Muhtasari wa Maumivu

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Maumivu ni hisia zisizofurahisha ambazo huambia mwili wako kwamba unaweza kuwa umejeruhiwa.

Je, nini husababisha maumivu?

Majeraha, kama vile kukatwa, kuungua, kuvunjika, kutenguka, na kuvilia damu, huchochea vipokezi vya maumivu vinavyozunguka jeraha.

  • Vipokezi vya maumivu vinapatikana kwenye ncha za nyuzi za neva ndefu

  • Nyuzi husafarisha maumivu hadi kwenye uti wa mgongo wako

  • Neva zingine kwenye uti wa mgongo wako husafirisha ishara za maumivu hadi kwenye ubongo wako

  • Unahisi maumivu pale tu ubongo wako unapochakata ishara za maumivu

Wakati mwingine neva zako hutuma ishara za maumivu hata kama hujaumia au kupata jeraha. Hii inaweza kutokea ikiwa neva zako zimeharibiwa na ugonjwa kama vile kisukari (unaitwa ugonjwa wa neva utokanao na kisukari), au wakati neva zako zinapopondwa au kukatwa na jeraha. Maumivu yanayosababishwa na uharibifu wa neva huitwa ugonjwa wa neva.

Maumivu yanayorejelewa ni wakati maumivu kutoka sehemu moja ya mwili wako unapoyahisi katika sehemu tofauti. Kwa mfano, maumivu yatokanayo na shambulio la moyo kwa kawaida huyahisi kwenye kifua chako, kwa sababu hapo ndipo ulipo moyo wako. Lakini wakati mwingine shambulizi la moyo husababisha maumivu kwenye shingo, taya au mkono wako wa kushoto kwa sababu ishara kutoka sehemu hizo husafiri kwenye neva ambazo zinakaribiana na neva zinazotoka kwenye moyo wako.

Wasiwasi, unyongofu, au matatizo ya usingizi yanaweza kufanya maumivu kuwa makali zaidi kuliko kawaida.

Je, madaktari hutibu vipi maumivu?

Madaktari watatibu tatizo ambalo linasababisha maumivu yako. Kwa mfano, ukiwa na mfupa ambao umevunjika, wataurudisha mahali pake na kuufunga bandeji.

Pia wanaweza kukupatia dawa ya kuzuia maumivu. Aina mbalimbali za dawa hufanya kazi kweye sehemu mbalimbali za njia za maumivu:

  • Malai na jeli za ganzi (unusukaputi) huenda kwenye ngozi yako ili kuzuia vipokezi vya maumivu

  • Sindano za ganzi kwenye ngozi yako au kwenye neva kuu huzuia ishara za maumivu kwenye neva hizo

  • Sindano za maumivu karibu na uti wako wa mgongo (kama vile kuchoma sindano katika uti wa mgongo wakati wa kujifungua) huzuia ishara za maumivu kwenye uti wa mgongo wako

  • Dawa za maumivu za kumeza au sindano (dawa za kuzuia hali ya kusikia maumivu) huathiri ishara za maumivu katika mwili wako wote

Kwa maumivu ya neva, wakati mwingine madaktari hukufanya utumie dawa za kuzuia mfadhaiko au dawa za kuzuia kifafa. Dawa hizi huathiri ishara za neva kwa njia ambayo huondoa maumivu hata kama huna mfadhaiko au kifafa.

Je, ni matibabu gani ya maumivu ambayo hayahusishi dawa?

Baadhi ya matibabu ya maumivu hayahusishi dawa.

  • Kichocheo cha umeme kwenye ngozi (TENS) huweka mkondo wa umeme kwa ngozi yako kupitia pedi ndogo inayonata. Mkondo husisimua lakini hauleti hisia ya mshtuko. Hauondoi maumivu, lakini unaweza kuwasaidia baadhi ya watu.

  • Madaktari wanaweza kuweka pia kichocheo cha umeme kwenye uti wa mgongo wako. Hupandikiza elektrodi ya waya ndogo karibu na uti wa mgongo wako na kutuma ishara ambazo huingilia ishara za maumivu.

