Je, upungufu wa homoni ya ukuaji ni nini?
Upungufu wa homoni ya ukuaji ni hali inayosababishwa na tezi ya pituitari kutotengeneza homoni ya kutosha ya ukuaji. Hii inaweza kusababisha ukuaji duni wa jumla na kimo kifupi.
Kimo kifupi ni urefu ambao ni mfupi kuliko takriban watoto wengine wote wa umri na jinsia sawa
Kimo kifupi hakimaanishi kuwa kuna shida kila wakati
Dalili zingine za upungufu wa homoni ya ukuaji hutegemea umri wa mtoto na chanzo cha upungufu huo
Ikiwa watoto hawana homoni ya kutosha ya ukuaji, madaktari huwadunga sindano za homoni za ukuaji
Kimo kifupi si kitu sawa na ugonjwa unaojulikana na ukuaji mfupi wa mifupa kuliko kawaida, ambayo pia huitwa osteochondrodysplasia. Watoto walio na ugonjwa unaojulikana na ukuaji mfupi wa mifupa kuliko kawaida wana tatizo la jeni ambalo husababisha ukuaji usio wa kawaida wa mfupa na gegedu pamoja na kimo kifupi.
Je, ni nini husababisha upungufu wa homoni ya ukuaji?
Homoni ya ukuaji ni mjumbe kemikali ya mawasiliano inayotengenezwa kwenye tezi ya pituitari kwenye ubongo wako. Inatuma ishara kwa tishu zote katika mwili wako kuongezeka na kukua. Mara nyingi, madaktari hawajui kwa nini mtoto hana homoni ya kutosha ya ukuaji. Lakini wakati mwingine inasababishwa na matatizo mengine ya kiafya kama vile:
Uvimbe au jeraha la ubongo
Mionzi
Maambukizi, kama vile homa ya uti wa mgongo na kifua kikuu
Je, dalili za upungufu wa homoni ya ukuaji ni zipi?
Dalili kuu za upungufu wa homoni ya ukuaji ni:
Viwango duni vya ukuaji kwa jumla
Kuwa mfupi sana ukilinganisha na watoto wengine wa rika na jinsia sawa
Watoto walio na upungufu wa homoni ya ukuaji kwa kawaida:
Hukua polepole
Hupata meno yao ya utu uzima baadaye kuliko kawaida
Huwa na uwiano wa kawaida (mikono na miguu yao inalingana na urefu wao)
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana upungufu wa homoni ya ukuaji?
Madaktari watafanya:
Kupima urefu na uzani wa mtoto wako na kuuchora kwenye chati za ukuaji
Kufanya eksirei za mifupa ya mkono wa mtoto wako ili kupima umri wa mifupa
Ili kujua kiini cha ukuaji polepole wa mtoto wako, madaktari wanaweza kufanya:
MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) ya kichwa
Vipimo vya damu
Madaktari hufanya MRI ya kichwa ili kuangalia uvimbe au matatizo mengine ya tezi inayotengeneza homoni ya ukuaji (tezi ya pituitari).
Je, madaktari wanatibu vipi upungufu wa homoni ya ukuaji?
Madaktari hutibu upungufu wa homoni ya ukuaji kwa kutumia:
Sindano za homoni ya ukuaji
Homoni ya ukuaji itafanya kazi tu ikiwa inatolewa kabla ya mifupa kuacha kukua.
Ikiwa mtoto wako ana uvimbe wa ubongo, madaktari wanaweza kufanya upasuaji ili kuuondoa.