Je, maumivu ya hedhi ni nini?
Maumivu ya hedhi ni maumivu kwenye sehemu ya chini ya tumbo ambayo hutokea siku chache kabla, wakati, au baada ya kipindi chako cha hedhi.
Maumivu yako yanaweza kuwa ya ghafla au makali
Maumivu yanaweza kuanzia sehemu ya chini tumbo hadi sehemu ya chini ya mgongo na chini hadi sehemu ya nyuma ya miguu yako
Kupata usingizi wa kutosha, kufanya mazoezi, na kutumia NSAID (dawa za kupunguza maumivu zisizo za steroidi), kama vile ibuprofeni, kunaweza kusaidia kupunguza maumivu yako
Kuna aina 2 za maumivu ya hedhi:
Ya kawaida
Yasiyo ya kawaida
Maumivu ya kawaida ya hedhi ndiyo aina ya kawaida zaidi. Maumivu kama haya:
Kwa kawaida huanza ukiwa kijana
Mara nyingi hurithiwa katika familia
Kawaida hupungua unapokua au baada ya kupata mtoto
Maumivu ya hedhi yasiyo ya kawaida:
Husababishwa na tatizo lingine la kiafya, kama vile fibroidi
Kwa kawaida huanza ukiwa mtu mzima
Je, ni nini husababisha maumivu ya hedhi?
Maumivu ya kawaida ya hedhi yanaweza kusababishwa na:
Viwango vya juu vya prostaglandini
Prostaglandini ni kemikali ambazo mwili wako hutengeneza. Hufanya uterasi yako kukazika, na miisho ya nyuzi za neva zako kuhisi uchungu zaidi.
Maumivu yasiyo ya kawaida ya hedhi mara nyingi husababishwa na matatizo ya kiafya yanayoathiri uterasi yako kama vile:
Endometriosisi: tishu (endometriamu) ambayo kwa kawaida huwa ndani ya uterasi yako hukua nje ya uterasi yako
Fibroidi: uvimbe (ambao si saratani) kwenye uterasi yako
Adenomiosisi: tishu kwenye utando wa uterasi yako hukua hadi kwenye ukuta wa uterasi yako, na hivyo kuifanya kuwa kubwa na kuvimba wakati wa hedhi
Je, dalili za maumivu ya hedhi ni zipi?
Dalili kuu ni:
Maumivu ya ghafla au makali kwenye sehemu ya chini ya tumbo lako—maumivu yanaweza kuja na kupotea, au kuwa na maumivu makali ya mara kwa mara
Huenda pia:
Maumivu ya kichwa
Kuhisi mgonjwa kwenye tumbo lako au kutapika
Kufunga choo
Kuhara (kinyesi cha maji, mara kwa mara)
Kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na dalili kali ikiwa:
Hedhi yako ilianza ukiwa na umri mdogo
Unavuja damu kwa wingi kwa muda mrefu wakati wa hedhi
Unavuta sigara
Una wanafamilia walio na maumivu makali ya hedhi
Je, ni wakati gani ninapaswa kwenda kwa daktari kwa maumivu ya hedhi?
Maumivu ya hedhi hayapendezi lakini si hatari. Hata hivyo, matatizo makubwa zaidi ya afya wakati mwingine husababisha maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo.
Nenda kwa daktari leo ikiwa una maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo na mojawapo ya haya:
Maumivu makali ambayo yalianza ghafla
Maumivu ya mara kwa mara
Maumivu ambayo yanazidi unapogusa tumbo lako au unapotembea
Homa au mzizimo
Kutokwa na uchafu mwingi, mweupe au wa manjano (majimaji) kutoka kwenye uke wako
Nenda kwa daktari ndani ya siku chache ikiwa una maumivu ya hedhi ambayo ni mabaya kuliko kawaida au yanayodumu kwa muda mrefu kuliko kawaida. Ikiwa huna maumivu yoyote yaliyo hapo juu, pigia simu daktari wako wakati unaweza.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina maumivu ya hedhi?
Madaktari watashuku maumivu ya hedhi kulingana na dalili zako na uchunguzi. Ili kuhakikisha kuwa hakuna sababu nyingine ya dalili zako, wanaweza kufanya kipimo kimoja au zaidi:
Kupima ujauzito
Kipimo cha picha kinachotumia mawimbi ya sauti katika sehumu ya chini ya tumbo lako ili kuchunguza ovari zako, uterasi, na mlango wa kizazi
Ikiwa daktari wako anafikiri kuwa unaweza kuwa na ugonjwa wa uvimbe kwenye fupanyonga, atachukua sampuli kutoka kwenye mlango wa kizazi kwa usufi wa pamba na kuipima ili kubaini ikiwa ina maambukizi
Kwa nadra sana, daktari wako anaweza kuhitaji kufanya vipimo vya picha, kama vile MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku), au kwa kutumia bomba la kuangalia (histeroskopia) kutazama ndani ya uterasi yako.
Je, madaktari hutibuje maumivu ya hedhi?
Ikiwa una maumivu ya hedhi ya kawaida, madaktari watapendekeza njia za kupunguza maumivu yako:
Kupata usingizi wa kutosha
Mazoezi
Weka pedi ya kupasha joto kwenye sehemu ya chini ya tumo lako
Tumia NSAID (dawa za kupunguza maumivu zisizo za steroidi), kama vile ibuprofeni siku moja au 2 kabla ya kuanza kwa kipindi chako cha hedhi na siku 2 za kwanza za kipindi chako cha hedhi
Ikiwa ungali na maumivu, madaktari wanaweza:
Kukupa dawa za kuzuia mimba—dawa hizi huzuia ovari zako kutoa yai
Kukupa matibabu mengine ya homoni
Kujaribu dawa za maumivu ya neva kama vile gabapentini
Kupendekeza matibabu mbadala kama vile kudunga ngozi na sindano nyembamba
Ikiwa maumivu yako ni makali sana hata kwa matibabu, madaktari wanaweza:
Kufanya upasuaji ili kukata neva zinazotuma ishara za maumivu kutoka kwa uterasi hadi kwa ubongo wako
Ikiwa una maumivu ya hedhi yasiyo ya kawaida, madaktari watatibu tatizo la kiafya linalosababisha maumivu yako.