  • Katika tiba vitobo, waeledi wa tiba huweka sindano ndogo katika maeneo fulani ya mwili na kuziondoa baada ya dakika chache. Wanaweza kuweka mkondo mdogo wa umeme kwenye sindano hizo. Sindano hizi zinaonekana kusaidia kupunguza maumivu, ingawa madaktari hawana uhakika kwa nini.

  • Mbinu maalum za akili kama vile mrejesho wa kibayolojia, mafunzo ya ulegezaji, mbinu za kupumua, na hiponozi zinaweza kukusaidia kuhimili maumivu.

Je, opioid ni nini?

Opioid ni dawa kali sana za maumivu. Zinaitwa opioid kwa sababu kwanza zilitoka kwenye mpopi ya afyuni. Baadhi ya opioid bado hutoka kwa mimea, lakini nyingi hutengenezwa katika maabara. Kuna opioidi nyingi tofauti, zikiwemo afyuni, oksikodoni, fentanyl, na kodeini.

Opioid ni nzuri kwa kupunguza maumivu makali, kama vile ya kuungua, mfupa uliovunjika, au saratani. Lakini opioid zinaweza kuwa na madhara makubwa hivyo madaktari hujaribu kutozitumia kwa matatizo madogo sana.

Je, opioid zina madhara gani?

Opioids hukufanya upate usingizi na utulivu. Ikiwa utatumia kiasi kikubwa unaweza:

  • Kuchanganyikiwa sana

  • Kuzirai

  • Kuacha kupumua na kuaga dunia

Watu wengi wanakufa kila mwaka kutokana na kuzidisha kipimo cha opioid kwa bahati mbaya.

Madhara mengine ya kawaida ya opioid ni pamoja na:

  • Kichefuchefu (kuhisi kutapika)

  • Kufunga choo (kuacha kujisaidia)

  • Kuwasha

Je, ninaweza kupata uraibu wa opioid?

Opioid hukufanya ujisikie vizuri. Mara unapoanza kutumia opioid, inaweza kukuwia ngumu kuacha. Hali hiyo inaweza kusababisha ugonjwa wa matumizi ya vilevi. Sababu mojawapo inayofanya iwe vigumu kuacha ni kwamba unapata dalili za kuacha dawa za kulevya.

Arosto ya opioid inaweza kutokea hata ikiwa umetumia opioid kwa muda wa chini ya wiki moja. Arosto huwa mbaya zaidi kwa kadiri unavyotumia dawa. Dalili za arosto ya opioid ni pamoja na:

  • Kuwa na wasiwasi na kutetemeka

  • Pua zinazotoa makamasi na macho yaliyojaa machozi

  • Kupiga miayo na kuvuja jasho

  • Kukakamaa kwa tumbo na kutapika

Kwa bahati nzuri, arosto ya opioid haiwezi kukuua.

Ili kupunguza uwezekano wako wa kupata uraibu, madaktari:

  • Hutumia opioid kwa maumivu ambayo hayawezi kudhibitiwa na matibabu mengine

  • Uagiza matumizi ya opioid kwa kipindi kifupi kwa kadiri iwezekanavyo

Je, dawa za kupunguza uvimbe zisizo na asteroidi (NSAIDs) ni nini?

NSAID ni dawa za maumivu kama vile aspirini na ibuprofen. Si opioid. Hupunguza maumivu na kuzuia kuvimba, kama vile viungo vilivyovimba kwa sababu ya ugonjwa wa baridi yabisi. Japokuwa hazina nguvu kama opioid, ni zenye ufanisi.

Je, NSAID zina madhara gani?

Tofauti na opioids, NSAID hazikufanyi upate usingizi au kuacha kupumua. Hata hivyo, NSAID zinaweza:

  • Kuvuruga tumbo lako na kusababisha maumivu

  • Kuongeza hatari ya kuvuja damu, kama vile kwenye tumbo lako au ubongo wako

  • Kusababisha uhifadhi wa majimaji na matatizo ya figo

  • Baadhi ya NSAID huongeza hatari ya shambulizi la moyo na kiharusi

Je, ni dawa gani nyingine za maumivu?

Asitamainofeni (Tylenol) ni dawa ya maumivu ambayo ni maarufu. Sio opioid na ni sawa na NSAID, lakini haivurugi tumbo lako au kuongeza hatari ya kuvuja damu. Hata hivyo, kiasi kikubwa cha asitamainofeni kinaweza kuharibu ini lako.