  • Chunjua nyingi hazina madhara, lakini aina fulani za chunjua za uzazi zinaweza kusababisha saratani

  • Ikiwa chunjua yako haitatoweka yenyewe, madaktari wanaweza kuiondoa kwa kemikali, kuigandisha, au kwa kuchoma na kukata

  • Chanjo inaweza kuzuia maambukizi na aina fulani za HPV, hasa aina ambazo pia zinaweza kusababisha saratani

Ni nini husababisha chunjua?

Chunjua husababishwa na aina ya virusi vinavyoitwa HPV. Kuna zaidi ya aina 100 za HPV. Unaweza kupata chunjua kwa kugusa chunjua ya mtu mwingine, ikiwa ni pamoja na kufanya ngono na mtu ambaye ana chunjua kwenye uume, uke, au rektamu. Ngono ya mdomo inaweza kusababisha maambukizi ya HPV mdomoni au kooni.

Watoto na vijana wana uwezekano mkubwa wa kupata chunjua. Hatari pia ni kubwa kwa watu walio na mfumo wa kingamwili dhaifu, kama vile walio na VVU/UKIMWI au wale ambao wamepandikizwa viungo.

Ni aina gani maalum za chunjua?

Chunjua za kawaida:

  • Ni viota vidogo, imara vyenye uso mgumu na vinaweza kuwa vya kijivu, njano, kahawia, au vyeusi

  • Huonekana kwenye sehemu za mwili ambazo mara nyingi hujeruhiwa, kama vile magoti, uso, vidole au viwiko vyako

  • Zinaweza kuenea kwenye ngozi iliyo karibu

Chunjua za miguu na za kiganja:

  • Ni ngumu, tambarare, na za kukwaruza na zinaweza kuwa za kijivu au kahawia na sehemu ya kati ambayo ni ndogo nyeusi

  • Chunjua za kiganja zinaonekana kwenye kiganja cha mkono wako

  • Chunjua za miguu huonekana kwenye nyayo za miguu wako lakini zinaweza kuonekana kama viota vilivyoinuka juu ya mguu wako au kwenye vidole vyako

  • Chunjua za miguu mara nyingi huwa laini na zinaweza kuwa chungu unaposimama au kutembea

Chunjua za nakshi ni vikundi vya chunjua ndogo za miguu au za mikono ambazo huungana pamoja.

Chunjua za karibu na kucha:

  • Ni viota vinene karibu na kucha ambavyo vinaweza kuwa na muundo wa koliflawa

  • Zinaweza kusababisha matatizo kama vile maambukizi kwenye ngozi karibu na kucha

  • Kawaida hutokea kwa watu wanaouma kucha zao au mara nyingi huwa na mikono yenye maji, kama vile wanaosafisha vyombo

Chunjua uzi:

  • Ni viota virefu, vyembamba, vidogo ambavyo kawaida huonekana kwenye kope, uso, shingo, au midomo yako

  • Kwa kawaida ni rahisi kutibu

Chunjua bapa:

  • Zinapatikana zaidi kwa watoto na vijana

  • Kwa kawaida huonekana katika vikundi kama madoa laini bapa, ya manjano-kahawia, waridi, au rangi ya ngozi

  • Mara nyingi huonekana kwenye uso wako, sehemu za juu za mikono yako, kwenye alama za mikwaruzo, au mahali unaponyoa—kama vile kwenye ndevu za mwanamume au kwenye miguu ya mwanamke

  • Zinaweza kuwa ngumu kutibu

Chunjua sehemu za siri:

  • Huonekana kwenye uume, tundu la haja kubwa, valva, uke, au mlango wa kizazi

  • Zinaweza kuwa tambarare na laini au zinaweza kuwa uvimbe kama kaliflawa

  • Mara nyingi huwasha ikiwa ziko karibu na tundu la haja kubwa

  • Huenezwa kwa kufanya ngono

  • Huongeza hatari ya saratani katika eneo ambapo chunjua zipo

  • Zinaweza kuzuiwa kwa kupata chanjo ya HPV

Madaktari wanawezaje kujua kama nina Chunjua?

Madaktari hutambua chunjua kwa jinsi zinavyoonekana. Ikiwa una kiota cha ngozi ambacho madaktari hawatambui, wanaweza kukiondoa ili kutazama kwa hadubini (uondoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi).

Madaktari wanatibu vipi chunjua?

Chunjua nyingi hupotea bila matibabu kwa mwaka mmoja au miwili, hasa chunjua za kawaida. Ikiwa una chunjua sehemu za siri, madaktari watazitibu kwa krimu, kemikali, au wakati mwingine upasuaji. Madaktari wataondoa aina nyingi za chunjua kwa kutumia kemikali, kugandisha, kuchoma kwa leza, au kuzikata. Matibabu yanategemea aina ya chunjua, mahali zilipo kwenye mwili wako, na ukubwa wake.

Aina yoyote ya chunjua inaweza kurudi baada ya kuondoka au kuondolewa, hasa chunjua za miguu.

Kuondoa chunjua kwa kutumia krimu za kemikali na vimiminiko:

  • Madaktari kwa kawaida hutumia krimu au vimiminiko vilivyo na asidi ya salicylic, asidi ya trichloroacetic, au kemikali nyinginezo zinazofanya chunjua kutoweka au kuchibuka

  • Kemikali nyingine unaweza kujipaka mwenyewe ukiwa nyumbani kwa kufuata maagizo kwa uangalifu ili usichome ngozi yako

  • Wewe au daktari wako mnahitaji kukwangua tishu zilizokufa za chunjua kabla ya kila matibabu

  • Ili kuondoa chunjua, wewe au daktari wako itabidi kuitibu mara nyingi kwa wiki kadhaa hadi miezi

Kuondoa chunjua kwa kutumia kugandisha (matibabu kwa baridi):

  • Madaktari kawaida hutumia kugandisha kutibu chunjua za miguu, chunjua uzi, na chunjua za chini ya vidole

  • Madaktari wanaweza kufanya eneo hilo liwe bila hisia wakati wa kutibu kwa watoto

  • Kwa kawaida utahitaji kupata matibabu mengi kwa mwezi mmoja, hasa ikiwa chunjua zako ni kubwa

Kuondoa chunjua kwa kutumia kuchoma na kukata:

  • Madaktari hutumia leza au mkondo wa umeme kuchoma chunjua

  • Matibabu haya hufanya kazi vizuri lakini yanaumiza zaidi na kwa kawaida huacha kovu