Je, misuli ni nini?
Misuli ni tishu ambazo hukaza ili kusogeza viungo vya mwili wako. Una aina mbalimbali ya misuli:
misuli ya kiunzi cha mifupa
Misuli laini
Misuli ya moyo
Misuli ya kiunzi cha mifupa imeunganishwa kwenye mifupa na huwa katika jozi—kwa mfano, misuli ya mbele ya mikono hukunja viwiko vyako, na misuli ya nyumba ya mkono huvinyoosha. Misuli ya kiunzi cha mifupa ni ya hiari (maana yake huisogeza pale unapotaka).
Misuli laini huzunguka ateri, vena na utumbo wako. Misuli laini ya kwenye mishipa yako ya damu hukaza na kulegea ili kurekebisha mtiririko wa damu. Mishipa laini iliyo ndani ya utumbo wako hukaza ili kupitisha chakula na kinyesi katika mfumo wako wa umeng'enyaji wa chakula. Huwezi kudhibiti misuli yako laini. Hufanya kazi yake pasipo wewe kufikiria.
Msuli wa moyo ni aina maalum ya misuli ambayo kamwe haitaji kusimama kwa ajili ya kupumzika, na haiko chini ya udhibiti wako wa hiari.
Je, misuli hufanyaje kazi?
Misuli huzalisha nishati kutoka kwenye chakula na oksijeni ambavyo huletwa kupitia mtiririko wa damu. Misuli hutumia nishati hii kukaza (kusinyaa). Kadiri misuli inavyokuwa mikubwa na ndivyo inavyosambaza damu nyingi zaidi, na ndivyo inavyoweza kukaza kwa nguvu zaidi.
Misuli inaweza kuvuta tu, haiwezi kusukuma
Bila usambazaji mzuri wa damu, misuli yako haiwezi kufanya kazi nyingi.
Aina fulani ya mazoezi, kwa mfano, kunyanyua vitu vizito, yanaweza kufanya misuli yako kuwa mikubwa na thabiti. Aina nyingine ya mazoezi, kama vile kukimbia, inaweza kuifanya misuli yako iwe na ustahimilivu zaidi (iweze kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi).
Je, misuli inawezaje kufanya mwili wako usogee?
Ili kuufanya mwili wako usogee, misuli lazima iunganishe mfupa mmoja na mfupa mwingine kupitia kiungo.
Misuli imeunganishwa na mifupa kwa kamba nene za tishu zinazoitwa tendoni
Misuli inapokaza, tendoni huvuta mifupa yote na kuisogeza kwenye uelekeo ambao kiungo kinaruhusu. Kwa sababu misuli inaweza tu kukaza, iwapo msuli mmoja utafanya kiungo kipinde, utapaswa kukaza msuli mwingine wa upande wa pili wa kiungo ili kukinyoosha.
Je, misuli inaweza kupata matatizo gani?
Matatizo ya misuli ni pamoja na:
Majeraha (kuchanika na kuteguka)
Kuvimba (kuvimba misuli)
Tendoni zinaweza kuvimba pia (tatizo linaloitwa tendinitis).