Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi ni nini?
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi ni jeraha ambapo sehemu ya mwili wako inaganda. Tishu zilizoganda hufa na haziwezi kuendelea kuishi. Baridi pia inaweza kuharibu tishu pasipo kuigandisha. Hii inaitwa jeraha la tishu lisiloganda.
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi unaweza kufanya ngozi yako ipate ganzi, iwe nyeupe, ivimbe, ipate malengelenge, au kuwa nyeusi na ngumu
Ukiwa na ugonjwa mkali wa kuganda tishu kwa jalidi, unaweza kupoteza sehemu za vidole vya mikono na miguu, pua, au masikio yako
Pasha sehemu zenye ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kwa maji ya vuguvugu
Usifikiche sehemu zenye ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi—unaweza kuharibu ngozi na tishu
Muone daktari mara moja iwapo unadhani kuwa una ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi.
Je, nini husababisha ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi?
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi hutokea pale halijoto ya baridi inapogandisha ngozi yako. Kwa ugonjwa mkali wa kuganda tishu kwa jalidi, tishu zilizo chini ya ngozi huganda pia.
Seli zozote zilizoganda zinakufa. Haziwezi kuishi tena baada ya kuyeyushwa. Tishu zilizokufa ni rahisi kuambukizwa
Seli zilizo karibu ambazo hazijagandishwa zinaweza kuharibiwa na baridi. Zinaweza kuishi ikiwa zitapata joto kwa haraka lakini bado zinaweza kufa hapo baadaye. Inaweza kuchukua muda mrefu kujua kama baadhi ya tishu zitaendelea kuishi.
Una hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi ikiwa utakaa nje wakati hali ya hewa ni ya baridi na:
Umelowa maji
Kuna upepo mkali
Unagusa metali
Una mtiririko dhaifu wa damu (kwa mfano, kwa sababu ya kisukari)
Glavu au buti zako zinakubana sana
Uso, mikono na masikio yako hayajafunikwa
Zipi ni dalili za ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi?
Sehemu zenye ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi huwa zimekufa ganzi na ukizigusa ni za baridi. Dalili nyingine hutegemea ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi umepenya kwa kiasi gani.
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kwenye sehemu ya juu: Doa jeupe la ngozi lililokufa ganzi ambalo hubanduka pale ngozi inapopata joto
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kwa kiasi: Malengelenge na kuvimba
Ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kwa kina: Ngozi nyeusi na ngumu (gangrini)
Sehemu yenye ugonjwa wa jalidi inapopata joto, huacha kufa ganzi na kuuma sana.
Ngozi yoyote nyeusi na ngumu hatimaye hubanduka na kudondoka. Wakati mwingine kidole chako chote au sikio hudondoka. Hili linaweza lisitokee kwa muda mrefu.
Baada ya ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kupona, mara nyingi sehemu hiyo ya mwili huathiriwa sana na baridi. Inaweza kubaki imekufa ganzi au ikiuma daima. Kucha za vidole vyako vya mikono na miguu zinaweza kuwa na mwonekano usio wa kawaida.
© Springer Science+Business Media
© Springer Science+Business Media
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi?
Madaktari wanaweza kufahamu ikiwa una ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi kwa kukufanyia uchunguzi. Wakati mwingine ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi mwanzo hufanana na jeraha la tishu lisilotokana na kuganda.
Je, madaktari wanatibu vipi ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi?
Kadri unavyowahi kupasha joto sehemu yenye ugonjwa wa jalidi, ndivyo bora zaidi. Ikiwa huwezi kufika hospitali mara moja:
Pasha joto mwili wako kwa kutumia blangeti lenye joto
Tumbukiza ngozi yako yenye ugonjwa wa jalidi kwenye maji ya uvuguvugu (kiasi cha joto la 100 to 104° F, or 40° C)
Nenda hospitali haraka iwezekanavyo
Maji ya uvuguvugu yatakuwa ni yenye joto linalofaa ikiwa mtu mwingine asiyekuwa na ugonjwa wa kuganda tishu kwa jalidi anaweza kutumbukiza mkono wake bila shida. Maji ya moto sana yataharibu ngozi yako zaidi.
Ikiwa miguu yako ni yenye ugonjwa wa jalidi na inakubidi utembee hadi kwenye eneo salama, ni afadhali usiyeyushe kwanza. Ni vibaya sana kutembea kwa miguu iliyoyeyushwa kuliko kutembea kwa miguu yenye ugonjwa wa jalidi. Na ni vibaya zaidi ikiwa miguu yako uliyoiyeyusha itaganda kwa mara ya pili.
Usifanye yafuatayo:
Kufikicha ngozi yako
Kuweka theluji kuzunguka sehemu yenye ugonjwa wa jalidi
Kupasha moto ngozi yako kwa kukaa mbele ya moto, au kwa kutumia pedi ya joto au blangeti la umeme kwa sababu ngozi yako iliyokufa ganzi haiwezi kuhisi kama joto ni kali sana
Madaktari watapasha moto sehemu yenye ugonjwa wa jalidi kwenye maji ya uvuguvugu na pia:
Watakupatia dawa za kupunguza maumivu
Watakupaka malai ya dawa za kuua bakteria kwenye malengelenge yaliyopasuka
Wataweka ngozi yako safi na kavu
Wakati mwingine watakupatia dawa ya kuboresha mtiririko wa damu au dawa za kuua bakteria ili kutibu maambukizi
Wakati mwignine watafanya upasuaji ili kukata na kuondoa ngozi iliyokufa au kukata sehemu ya mwili
Madaktari hujaribu kusubiri kwa kadiri wanavyoweza kabla ya kufanya upasuaji. Kusubiri huwafanya waone kama tishu zimekufa au kuharibiwa vibaya tu.