Muhtasari wa Figo na Njia ya Mkojo

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2023

Je, figo ni nini?

Figo zako ni viungo 2 vyenye umbo la maharagwe vinavyotoa mkojo. Zinalingana na ukubwa wa ngumi yako. Ziko nyuma ya fumbatio, pande zote mbili za mgongo wako.

Figo husawazisha viwango vya maji na madini mwilini na kuchuja uchafu kwenye damu.

Uharibifu wa figo moja hausababishi matatizo makubwa ili mradi figo yako nyingine iwe inafanya kazi—figo zote mbili zinapaswa kuacha kufanya kazi ili wewe kupata matatizo makubwa.

  • Kazi ya msingi ya figo zako ni kuweka uzani wa maji na elektroliti katika mwili wako.

  • Hufanya kazi hii kwa kurekebisha kiasi cha maji na elektroliti kinachoingia kwenye mkojo

  • Figo pia huchuja takataka, husaidia kudhibiti shinikizo la damu, na kutoa (kuachia) baadhi ya homoni

Je, njia ya mkojo ni nini?

Njia ya mkojo ni njia ambayo hupitisha mkojo na kuutoa nje ya mwili wako. Njia yako ya mkojo inajumuisha:

  • Figo

  • Ureta

  • Kibofu cha mkojo

  • Mrija wa Mkojo

Njia ya Mkojo

Figo zinatengeneza mkojo, ambao hutoka kupitia ureta na kuingia kwenye kibofu cha mkojo. Kutoka kwenye kibofu cha mkojo, mkojo huingia kwenye mrija wa mkojo. Mkojo hutoka mwili kupitia uume kwa wanaume na uke kwa wanawake.

Ureta

Ureta zako ni bomba za misuli ambazo husafirisha mkojo kati ya figo na kibofu chako cha mkojo. Hujibana ili kusukuma mkojo upite.

Kibofu cha mkojo

Kibofu cha mkojo ni kifuko cha misuli ambacho hubeba mkojo. Hutanuka ili kuhifadhi mkojo ambao umetengenezwa na figo.

Kibofu cha mkojo kinapojaa, ishara za neva hukujulisha ili utoe mkojo. Sfinkta za mkojo hufunguka, na mkojo hupita hadi kwenye mrija wa mkojo.

Mrija wa Mkojo

Mrija wa mkojo ni bomba ambalo linabeba mkojo na kuutoa nje ya mwili wako.

Wanaume wana mrija wa mkojo unaokomea kwenye ncha ya uume wao. Wanawake wana mrija wa mkojo mfupi zaidi ambao hukomea kwenye uke wao. Mrija wa mkojo mfupi unamaanisha kwamba ni rahisi zaidi kwa bakteria kutoka nje ya mwili kufikia kibofu cha mkojo na kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo.