Kushindwa Kujizuia Kukojoa kwa Watu Wazima

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2024

Kutoweza kujizuia kukojoa ni nini?

Kutoweza kujizuia kukojoa ni hali ya kukojoa pasipo kukusudia.

  • Kutoweza kujizuia kukojoa kunaweza kuhusisha kutiririka kwa mkojo kidogo au kuvujisha mkojo mwingi

  • Unaweza kuwa na hali ya kutoweza kujizuia kukojoa wakati wote, usiku tu, au pale unapokohoa au kupiga chafya

  • Kutoweza kujizuia kukojoa ni hali inayowapata sana watu wazima, hasa wanawake wazee, lakini si sehemu ya kawaida ya kuzeeka

Ni wakati gani ninapopaswa kumwona daktari kuhusiana na hali ya kutoweza kujizuia kukojoa?

Onana na daktari mara moja ikiwa una halil ya kutoweza kujizuia kukojoa na ishara hizi za onyo za uharibifu wa mgongo, kama vile:

  • Udhaifu katika miguu yako

  • Kupoteza hisia kwenye miguu yako au sehemu inayozunguka sehemu zako za siri au tundu la haja kubwa

Ikiwa una hali ya kutoweza kujizuia kukojoa pasipo ishara hizi za onyo, mpigie simu daktari wako. Daktari wako ataamua ni mapema kiasi gani anapaswa kuonana nawe kwa kutegemea dalili zako nyingine.

Watu wengine huwa wanaona aibu kuzungumza na daktari wao kuhusu hali ya kutoweza kujizuia kukojoa au huwa wanahisi ni sehemu ya kawaida ya kuzeeka. Hii si kweli. Unapaswa kuonana na daktari ikiwa hali yako ya kutoweza kujizuia kukojoa inakupa wasiwasi, inakuzuia kufanya shughuli zako za kila siku, au kukufanya ujiepushe na shughuli za kijamii.

Je, nini husababisha hali ya kutoweza kujizuia kukojoa kwa watu wazima?

Sababu za kutoweza kujizuia kukojoa ni pamoja na:

  • Udhaifu kwenye misuli inayoshikilia mkojo kwenye kibofu chako cha mkojo—hili linaweza kuwapata wanawake baada ya kujifungua au wanaume baada ya upasuaji wa saratani ya tezi dume

  • Kizuizi kwenye kibofu cha mkojo, kama vile jiwe kwenye figo au tezi dume iliyotanuka, ambacho hufanya kibofu chako cha mkojo kubaki kimejaa hadi mkojo kumwagika

  • Mikazo ya ghafla ya misuli kwenye kibofu chako cha mkojo

  • Tatizo la neva ambazo hudhibiti kibofu chako cha mkojo (kibofu cha mkojo chenye nyurojeniki)

Wakati mwingine watu hupata tu hali ya kutoweza kujizuia kukojoa kwa sababu wana tatizo linalowafanya washindwe kufika chooni. Watu ambao wamewahi kupata kiharusi au tatizo la akili wanaweza kupata shida ya kufika bafuni wao wenyewe.

Kunywa vimiminiko vingi au kutumia vidonge vya maji (viongeza mkojo) peke yake haviwezi kusababisha hali ya kutoweza kujizuia kukojoa. Lakini inaweza kufanya hali ya kutoweza kujizuia kukojoa kuwa mbaya zaidi ikiwa tayari una tatizo hilo.

Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?

Madaktari watakuuliza kuhusu dalili zako na kukupima (kwa wanawake, watajaribu kupima fupanyonga). Watakuuliza kuhusu dawa yoyote ambayo unaitumia. Wanaweza kukuomba uweke kumbukumbu ya kukojoa kwako kwa kipindi cha siku moja au 2.

Pia madaktari wanaweza kufanya vipimo kama vile:

  • Kipimo cha mkojo au damu

  • Kupima ni kiasi gani cha maji wanachoweza kuweka kwenye kibofu chako cha mkojo kupitia bomba dogo kabla hujapata haja ya kukojoa (sistometri)

  • Kukufanya ukojoe kwenye kifaa maalum ambacho hupima kasi na kiasi gani cha mkojo hutoka (kiwango cha juu cha mtiririko wa mkojo)

  • Kupima shinikizo la kibofu cha mkojo wakati kibofu cha mkojo kimejazwa kwa viwango tofauti vya maji (sistometri)

Je, madaktari hutibu vipi hali ya kutoweza kujizuia kukojoa kw watu wazima?

Madaktari watatibu chanzo maalum cha kutoweza kujizuia kukojoa. Ikiwa dawa unayotumia inasababisha kutoweza kujizuia kukojoa, madaktari wanaweza kujaribu kukubadilishia dawa.

Kwa chanzo chochote cha hali ya kutoweza kujizuia kukojoa, inaweza kusaidia kwa:

  • Kuweka kikomo cha kunywa vitu vya majimaji wakati wa kulala na epuka matumizi kafeini

  • Kufunza kibofu chako cha mkojo kufuata ratiba ya kukojoa isiyobadilika

  • Kufanya mazoezi ya kigeli ili kuimarisha misuli yako ya fupanyonga (kubana kwa nguvu na kulegeza misuli inayoanzisha na kusitisha kukojoa)

Matibabu mengine ni pamoja na:

  • Dawa

  • Malai ya estrojeni kwa wanawake

  • Kuchangamsha kwa umeme

  • Wakati mwingine upasuaji, katheta, au vifaa vingine