Jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Ni nini maana ya jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Mshtuko wa ubongo ni jeraha kwenye ubongo wako ambalo huathiri kwa muda mawazo na ufahamu wako.

Mfupa wa fuvu hulinda ubongo wako. Kiowevu kwenye fuvu lako pia hulinda ubongo wako. Hata hivyo, kichwa chako kikigongwa kwa kiasi cha kutosha, ubongo wako unaweza kusogea ndani ya fuvu la kichwa na kugongana na fuvu lako. Hii inaweza kuumiza ubongo wako na kubadilisha kwa muda jinsi ubongo wako unavyofanya kazi.

  • Huenda ukazimia (kupoteza fahamu) au huenda ukawa umechanganyikiwa tu

  • Madaktari hufanya uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta) ili kuhakikisha kuwa ubongo wako hauvuji damu au haujavilia

  • Ukishapata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa, kuna uwezekano kwamba unaweza kupata mishtuko ya ubongo katika siku za usoni, hususan ikiwa ubongo wako haujapona

  • Majeraha ya ubongo ya kujirudia yanayotokana na kupigwa/kugongwa yanaweza kuongeza uwezekano wako wa kupata uharibifu wa kudumu wa ubongo na kupoteza utambuzi

Ni nini husababisha jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa husababishwa na kitu kugonga kichwa chako kwa nguvu sana (majeraha ya kichwa). Hali hii inaweza kutokea wakati, kwa mfano:

  • Kuanguka na kugonga kichwa chako

  • Umejipata kwenye ajali ya gari au pikipiki

  • Umepigwa ngumi au kugongwa kwenye kichwa na kitu

Aina nyingi za spoti huweka watu katika hatari ya kupata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa (tazama Sehemu ya Jeraha la Ubongo Linalohusiana na Spoti la Kupigwa/Kugongwa).

Zipi ni dalili za jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Ikiwa una jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa, unaweza:

  • Kupoteza fahamu kwa muda (kwa kawaida kwa chini ya dakika 15)

  • Kuwa na hisia ya kutunduwaa, kuchanganyikiwa, au kizunguzungu

  • Kujibu maswali polepole

  • Kupata maumivu ya kichwa, kuona vitu viwili viwili, au kuathiriwa na mwangaza

  • Kuwa goigoi au kutokuwa imara

  • Kuwa na tatizo la kukumbuka kilichofanyika punde tu kabla na baada ya kujeruhiwa

Ni nini maana ya ugonjwa wa baada ya jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Ugonjwa wa baada ya jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa ni wakati unapata dalili baada ya kuathiriwa na jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa. Unaweza kuwa na:

  • Maumivu ya kichwa

  • Kizunguzungu na wepesi wa kichwa

  • Kuwa na uchovu, kukasirika haraka, au kuathiriwa na mwangaza au kelele

  • Kutoweza kumakinika

  • Uwezo duni wa kukumbuka

  • Mfadhaiko na wasiwasi

Kwa kawaida dalili hizi hutoweka baada ya wiki moja au mbili. Kwa nadra, dalili hizi zinaweza kudumu kwa miezi kadhaa

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Daktari wako anaweza kujua kuwa umepata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa kulingana na dalili ulizonazo baada ya kupata jeraha la kichwa.

Ili kujua iwapo umepata majeraha yoyote ya ubongo, madaktari wakati mwingine hufanya yafuatayo:

  • Uchanganuzi wa CT wa kichwa chako ili kuhakikisha kuwa ubongo wako hauvuji damu au haujavilia

Huenda usihitaji kipimo cha uchanganuzi wa CT ikiwa dalili zako zilitoweka ndani ya dakika chache baada ya kupata majeraha ya kichwa.

Je, madaktari wanatibu vipi jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa?

Daktari wako atakuelekeza:

  • Kupumzika

  • Umeze asetaminofeni ikiwa una maumivu ya kichwa

Usicheze michezo ya kugusana, inayokuweka katika hatari zaidi ya kupata jeraha la ubongo linalotokana na kupigwa/kugongwa, hadi daktari wako atakaposema kuwa majeraha yako ya kichwa yamepona kabisa na kwamba unaweza kurejea kucheza.