Uhifadhi wa mkojo ni nini?
Uhifadhi wa mkojo ni pale ambapo:
Huwezi kukojoa kabisa au unakojoa kidogo
Huwezi kukojoa lakini bado kuna mkojo kwenye kibofu chako cha mkojo baada ya kumaliza kukojoa
Ukiwa na hali ya kuhifadhi mkojo:
Pia unaweza kuvujisha mkojo na kukojoa pasipo kukusudia (kutoweza kujizuia kukojoa)
Madaktari watafanya kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti baada ya wewe kukojoa ili kuona kiasi cha mkojo kilichobaki kwenye kibofu
Madaktari wanaweza kutumia katheta (bomba jembamba linaloweza kujipinda) ili kuondoa mkojo wote kwenye kibofu chako cha mkojo
Je, nini husababisha uhifadhi wa mkojo?
Husababishwa na:
Shida kwenye misuli ya kibofu chako cha mkojo
Kitu kinachoziba uwazi wa kibofu chako cha mkojo, kama vile jiwe kwenye figo au tezi dume iliyotanuka
Tatizo kubwa la kufunga choo (mkusanyiko wa kinyesi)
Matatizo ya neva kwenye kibofu chako cha mkojo (haya yanaweza kuwapata watu wenye matatizo ya kiafya kama vile kisukari au ugonjwa wa Parkinson)
Dawa fulani
Uhifadhi wa mkojo huwapata zaidi wanaume kwa sababu ukuaji wa tezi dume unaweza kuzuia mtiririko wa mkojo.
Zipi ni dalili za uhifadhi wa mkojo?
Ikiwa huwezi kuondoa mkojo wote kwenye kibofu chako cha mkojo:
Kutatizika kuanza kukojoa
Mkondo dhaifu wa mkojo
Hisia za kwamba kuna mkojo uliobaki kwenye kibofu chako cha mkojo
Wakati mwingine kuvuja kwa mkojo, kukojoa usiku, au kuhitaji kukojoa mara kwa mara
Ikiwa huwezi kukojoa kabisa:
Huna uwezo wa kuanza kukojoa
Maumivu kwenye kibofu chako cha mkojo pale kinapotanuka
Kuvimba kwenye sehemu ya chini ya tumbo lako
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina tatizo la uhifadhi wa mkojo?
Ikiwa huwezi kukojoa kabisa, madaktari watajua kuwa una tatizo la uhifadhi wa mkojo. Ikiwa una uwezo wa kukojoa kiasi kidogo cha mkojo, madaktari watafanya kipimo ili kuona ni kiasi gani cha mkojo kinabaki kwenye kibofu chako cha mkojo.
Madaktari watakufanya ukojoe kwa kadiri unavyoweza
Watafanya kipimo cha upigaji picha kwa mawimbi ya sauti kwa kibofu chako cha mkojo au wataweka katheta kwenye kibofu chako cha mkojo ili kuona kama kuna mkojo uliobaki kwenye kibofu chako cha mkojo
Ikiwa kiasi cha mkojo kilichosalia ni zaidi ya nusu kikombe, madaktari watajua kuwa una tatizo la uhifadhi wa mkojo
Pia madaktari watafanya vipimo vifuatavyo:
Kwa kawaida, uchunguzi wa rektamu—daktari kuhisi hali ya ndani ya tundu lako la haja kubwa kwa kuingiza kidole ili kuona kama kumezibwa na kinyesi au, kama wewe ni mwanaume, ili kuona kama una tezi dume zilizotanuka
Kipimo cha mkojo
Vipimo vya damu
Je, mdaktari hutibu vipi uhifadhi wa mkojo?
Ikiwa huwezi kukojoa kabisa, madaktari wataingiza katheta kwenye kibofu chako cha mkojo mara moja ili kutoa mkojo. Ili kutibu chanzo cha uhifadhi wa mkojo, madaktari wanaweza:
Kukuzuia kutumia dawa zozote ambazo zinaweza kuwa zimesababisha tatizo hilo
Ikiwa wewe ni mwanaume mwenye tezi dume zilizotanuka, watazitibu kwa upasuaji au kwa dawa
Kukuagiza dawa za kutuliza misuli iliyo kwenye mlango wa kibofu chako cha mkojo
Ikiwa una tatizo la neva, watakufanya uweke katheta kwenye kibofu chako cha mkojo mara kadhaa kwa siku ili kutoa mkojo
Wakati mwingine, kufanya upasuaji wa kuondoa mkojo mwilini mwako kwa njia nyingine