Uchungu wa uzazi ni nini?
Uchungu wa uzazi ni hatua ya kwanza ya kujifungua. Wakati wa uchungu wa uzazi misuli ya tumbo lako la uzazi (uterasi) inabana tena na tena ili kumsukuma mtoto wako nje. Mikazo hii huitwa uchungu wa kuzaa. Mikazo huacha na kuanza yenyewe. Huna udhibiti wowote juu yenyewe. Inakuwa na nguvu kadiri uchungu wa uzazi unavyoendelea.
Kujifungua ni hatua ya pili ya uzazi, mtoto anapopita katika njia yako ya uzazi na kutoka.
Kwa kawaida utapata uchungu wa uzazi wakati wowote kuanzia wiki 2 kabla hadi wiki 2 baada ya tarehe yako ya kujifungua
Kwa kawaida uchungu wa uzazi unapoanza huwa kama vile maumivu ya mgongo au kama maumivu ya hedhi ambayo huendelea kuwa makali zaidi na kukaribiana kadiri muda unavyopita.
Kwa kawaida uchungu wa uzazi huchukua saa 12 hadi 18 katika ujauzito wako wa kwanza na karibu nusu yake kwa ujauzito unaofuata
Wakati wa uchungu wa uzazi, madaktari na wauguzi hukukagua mara kwa mara ili kutafuta matatizo
Dawa au mazoezi maalum ya kupumzika yanaweza kukusaidia kukabiliana na uchungu wa kujifungua
Ni wakati wa kwenda hospitali (au kituo cha kujifungua) moja ya yafuatayo yanapotokea:
Maji yako yanapasuka
Mikazo yako hudumu kwa sekunde 30 au zaidi na hutokea baada ya dakika 6
Ni nini hufanyika wakati wa uchungu wa uzazi?
Mlango wako wa kizazi ni sehemu ya chini ya uterasi yako ambapo inaunganishwa na uke wako. Mlango wa kizazi una mwanya mdogo ambao hubaki ukiwa umefungwa kabisa unapokuwa mjamzito. Wakati wa uchungu wa uzazi, mikazo yako polepole huvuta mlango wa kizazi na kuufungua hadi upanuke vya kutosha kwa mtoto wako kutoka.
Uchungu wa uzazi una sehemu 2:
Uchungu wa uzazi wa mapema
Uchungu wa uzazi unaoendelea
Wakati wa uchungu wa uzazi wa mapema:
Shingi yako ya kizazi huanza kuwa nyembamba na kufunguka takriban inchi 1 hadi 2 (sentimita 2 hadi 5)
Mikazo huja na kuondoka na kupata nguvu na kugawanyika kwa usawa zaidi
Maumivu haya siyo mabaya sana
Wakati wa uchungu wa uzazi unaoendelea:
Mlango wako wa kizazi hufunguka kikamilifu, takriban inchi 4 (sentimita 10) na kubana kabisa.
Mtoto wako anashuka (husogea chini kwenye fupanyonga lako na kuwa tayari kuingia kwenye njia ya uzazi)
Unaanza kujisikia kama unahitaji kusukuma mtoto nje
Maumivu ni makali zaidi
kupasuka kwa chupa yako ya uzazi ni wakati mfuko wa amnioti hupasuka na kiowevu cha amnioti kutoka kwenye uke wako. Hii inaweza kutokea kabla ya kuanza kwa uchungu wa uzazi au wakati wa uchungu wa uzazi.
Huwezi kujifungua mtoto wako hadi shingo yako ya uzazi iwe wazi kabisa na maji yako yamepasuka.
Nitajuaje uchungu wa zazazi utakapoanza?
Dalili kuu za uchungu wa uzazi ni:
Mikazo, ambayo unaweza kuhisi kama maumivu ya hedhi ambayo huja na kuondoka kwa vipindi vya kawaida
Maumivu ya mgongo
Kabla ya mikazo au maumivu ya mgongo, dalili za mapema kwamba uchungu wa uzazi uko karibu kuanza ni pamoja na:
Onyesho la damu (kiasi kidogo cha damu na kamasi inayotoka kwenye uke wako mwanzoni mwa uchungu wa uzazi)
"Kupasuka kwa chupa yako ya uzazi"
Maji yako yakipasuka, unapaswa kumwita daktari wako au mkunga mara moja. Kwa kawaida, uchungu wa uzazi huanza ndani ya saa 24. Walakini, ikiwa hautaanza ndani ya saa kadhaa, daktari wako au mkunga anaweza kuanza uchungu wa uzazi na dawa.
Ikiwa maji yako yatapasuka zaidi ya wiki 6 kabla ya tarehe yako ya kujifungua, daktari wako anaweza kukupa dawa ya kusitisha uchungu wa uzazi. Hii inamruhusu mtoto kukua kidogo kabla ya kuzaliwa.
