Muhtasari wa Mapafu

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Je, mapafu ni nini?

Mapafu ni viungo vinavyohusika katika upumuaji.

  • Kupumua ni mchakato wa hewa kuingia na kutoka kwenye mapafu yako

  • Unaingiza oksijeni unapovuta pumzi ndani (vuta hewa) na kuondoa kaboni dioksidi unapotoa pumzi nje (toa hewa)

Seli zote mwilini mwako zinahitaji oksijeni ili kubadilisha chakula kuwa nishati. Mchakato wa kubadilisha chakula kuwa nishati hutengeneza takataka katika muundo wa kaboni dioksidi, ambazo lazima ziondolewe kwenye mwili wako.

Una mapafu 2 kwenye kifua chako, yaliyozungukwa na kizimba cha mbavu. Hewa huingia kwenye mapafu yako kupitia bomba la upepo, ambalo pia huitwa koo. Bomba la upepo hugawanyika katika njia ndogo za hewa zinazoitwa koromeo. Kama matawi ya mti, koromeo hugawanyika katika njia ndogo zaidi zinazoitwa bronkioli. Pande za mwisho za bronkioli zina mamilioni ya vifuko vya hewa vinavyoitwa alveoli.

Njia zako za hewa pia hutengeneza ute unaofunika utando wake. Ute huo hunasa vumbi na vijidudu ili visiingie kwenye mapafu yako. Njia zako za hewa pia zina vinywele vidogo sana. Vinywele vidogo hivyo husukuma ute kwenye trakea, na hatimaye ute huo unaukohoa kuutoa au unaumeza.

Kifuniko kidogo kinachoitwa kimio huzuia chakula kuongia kwenye bomba la upepo wakati unapomeza.

Ndani ya Mapafu na Mkondo wa Hewa

Je, upumuaji hufanyaje kazi?

Mtu mzima wa wastani hupumua takriban mara 15 kila dakika akiwa amepumzika. Mtu aliye na shughuli za wastani hupumua galoni 5,000 (karibu lita 20,000) za hewa kwa kila saa 24.

Ubongo wako hutuma ujumbe kiotomatiki ili upumue, hata ukiwa umelala au kuzimia.

  • Ubongo wako hufuatilia viwango vya oksijeni, kaboni dioksidi, na asidi katika damu yako

  • Viwango hivi huamua kasi na kiasi cha uvutaji hewa ambacho ubongo wako itakufanya upumue

Ubongo wako hutuma ishara kwenye misuli ya mbavu na kiwambo ili kukufanya upumue. Ili kuvuta hewa ndani, misuli iliyo katikati ya mbavu zako hukaza na kiwambo chako hukaza. Kiwambo chako ni msuli mkubwa, bapa ambao hutenganisha kifua chako na tumbo. Mapafu yako hayana misuli yake yenyewe.

  • Kukaza kwa misuli ya mbavu na kiwambo chako hupanua kifua chako na kuvuta hewa ndani

  • Pale misuli hii inapolegea, kifua chako hupungua na kutoa hewa nje

Jukumu la Kiwambo katika Upumuaji

Kiwambo kinapokaza na kushuka chini, mvungu wa kifua hupanuka, na kupunguza shinikizo la ndani ya mapafu. Ili kusawazisha shinikizo, hewa huingia kwenye mapafu. Kiwambo kinapolegea na kupanda juu, mnyumbuko wa kuta za mapafu na kifua husukuma hewa nje ya mapafu.

Nini hutokea kwenye hewa iliyo kwenye mapafu?

Mapafu yako yana vifuko vidogo vya hewa vinavyoitwa alveoli. Damu hutiririka kupitia kuta za vifuko vya hewa na kuchukua oksijeni kutoka kwenye hewa iliyo kwenye vifuko. Wakati huo huo, kaboni dioksidi hutoka kwenye damu yako na kuingia kwenye vifuko vya hewa. Kisha kaboni dioksidi inaweza kuondoka mwilini mwako utakapotoa hewa nje.

Damu yote kwenye mwili wako hupita kwenye mapafu kila dakika au zaidi. Hiyo inamaanisha mapafu yanahitaji kiasi kikubwa cha mishipa ya damu.

Ubadilishanaji wa Gesi Baina ya Nafasi za Alveoli na Kapilari

Kazi ya mfumo wa upumuaji ni kuhamisha gesi mbili: oksijeni na dioksidi kaboni. Ubadilishanaji wa gesi hufanyika katika mamilioni ya alveoli kwenye mapafu na kapilari zinazozifunika. Kama inavyoonyeshwa hapa chini, oksijeni iliyovutwa ndani huhama kutoka kwenye alveoli hadi kwenye damu iliyo kwenye kapilari, na kaboni dioksi huhama kutoka kwenye damu iliyo kwenye kapilari hadi kwenye hewa iliyo kwenye alveoli.

Je, ni matatizo gani yanaweza kutokea kwa mapafu yako na upumuaji?

Matatizo yanayohusisha ubongo, kama vile kiharusi, kuzidisha kiasi cha dawa, au ulevi mkubwa wa pombe, vinaweza kuingilia sehemu ya ubongo wako inayohusika na kudhibiti upumuaji. Matatizo haya yanaweza kufanya upumuaji kuwa wa taratibu sana au hata kusimamisha upumuaji.

Njia zako za hewa na mapafu yanaweza kupata maambukizi, hivyo kusababisha mkamba, , bronkiolitisi, au nimonia, kutegemea na mahali maambukizi yalipo. Nimonia ni maambukizi ya alveoli.

Njia za hewa zinaweza kuwa nyembamba kutokana na pumu au kuzibwa na kitu kutoka nje ya mwili kama vile kipande cha chakula.

Mishipa ya damu ndani ya mapafu yako inaweza kuzuiwa na damu iliyoganda, hali inayoitwa kuziba kwa mishipa ya mapafu.