Kutoboka kwa Kiwambo cha Sikio

(Kiwambo cha Sikio Kilichotoboka; Kiwambo cha Sikio Kilichopasuka, Kiwambo cha Sikio)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024

Kiwambo cha sikio lako ni utando mwembaba (kama ngozi) ndani ya sikio lako. Umenyooka kwa kukaza kama kiwambo na unatetema sauti inapogonga. Mitetemo inakwenda kwenye sikio lako la kati na la ndani na inabadilishwa kuwa ishara za neva. Ishara za neva zinakwenda kwenye ubongo wako hivyo unasikia sauti. Kiwambo cha sikio lako pia huzuia maji na uchafu usiingie ili kulinda mifupa midogo ndani ya sikio lako.

Je, kutoboka kwa kiwambo cha sikio ni nini?

Ndani ya Sikio

Kutoboka kwa kiwambo cha sikio ni tundu lililo kwenye kiwambo cha sikio lako. Pia inaitwa kiwambo cha sikio kilichochanika.

  • Maambukizi ya sikio ni sababu kuu sana ya kutoboka kwa kiwambo cha sikio

  • Dalili zinajumuisha maumivu ya ghafula ya sikio na wakati wingine kuvuja damu kwenye sikio lako, kupoteza uwezo wa kusikia, au kelele kwenye sikio lako

  • Daktari wako anaweza kuona kutoboka kwa kiwambo cha sikio kwa kuangalia kwenye sikio lako kwa kutumia tochi ya mkononi

  • Kwa kawaida, kiwambo cha sikio kinapona chenyewe

Ni nini husababisha kutoboka kwa kiwambo cha sikio?

Sababu za kutoboka kwa kiwambo cha sikio hujumuisha:

  • Maambukizi ya sikio

  • Mabadiliko ya ghafula kwenye shinikizo (kama vile kutokana na mlipoko, kofi kwenye sikio lako, kupiga mbizi chini ya maji, au kupaa kwenye ndege)

  • Kuchokonoa sikio lako kwa kutumia kitu (kama vile pamba au penseli)

Wakati mwingine watu wanajaribu kuondoa uchafu wa kwenye sikio kwa kutumia pamba au vitu vingine, kama vile njiti ya kiberiti au penseli. Usifanye hivi, kwa sababu kwa sababu kufanya hivi kutasukuma uchafu kwenda ndani zaidi kwenye sikio lako na kitendo hiki kinaweza kujeruhi kiwambo cha sikio.

Dalili za kutoboka kwa kiwambo cha sikio ni zipi?

Dalili zako zinategemea kile kilichosababisha kutoboka huko.

Maambukizi ya sikio yanayotoboa sikio kimsingi yanapunguza maumivu ya maambukizi ya sikio. Maambukizi ya sikio yana maumivu kwa sababu kiowevu au usaha unajikusanya nyuma ya kiwambo cha sikio lako. Kiwambo cha sikio lako kinapopata shimo ndani yake (kinatoboka), usaha hutoka hivyo kupunguza maumivu.

Ikiwa shinikizo litabadilika au kuweka kitu kwenye sikio lako kilichosababisha kutoboka, utakuwa na:

  • Maumivu makali ya ghafla

  • Wakati mwingine kuvuja damu kidogo

Matatizo ya kutoboka kwa kiwambo cha sikio ni yapi?

Huenda usiwe na dalili au matatizo yoyote baada ya kutoboka kwa kiwambo cha sikio. Lakini baadhi ya watu:

  • Kupoteza uwezo wa kusikia

  • Wanasikia kelele kwenye masikio (kusikia kelele masikioni)

  • Hisia kama unazunguka au kujongea (kizunguzungu)

Ikiwa maji au uchafu utaingia kwenye tundu, unaweza kupata maambukizi ya sikio.

Daktari wangu atajuaje ikiwa nina hali ya kutoboka kwa kiwambo cha sikio?

Madaktari wanaweza kuona kutoboka kwa kiwambo cha sikio kwa kuangalia kwenye sikio lako kwa kutumia tochi ya mkononi. Wakati mwingine madaktari wanafanya kipimo cha kusikia kuona ikiwa kutoboka kumeathiri uwezo wako wa kusikia.

Madaktari hutibu vipi kutoboka kwa kiwambo cha sikio?

Unapaswa kuhakikisha sikio lako ni kavu, lakini huenda usihitaji matibabu mengine. Hali nyingi za kutoboka zinapona zenyewe.

Ikiwa kiwambo cha sikio lako hakitapona ndani ya miezi 2 au ikiwa ulipata jeraha baya la sikio, huenda ukahitaji upasuaji ili kurekebisha kiwambo cha sikio lako.