Je, ninapaswa kwenda hospitalini au kituo cha kujifungulia lini?
Unapaswa kwenda hospitalini au kituo cha kujifungua wakati mojawapo ya yafuatayo yanapotokea:
Maji yako yanapasuka
Mikazo yako hudumu kwa sekunde 30 au zaidi na hutokea baada ya dakika 6
Daktari au mkunga ataangalia ili kuona kama umeanza kupata uchungu wa uzazi. Karibu na tarehe yao ya kujifungua, baadhi ya wanawake hupata mikakamao inayofanana na uchungu wa uzazi lakini si uchungu wa uzazi. Ikiwa bado hujapata uchungu wa uzazi, utarudishwa nyumbani.
Ikiwa umepata uchungu wa uzazi, daktari wako:
Ataangalia uke wako kuona kama chupa ya maji yako ya uzazi imepasuka na, ikiwa imepasuka, ataangalia rangi ya umajimaji
Gusa shingo yako ya uzazi ili kuona jinsi ilivyo wazi
Gusa tumbo lako ili kuona mtoto yuko katika nafasi gani
Weka IV kwenye mshipa wa mkono ili kukusaidia kukupa dawa na viowevu katika kipindi cha uchungu wa uzazi
Ikiwa ulijifungua mtoto hapo awali na ilikuwa haraka (ilichukua chini ya saa 6), unapaswa kumjulisha daktari wako mara tu unapofikiri kwamba uchungu wa uzazi umeanza. Una uwezekano wa kujifungua haraka kwa sababu kila kipindi cha uchungu wa uzazi huwa ni kifupi kuliko kilichotangulia.
Madaktari humchunguzaje mtoto wakati wa uchungu wa uzazi?
Wakati wa uchungu wa uzazi, jambo kuu ambalo huwaelewesha madaktari jinsi mtoto alivyo ni:
Kipimo cha mapigo ya moyo cha mtoto
Madaktari wanaweza kuangalia mapigo ya moyo wa mtoto kwa kutumia:
Stetoskopu
Kifaa cha kupiga picha kilichowekwa kwenye tumbo lako
Kichunguzi cha kielektroniki cha kufuatilia wa moyo wa fetasi kilichowekwa ndani ya uke wako ili kurekodi kwa mfululizo mapigo ya moyo ya mtoto wako
Ikiwa mapigo ya moyo wa mtoto wako ni ya haraka sana au ya polepole sana, mtoto wako anaweza kuwa na matatizo. Madaktari wako wanaweza kupiga picha za ndani za mtoto.
Madaktari hutibuje uchungu wa uzazi?
Kiwango cha maumivu wakati wa kipindi cha uchungu wa uzazi hutofautiana. Wanawake wengine wanahitaji msaada zaidi wa maumivu kuliko wengine wakati wa kipindi cha uchungu wa uzazi. Kuhudhuria madarasa ya kujifungua wakati wa ujauzito na kukaa na mtu wa kukusaidia kunaweza kukusaidia kujisikia vizuri zaidi wakati wa kipindi cha uchungu wa uzazi na kunaweza kupunguza hitaji lako la dawa za maumivu.
Wakati wa ujauzito, utazungumza na daktari wako au mkunga kuhusu aina gani ya dawa za maumivu unazotaka. Dawa za maumivu wakati wa uchungu wa uzazi ni pamoja na:
Dawa za maumivu za opioid IV, kama vile morphine au fentanyl, ambazo hukufanya ustarehe zaidi lakini zinaweza kumfanya mtoto wako apumue polepole sana ikiwa utapata dawa karibu sana na wakati mtoto anazaliwa
Kinga ya epidural, ambayo ni sindano ya dawa ya kufa ganzi (anesthetic ya ndani) au dawa ya maumivu kwenye mgongo wako wa chini ya kua ganzi neva zinazo zunguka uti wa mgongo wako
Kizuizi cha neva, ambapo madaktari hudunga dawa ya kufa ganzi ndani ya uke wako ili kuzuia ishara za maumivu kutoka kwa neva kuu
Kutia nusukaputi ya ndani, sindano za dawa ya kufanya eneo la nje la uke liwe bila maumivu muda mfupi kabla ya mtoto kuzaliwa
Kuzaa mtoto kwa njia ya kawaida hutumia mbinu za kupumzika na kupumua badala ya dawa ili kudhibiti maumivu ya kipindi cha uchungu wa uzazi na kupunguza hitaji lako la dawa za maumivu. Baadhi ya wanawake wanaojifungua kwa njia ya kawaida hawatumii dawa yoyote ya maumivu. Ili kujiandaa, wewe na mtu wa kukusaidia kwa kawaida huchukua madarasa ya uzazi kwa wiki kadhaa ili kujifunza kuhusu uchungu wa uzazi na jinsi ya kupumua na kupumzika.