Maumivu Sugu

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Je, maumivu sugu ni nini?

Maamivu sugu ni maumivu yanayodumu kwa muda mrefu au yanayojirudia kwa miezi au miaka.

  • Maumivu sugu yanaweza kutokea kwa sababu ya ugonjwa au jeraha la muda mrefu ambalo haliponi

  • Wakati mwingine mfumo wako wa neva kuhisi sana ishara za maumivu kuliko kawaida

  • Unaweza kuwa na dalili nyingine kama vile kuhisi uchovu, matatizo ya kulala, kutohisi njaa, au kutovutiwa na kujamiiana

  • Unaweza pia kuwa na dalili za kihisia, kama vile mfadhaiko, wasiwasi au kujitenga na shughuli za kijamii

  • Madaktari wanaweza kutibu maumivu sugu kwa kutumia dawa, matibabu ya kimwili, na matatibu ya dalili za kihisia

Je, nini husababisha maumivu sugu?

Maumivu sugu husababishwa na matatizo endelevu kama vile:

  • Ugonjwa endelevu uliodumu kwa muda mrefu kama vile saratani, ugonjwa wa baridi yabisi, kisukari, au uyabisi wa misuli

  • Jeraha ambalo halijapona kabisa

Pia, ikiwa neva zako zinatuma ishara za maumivu kila wakati, wakati mwingine hiyo husababisha mabadiliko ya muda mrefu katika jinsi neva zako zinavyofanya kazi. Mabadiliko haya yanaweza kukufanya uwe na hisia kali kwa ishara za maumivu. Hii inaweza kufanya maumivu yaliyopo yaonekane kuwa mabaya zaidi na wakati mwingine kusababisha maumivu kutokana na kitu ambacho kwa kawaida hakisababishi maumivu.

Wakati mwingine madaktari hawajui nini husababisha maumivu sugu kwa mtu.

Je, dalili za maumivu sugu ni zipi?

Unaweza kuwa dalili zingine sambamba na maumivu, kama vile:

  • Uchovu

  • Kukosa usingizi

  • Kukosa hamu ya kula na kupungua uzani

  • Kupoteza hamu ya ngono na shughuli nyingine za kujifurahisha

  • Mfadhaiko

  • Wasiwasi

Maumivu sugu yanaweza kuifanya iwe vigumu kufanya kazi na kufanya shughuli za kawaida za kila siku.

Je, madaktari hutibu vipi maumivu sugu?

Iwapo madaktari watagundua chanzo cha maumivu, watatibu chanzo hicho.

Pia madaktari hutibu maumivu sugu kwa kutumia:

Tiba ya tabia inaweza kukusaidia kufanya kazi vizuri, hata ikiwa haipunguzi maumivu yako. Inaweza kujumuisha kwenda nje hatua kwa hatua, zaidi kwenye matukio ya kijamii na kufanya shughuli zaidi za kimwili. Pia inaweza kuhusisha kuwaomba wanafamilia na wafanyakazi wenzako kujiepusha vitu ambavyo hukufanya uzingatie maumivu, kama vile kukuuliza kuhusu afya yako kila mara au kusisitiza kwamba hupaswi kufanya kazi za kila siku.

Dawa ya maumivu

Kutegemea na kiwango cha maumivu yako, dawa zinaweza kujumuisha:

  • NSAID—dawa za maumivu za kununua duka la dawa, kama vile aspirini au ibuprofen

  • Opioid—dawa kali za kutuliza maumivu ambazo hutolewa kwa agizo la daktari

  • Dawa za kuzuia mfadhaiko au dawa za kutibu dalili nyingine

Maumivu yako yanaweza kutofautiana siku nzima. Madaktari wanaweza kubadilisha kipimo cha dawa na muda wa kutumia dawa ili kukusaidia kupunguza maumivu.

Kwa kawaida opioid hutibu maumivu kiasi hadi maumivu makali ya saratani au majeraha kama vile kuvunjika mfupa. Zinaweza kuwa na madhara makubwa, hivyo daktari wako anaweza kujaribu dawa zingine kwanza. Iwapo daktari wako akuagiza utumie opioid, daktari wako atakuchunguza kila mara ili kuhakikisha kuwa unazitumia kwa usalama. Kwa kawaida opioid huwa hazifanyi kazi kwa muda mrefu.