Je, shambulio la hofu ni nini?
Shambulio la hofu ni wakati unapopata hofu na wasiwasi sana ghafla. Unaweza pia kuwa na maumivu ya kifua na kuhisi kana kwamba unakabwa koo na kuhisi maumivu tumboni, kizunguzungu, na matatizo ya kupumua. Shambulio la hofu hudumu kwa muda mfupi.
Mashambulizi ya hofu yanaweza kuchochewa na kitu cha kutisha, kama vile kuona nyoka, au yanaweza kutokea yenyewe
Wakati wa shambulio la hofu, unaweza kufikiria kuwa una shida kubwa ya matibabu, kama vile shambulio la moyo au kiharusi
Ingawa mashambulizi ya hofu ni mabaya na yanatisha, si hatari
Mashambulizi ya hofu ni ya kawaida—kila mwaka, takriban 1 kati ya watu 10 wazima wanapata shambulizi la hofu
Je, tatizo la hofu ni nini?
Shambulio la hofu ni pale unapopata mashambulizi ya hofu mara kwa mara na pia:
Kuwa na wasiwasi sana kuhusu kupata mashambulizi zaidi
Kuwa na wasiwasi kwamba unakuwa wazimu au kwamba utapoteza udhibiti wa nafsi yako
Kuepuka kwenda mahali au kufanya shughuli zako za kawaida kwa sababu unafikiria kuwa unaweza kupata shambulio
Je, mashambulizi ya hofu husababishwa na?
Mashambulizi ya hofu yanaweza kuchochewa na kitu ambacho unakihofia. Kwa mfano, ikiwa unaogopa nyoka, unaweza kupata shambulio la hofu unapoona nyoka. Lakini wakati mwingine mashambulizi ya hofu hutokea bila sababu yoyote. Pia, madaktari hawana uhakika kwa nini baadhi ya watu hupata mashambulizi ya hofu wakati jambo la kutisha linatokea na baadhi hawapati.
Je, dalili za shambulio la hofu ni zipi?
Ingawa mashambulizi ya hofu hayafurahishi na yanatisha, sio hatari. Dalili huanza haraka, na kufika kileleni ndani ya dakika 10, na kutoweka dakika chache baadaye.
Dalili kuu ni:
Woga na maumivu ya ghafla
Watu hupata pia angalau dalili 4 kati ya zifuatazo:
Maumivu ya kifua au kujihisi vibaya
Kuhisi kama unakabwa koo
Kizunguzungu au kuhisi kuzirai
Kuhisi kichefuchefu au kuwa na maumivu ya tumbo au kuhara
Kufa ganzi kwenye midomo na vidole
Kuhisi moyo wako ukidunda au kupiga kwa haraka
Kuhisi kukosa pumzi au kana kwamba unasakamwa
Kutokwa jasho
Kutingishika au kutetemeka
Kuwa na hofu kuwa unakufa
Hofu kuwa unakuwa wazimu au unapoteza udhibiti
Kuhisi kana kwamba vitu vinavyokuzunguka sio halisi
Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina mashambulizi ya hofu?
Daktari wako atachunguza chanzo cha kimwili cha dalili zako. Kwa mfano, ikiwa una maumivu ya kifua, madaktari watachunguza moyo wako. Ikiwa dalili zako hazina chanzo cha kimwili, madaktari watashuku kuwa una mashambulizi ya hofu.
Je, madaktari hutibu vipi mashambulizi ya hofu au tatizo la hofu?
Baadhi ya watu hupata nafuu bila matibabu. Kwa wengine, mashambulizi ya hofu hutokea na kupotea kwa miaka mingi. Matibabu ya mashambulizi ya hofu na tatizo la hofu yanaweza kujumuisha:
Tiba, kama vile tiba ya kuzoeshwa, tiba ya tabia-tambuzi, au tiba ya usaidizi wa kisaikolojia
Dawa za kuzuia mfadhaiko
Dawa za kuzuia wasiwasi
Tiba ya kukuzoesha kitu unachokiogopa husaidia kupunguza hofu kwa:
Kukuzoesha pole pole na mara kwa mara kwa kitu chochote kinachochochea mashambulizi yako hadi utakapokizoea
Tiba ya tabia-tambuzi hukufundisha:
Kutoepuka hali zinazosababisha mashambulizi ya hofu
Kutambua wakati hofu zako si za kweli
Kukabiliana na mashambulizi kwa kuvuta pumzi polepole au mbinu zingine za kujituliza
Usaidizi wa kisaikolojia unajumuisha elimu na ushauri ili kukupa:
Maelezo ya jumla kuhusu ugonjwa huo na matibabu yake
Matumaini ya kweli ya kuboresha hali
Usaidizi unaotokana na uhusiano wa kuaminiana na daktari