Muhtasari wa Matatizo ya Wasiwasi

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Je, ugonjwa wa wasiwasi ni nini?

Wasiwasi ni kuwa na hofu au uwoga. Wasiwasi ni jambo la kawaida. Kwa mfano, watu wengi huwa na wasiwasi wanapokuwa na matatizo ya pesa, matatizo kazini, au matatizo ya kifamilia.

Hata hivyo, unaweza kuwa na ugonjwa wa wasiwasi ikiwa:

  • Una wasiwasi mara nyingi hata wakati huna matatizo au matatizo si mabaya

  • Wasiwasi umezidi sana na kuathiri maisha yako

Kuwa na wasiwasi kidogo kunaweza kukusaidia kuwa makini, lakini kuwa na wasiwasi mwingi hufanya iwe vigumu kufanya mambo vizuri.

  • Mbali na kuwa na wasiwasi, unaweza kuhisi kukosa pumzi, kizunguzungu, na kutokwa na jasho na kuwa na moyo kupiga haraka

  • Baadhi ya matatizo ya kiafya yanaweza kusababisha wasiwasi (kwa mfano, ugonjwa wa moyo, matatizo ya mapafu, au tezi dundumio inayotoa homoni zaidi)

  • Dawa nyingi na dawa za kulevya zinaweza kusababisha au kuzidisha wasiwasi (kwa mfano, amfetamini, kafeini, kokeni, na dawa ya kupunguza uvimbe)

  • Watu walio na wasiwasi wana uwezekano mkubwa wa kuwa na unyogovu kuliko watu wengine

  • Madaktari hutibu magonjwa ya wasiwasi kwa dawa na tiba

Je, ugonjwa wa wasiwasi husababishwa na nini?

Madaktari hawajui haswa kile kinachosababisha wasiwasi, lakini mambo yafuatayo huzindisha uwezekano wa kuwa nayo:

  • Historia ya familia ya kuwa na wasiwasi (hurithiwa)

  • Tukio la maisha lenye kusumbua, kama vile janga la asili au kuvunjika kwa uhusiano

  • Matatizo fulani ya kiafya, kama vile pumu

  • Matumizi ya vitu fulani, kama vile pombe

Je, dalili za ugonjwa wa wasiwasi ni zipi?

Dalili zinajumuisha:

  • Wasiwasi, uwoga, au hofu

  • Matatizo ya kupumua, kizunguzungu, na Mapigo ya moyo ya haraka

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ugonjwa wa wasiwasi?

Madaktari hukufanyia uchunguzi na kukuuliza maswali kuhusu dalili zako. Madaktari huzingatia matatizo na magonjwa mengine ambayo yana ishara na dalili zinazofanana na wasiwasi. Ikiwa hawatapata sababu nyingine, madaktari hufanya utambuzi wa kuwa una ugonjwa wa wasiwasi ikiwa wasiwasi wako:

  • Unakutatiza

  • Unavuruga uwezo wako wa kufanya kazi na shughuli za kila siku

  • Umedumu kwa muda mrefu au unarudi mara kwa mara

Je, madaktari hutibu vipi magonjwa ya wasiwasi?

Ikiwa wasiwasi wako unasababishwa au kuzidishwa na tatizo la kiafya au matumizi ya dawa za kulevya, madaktari watatibu tatizo hilo.

Madaktari hutibu magonjwa ya wasiwasi kwa:

  • Tiba

  • Dawa, kama vile za vizuizi vya uchaguzi wa kuchukua tena serotonini (SSRI)