Ni nini maana ya jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusishwa na spoti?
Mshtuko wa ubongo ni jeraha kwenye ubongo wako ambalo huathiri kwa muda mawazo na ufahamu wako. Huenda ukazimia (kupoteza fahamu) au huenda ukawa umechanganyikiwa tu.
Mfupa wa fuvu hulinda ubongo wako. Kiowevu kwenye fuvu lako pia hulinda ubongo wako. Hata hivyo, kichwa chako kikigongwa kwa kiasi cha kutosha, ubongo wako unaweza kusogea ndani ya fuvu la kichwa na kugongana na fuvu lako. Hii inaweza kuumiza ubongo wako na kubadilisha kwa muda jinsi ubongo wako unavyofanya kazi.
Jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusishwa na spoti ni jeraha la ubongo unalolipata wakati wa mchezo, kama vile kugongwa kichwa unapocheza soka.
Takribani mchezaji 1 kati ya 5 wanaocheza michezo ya kugusana hupata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa kila msimu.
jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linaweza kutokea katika mchezo wowote lakini hutokea zaidi katika michezo iliyo na migongano ya kasi ya juu kama vile kandanda, raga, hoki ya kwenye barafu na lakrosi
Ukipata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusiana na spoti, unaweza kupoteza fahamu au ukakosa kupoteza fahamu
Ukipata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusisha spoti na ukaendelea kucheza spoti, uko katika hatari kubwa ya kupata jeraha lingine la ubongo.
Majeraha ya ubongo ya kujirudia yanayotokana na kupigwa/kugongwa yanaweza kusababishwa na majeraha madogo ya kichwa
Mishtuko ya ubongo inayojirudia inaweza kuongeza uwezekano wako wa kupata madhara ya kudumu ya ubongo na kupata tatizo la akili
Muone daktari mara moja, hususani daktari ambaye ametibu majeraha mengi ya ubongo yanayotokana na kupigwa/kugongwa yanayohusishwa na spoti, ikiwa unafikiri kuwa una jeraha la ubongo linalohusishwa na spoti.
Ni michezo gani inayoweza kusababisha jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?
Jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa husababishwa na kitu kugonga kichwa chako kwa nguvu sana. Kwenye spoti, hali hii inaweza kutokea wakati:
Kuanguka na kugonga kichwa chako
Kichwa chako kinagongana na mchezaji mwingine
Umegongwa kichwani kwa kifaa kama vile mpira, gongo, au fimbo
Jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linaweza kutokea kwenye takribani mchezo wowote. Hata hivyo, inatokea sana kwenye spoti ambapo watu hugongana wanapokimbia kwa kasi, kama vile soka, ragbi, hoki ya barafuni, au lakrosi. Pia, inaweza kutokea sana kwenye michezo inayohusisha fimbo na matufe au mipira inayotupwa kwa kasi ya juu.
Zipi ni dalili za jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusiana na mchezo?
Unaweza kupoteza fahamu kwa muda mfupi (kwa kawaida kwa chini ya dakika 15). Hata hivyo, si lazima uwe umepoteza fahamu ili upate jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa. Huenda pia:
Kuchanganyikiwa, ikiwemo kutunduwaa au kushtuka, kutokuwa na uhakika kuhusu alama au timu unayochezea, au kujibu maswali polepole
Kupoteza kumbukumbu, kama vile kutojua michezo ya timu au kutokumbuka kilichofanyika kabla na baada ya kujeruhiwa
Kuona vitu viwili viwili, au kuathiriwa na mwangaza
Kuwa goigoi
Maumivu ya kichwa na kuhisi kizunguzungu
Kutokuwa imara
Baadhi ya dalili zinaweza kutokea baada ya siku au wiki chache tungu upate jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa:
Maumivu ya kichwa yanayoendelea
Matatizo ya kumbukumbu yako
Kuhisi uchovu na kuudhika upesi
Kukosa usingizi
Mihemko ya hisia
Kuathiriwa na mwangaza na kelele
Ukipata zaidi ya jeraha moja la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusiana na mchezo, hata kama ni majeraha madogo, unaweza kupata madhara ya kudumu ya ubongo yaitwayo CTE (kiwewe sugu cha ubongo). CTE hutokea miaka kadhaa baadaye. Inasababisha dalili kama vile:
Matatizo ya kumbukumbu
Matatizo ya kutambua mambo yanayofaa na kufanya maamuzi
Mabadiliko kwenye haiba yako, kama vile kukasirika haraka na kuwa na vurugu zaidi
Dalili na ishara zinazofanana na ugonjwa wa Parkinson—tatizo moja au zaidi la kusogeza viungo sawa na yale wanayopata watu wanaougua ugonjwa wa Parkinson, kama vile kutetemeka, kutembea taratibu, matatizo wakati wa kuongea, au misuli iliyokaza
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa linalohusiana na mchezo?
Ikiwa ulipata majeraha ya kichwa ukicheza spoti, daktari atafanya yafuatayo:
Atakuuliza maswali
Atafanya tathmini ya mwili ili kuona iwapo sehemu zote za ubongo wako zinafanya kazi vizuri
Usiporejea katika hali ya kawaida baada ya dakika chache au iwapo ulipoteza fahamu kwa muda mrefu, kwa kawaida daktari atafanya yafuatayo:
Atakutuma hospitalini ukafanyiwe uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) wa kichwa chako ili kuhakikisha kuwa ubongo wako hauvuji damu au haujavilia
Inapendekezwa umwone daktari mwenye uzoefu wa mishtuko ya ubongo inayohusiana na michezo.
Je, madaktari hushughulikia vipi mshtuko wa ubongo unaohusiana na michezo?
Daktari wako atakuomba:
Kupumzika
Umeze asetaminofeni kwa ajili ya maumivu ya kichwa
Uache shughuli zinazoweza kuchangamsha ubongo wako (kwa mfano kutumia kompyuta, kucheza michezo ya video na kutazama runinga)
Urudi hospitalini iwapo dalili zako zitazidi
Kabla ya kurudi uwanjani, huenda daktari wako akakuelekeza uanze kwa mazoezi mepesi na uyafanye polepole. Hupaswi kurudi kucheza kabla ya dalili zako kupotea na daktari wako kukuruhusu.
Ninawezaje kuzuia matukio mengine ya majeraha ya ubongo yanayotokana na kupigwa/kugongwa yanayohusiana na michezo?
Vaa helmeti zozote zinazopendekezwa kwa ajili ya spoti unayoshiriki
Usicheze michezo ya kugusana hadi daktari wako atakaposema kuwa majeraha yako ya kichwa yamepona kabisa
Anza taratibu unaporudi mchezoni
Baadhi ya wanariadha hufanyiwa vipimo vya akili (kupima utendakazi fulani wa ubongo) kabla ya kushiriki michezo. Kwa kufanya hivi, iwapo kunashukiwa kuwa kuna jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa, madaktari wanaweza kumpima mchezaji tena ili kubaini iwapo amepata matatizo ya ubongo.