Muhtasari wa Tezi Dundumio

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024
Nyenzo za Mada

Je, tezi dundumio ni nini?

Dundumio lako linapatikana chini ya kongomeo mbele ya shingo lako. Tezi huzalisha na kutoa homoni. Homoni zinachochea seli au tishu nyinginezo kuchukua hatua. Dundumio hutengeneza homoni za dundumio.

Locating the Thyroid Gland

Homoni za dundumio ni nini?

Homoni za dungumio hudhibiti kasi ya utendakazi wa kemikali za mwili wako (kiwango cha kimetaboli). Karibu kila seli mwilini inahitaji homoni za dundumio. Miongoni mwa majukumu mengine mengi, homoni za dundumio husaidia kudhibiti:

  • Jinsi mwili unavyotumia kalori

  • Jinsi moyo wako unavyopiga haraka

  • Joto la mwili wako

Kuna homoni 2 za dundumio:

  • T3

  • T4

Iodini inahitajika na tezi dundumio ili kutengeneza homoni za dundumio. Unahitaji tu kiasi kidogo cha iodini. Lakini ikiwa tezi dundumio yako haitapata iodini, haitaweza kutengeneza homoni za dundumio za kutosha (hali inayoitwa dundumio lisiloamilifu).

Nini kinachodhibiti homoni za dundumio?

Tezi ya pituitari katika ubongo wako inatengeneza homoni inayoitwa TSH.

  • TSH inaiambia tezi dundumio kutengeneza homoni za dundumio

Ikiwa tezi ya pituitari itabaini kuna kiasi kidogo sana cha homoni ya dundumio kwenye damu yako, hutoa zaidi TSH ili kusisimua tezi dundumio yako iweze kutengeneza zaidi homini ya dundumio. Ikiwa kuna homoni ya dundumio nyingi sana kwenye damu yako, pituitari yako inatoa TSH kidogo. Kisha tezi dundumio yako inatengeneza homoni ya dundumio kidogo.

Madaktari wanapima vipi tezi dundumio yako?

Vipimo vikuu vya tezi dundumio yako ni:

  • Vipimo vya damu

  • Vipimo vya picha

Vipimo vya damu vya dundumio hupima viwango vya:

  • Homoni dundumio

  • TSH

Kiwango cha juu cha TSH kwa kawaida humaanisha huna homoni za dundumio za kutosha. Na kiwango cha chini sana cha TSH kwa kawaida humaanisha unayo nyingi sana.

Vipimo vya picha vinajumuisha:

  • Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti, kuona ikiwa dundumio lako limetanuka

  • Vipimo vinavyotumia kemikali nunurishi

Kupitia vipimo vya kemikali nunurishi, madaktari wanakupa kiasi kidogo cha iodini ya mionzi. Kwa kuwa tezi dundumio inahitaji iodini, inachukua iodini ya mionzi. Madaktari wanagundua iodini ya mionzi kwa kutumia kamera maalumu. Ikiwa tezi dundumio yako haifanyi kazi, haitachukua iodini kwa kawaida. Kamera pia inaweza kugundua vitu vidogo vilivyoota (vinundu) kwenye dundumio lako. Kipimo hiki hakitumii mionzi mingi kuweza kukudhuru.